Mwanasayansi
na hisabati Blaise Pascal aliwahi kusema matatizo yote ya binadamu
yanatokana na mtu kushindwa kukaa mwenyewe kwenye chumba kwa utulivu.
Na
hili ni sahihi kabisa, kinachowafanya watu wengi kuingia kwenye
matatizo mbalimbali, ni kushindwa kutulia na mawazo yao, kukosa ujasiri
wa kukaa na kutafakari chochote walichonacho kwenye mawazo yao.
Mimi
nakwenda mbali na kusema kwamba watu wengi tunajiogopa sisi wenyewe.
Ndiyo maana tukikutana na upweke tu tunakimbia haraka sana.
Kama
unabisha jiangalie tu tabia yako, huwa unafanya nini pale unapojikuta
upo mwenyewe. Lazima utatafuta kitu cha kuchukua muda wako na kushika
mawazo yako. Labda utaanza kuchezea simu, utaanza kusoma kitu au hata kuwatafuta watu ambao hukuwa umepanga kuwatafuta.
Yote
hayo ni kuepuka tu kuwa peke yako, upweke umekuwa hofu kubwa kwetu,
hatutaki kabisa kukaa wenyewe, tukiwa tumeachwa na fikra zetu.
Rafiki, hebu acha kujiogopa, hebu rudisha urafiki kwako binafsi. Unapopata nafasi ya kuwa na upweke, itumie hiyo kuyatafakari maisha yako, itumie hiyo kujijengea taswira ya kule unakoenda.
Usijiogope
na kukimbia kila unapojikuta mpweke, badala yake tumia nafasi hiyo
kujenga urafiki na wewe binafsi na hata kujijua zaidi na kujua kwa kina
kule unakokwenda.