Tuesday, October 16, 2018

JE, TUWAPE WATOTO WETU SIMU ZETU ZA MKONONI WACHEZEE ??

14 Oktoba 2018, BBC  SWAHILI

  Simu yaweza kumsaidia mtoto kujifunza lakini bado nimuhimu kwa mzazi kuwa makini
Hivi karibuni imekuwa kawaida sana kumkuta mtoto anatumia simu ya mkononi ya mzazi wake na mara nyingine wanatumia bila hata kupata ridhaa ya mzazi mwenyewe.
Baadhi ya watoto huonyesha utaalamu wa hali ya juu katika kufungua kurasa mbalimbali za simu hizo.

Na inadaiwa kuwa kuna watoto ambao huwa wanajifunza mambo mengi kupitia simu za mkononi.
Hata hivyo si wazazi wote ambao hukubali simu zao zitumiwe na watoto, baadhi huwa wakali na kuweka kila aina ya nywila ingawa wengine huwa hawaoni shida kuwapatia watoto wao simu punde tu wanaporejea kutoka kwenye majukumu yao ya kila siku.

Baadhi ya wazazi huwa wanaona kuwa simu ndio njia pekee inayoweza kuwafanya watoto wao watulie na wao wapate muda wa kupumzika ama hata kufanya shughuli zao za nyumbani. 

Je,kuna faida yeyote endapo mtoto atatumia simu?
BBC imezungumza na baadhi ya wazazi ili kufahamu ni kwa kiasi gani watoto wao hutumia simu zao na wanawadhibiti vipi vitu anavyoangalia mtoto?

"Kwa kweli simu yangu hata sina uhuru nayo huwa nikifika tu nyumbani wanangu huwa wananipokea kwa mbwembwe zote na cha kwanza kubeba ni simu na nikihitaji lazima niwaombe wao.
Simu ikiita utakuta wao ndio wanapokea,mara nyingi wanaangalia video za kartoon au za watoto wenzao zilizopo you tube," Mama Brian anaeleza

Baadhi ya watoto hutambua hadi nywila za simu za wazazi wao
Alex Kayetta ambaye ni baba wa mtoto mmoja, anasema simu yake huwa haimiliki punde tu anapofika nyumbani ,
"Mwanangu akishashika simu yangu yani kuipata lazima nimbembeleze, na akichukua mara nyingine huwa lazima nimtafute alipo ,kuna siku nilimkuta amejificha ndani ya beseni akicheza michezo ya kwenye simu'game' nikampiga picha".

Freddie Kyara ni mwanasaikolojia kutoka nchini Tanzania ambaye anaeleza kuwa hali hii huwa inafanana na jinsi mzazi anapokua kwenye simu muda mrefu na hupoteza fursa ya kuwa karibu jamii na ndivyo hivyo inavyotokea kwa mtoto.

Na kwa upande wa mtoto kutumia simu huwa kuna madhara pia "Kukua kwa mtoto kunahitaji awe na mbinu za kijamii, kama vile kucheza na watoto wenzake na kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wenzake, lakini siku hizi unaweza kukuta mtoto anashindwa kucheza na watoto wengine kwa sababu amezoea yeye rafiki yake ni simu tu.

Ubunifu wa mtoto unaweza kupungua. Sisi wakati tunakuwa hatukuwa tunajua habari za simu, ilikuwa ni kucheza mpira na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za nyumbani na hali hiyo ilitufanya tuweze kujenga urafiki na watu na kujua tabia za watu tofautitofauti. 

Mtoto anaweza kujifunza pia kwenye simu lakini lazima uthibiti uwepo kwa sababu sio kila kilichopo kwenye simu kina maudhui mazuri kwa watoto na wanapaswa kutengewa muda" Kyara ,mtaalamu wa saikolojia alieleza.

Hata hivyo jumbe mbalimbali zimekuwa zikisambaa kuonya madhara ya mionzi ya simu kwa watoto wadogo na kudai kuwa umri sahihi wa kupewa simu ni kuanzia miaka kumi na sita.
Jambo ambalo Daktari Fredrick Mashili anasema madhara ya namna hiyo huwa inategemeana zaidi na umri wa mtoto japo kwa upande mwingine macho yanaweza kupata shida ingawa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madhara hayo ya mionzi.

"Kuna wasiwasi kwamba mtu akianza kutumia simu mapema anaongeza muda wa kuyashughulisha macho yake katika mionzi kwa muda mrefu zaidi kitu ambacho si kizuri kwa afya ya macho," Dkt.Mashili alieleza.


Friday, October 12, 2018

KILA MTU ANA NAMBA NA VIWANGO VYAKE KIFEDHA. HATUWEZI KULINGANA.

Linapokuja swala la fedha, kila mtu ana namba na viwango vyake. Kwa sababu tunatofautiana ndoto, kazi/biashara, kipato, mitindo ya maisha na hata mazingira, matokeo yetu ya kifedha hayawezi kulingana.

Hivyo kujipima hatua ulizopiga kifedha kwa kuwatumia wengine ni kujiumiza na hata kujirudisha nyuma, kwa sababu kuna namba nyingi ambazo utakuwa huzijui kuhusu wengine. Kwa mfano unaweza kumwona mtu kwa nje anaonekana kuwa na vitu vinavyoashiria ana fedha nyingi, lakini kumbe vitu vyote hivyo amepata kwa mkopo ambao ataulipa maisha yake yote.
Pia unaweza kumwona mtu ukafikiri hayupo vizuri kifedha kwa mwonekano wake wa nje, kumbe anafanya uwekezaji ambao baadaye utamwezesha kufikia uhuru wa kifedha.

Kwa kuwa ni vigumu kupima hatua ulizopiga kifedha kwa kuwatumia watu wengine, unahitaji kujitumia wewe mwenyewe.

UTOAJI WA FEDHA KWA WENGINE BILA KUTEGEMEA KUPATA CHOCHOTE NI MUHIMU SANA.

Kiasi cha fedha unachotoa kwa wengine bila ya kutegemea kupata chochote ni kiwango kingine muhimu sana cha kupima afya yako kifedha na kujua hatua ulizopiga. Kwa kadiri unavyotoa zaidi ndivyo unavyoonesha kwamba unaitumia fedha na siyo fedha inakutumia wewe.

Unahitaji kuwa na utaratibu wa kutoa fedha kuwasaidia wengine bila ya kutegemea kulipwa fedha hizo. Kwa sababu tunatoshelezwa zaidi na utoaji kuliko upokeaji.

Pia unapotoa fedha kwa wengine, unatengeneza pengo ambalo itabidi lizibwe, hivyo unakuwa umejiweka kwenye nafasi ya kuongeza kipato chako zaidi.

WEKA AKIBA ILI USIINGIE KWENYE MADENI MABAYA NA CHANGAMOTO ZA MAISHA.


Hichi ni kiwango kinachoonesha maandalizi yako uliyonayo sasa kwa upande wa fedha. Kadiri unavyokuwa na akiba kubwa kifedha, ndivyo unavyoweza kujilinda na dharura mbalimbali zinazoweza kukutokea. Akiba unayokuwa nayo ndiyo itakukinga usiingie kwenye madeni mabaya pale unapokutana na changamoto ambazo hukuzitegemea.

Kiwango sahihi cha akiba unayopaswa kuwa nayo ni ile inayoweza kutosheleza kuendesha maisha yako kwa miezi 6 mpaka mwaka mmoja hata kama utakuwa huna kipato kabisa katika kipindi hicho.

Kuza kiwango chako cha akiba na hili litakupa pumziko na kukuondolea wasiwasi kuhusu fedha kitu ambacho kitakuwezesha kufanya mambo yako kwa utulivu na ufanisi mkubwa.

EPUKA MADENI ILI KUEPUKA KUJIWEKA KWENYE WAKATI MGUMU KIFEDHA.

Kiasi cha fedha unachodaiwa na wengine kutokana na vitu ulivyonunua bila ya kuwa na fedha ni kipimo cha maamuzi yako ya kifedha kwa siku za nyuma. Kadiri madeni yako yanavyokuwa makubwa, ndivyo sehemu kubwa ya kipato chako inavyoelekea kwenye kulipa madeni hayo na wewe kubaki na kiasi kidogo ambacho hakiwezi kukutosheleza.

Unahitaji kutokuwa na deni binafsi kabisa, na madeni mazuri unayopaswa kuwa nayo ni yale yanayojilipa yenyewe. Madeni yanayojilipa yenyewe ni yale ambayo yanazalisha faida na faida hiyo unatumia kulipa deni. Haya ni madeni ambayo hayakuumizi.

Lakini madeni ambayo unalipa kwa fedha zako unazopata kwenye shughuli zako binafsi, ni utumwa ambao utakutesa kwa muda mrefu. Kama upo kwenye madeni ya aina hii kazana kuondoka na usiingie tena ili kuepuka kujiweka kwenye wakati mgumu kifedha.

WEKEZA SASA KWA AJILI YA BAADAYE , WAKATI UNA NGUVU ZA KUFANYA KAZI.

Kiwango ambacho umekiwekeza kwenye maeneo ambayo yanazalisha riba au faida ni kipimo muhimu kwa maandalizi yako ya kifedha ya baadaye. Kama hapo ulipo hujafanya uwekezaji wote kwa ajili ya baadaye, kama hujawa na maandalizi ya kukuwezesha kuingiza kipato bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja, huna maandalizi ya kifedha ya baadaye, na haupo eneo zuri kifedha.

Unahitaji kufanya uwekezaji kwa ajili ya baadaye, kwa sababu utakuja wakati ambapo huna uwezo wa kufanya kazi kama unavyofanya sasa, lakini una mahitaji muhimu kwa maisha yako. Unapokuwa umewekeza na uwekezaji unazalisha, maisha yako yanakwenda vizuri.

Kiwango sahihi cha uwekezaji unachopaswa kuwa nacho ni kile ambacho kinazalisha faida au riba ambayo inakuwezesha wewe kuendesha maisha yako kwa kadiri ya mahitaji yako.

Wednesday, October 10, 2018

TATIZO NI TAFSIRI YA MATUKIO YANAYOTUTOKEA.

Watu wawili wanaweza kushindwa kwenye kitu kimoja, mmoja akachukulia kushindwa huko kama kichocheo cha kufanya zaidi na akafanikiwa. Mwingine anaweza kuchukulia kushindwa huko kama sababu ya kukata tamaa na kushindwa kabisa.

Tukio ni moja, tafsiri tofauti na matokeo tofauti kabisa.
Siyo kinachotokea, bali namna unavyotafsiri kinachotokea ndiyo inaleta madhara kwako.
Kwenye Falsafa ya Ustoa pia kuna dhana inayoitwa upili wa udhibiti. Dhana hii inaeleza kwamba vitu vyote vinavyotokea kwenye maisha yako, vinagawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni vitu unavyoweza kuviathiri, hivi vipo ndani ya uwezo wako. Kundi la pili ni vitu usivyoweza kuviathiri, hivi vipo nje ya uwezo wako.

Hivyo unapokutana na chochote na ukajiambia ni kigumu au kinakushinda, huna haja ya kusumbuka, badala yake jiulize je kipo ndani ya uwezo wako au nje ya uwezo wako. Kama kipo ndani ya uwezo wako chukua hatua sahihi, kama kipo nje ya uwezo wako kikubali kama kilivyo au kipuuze. Hakuna namna bora ya kuendesha maisha yako kama hii, kwa sababu hakuna chochote kitakachotokea, ambacho kitakuvuruga kabisa.

Ndugu  yangu , nikukumbushe tena ya kwamba kama unataka kuitawala dunia, kuna mtu mmoja unayepaswa kumtawala, na mtu huyo ni wewe mwenyewe. Hutaweza kujitawala wewe mwenyewe kwa mabavu au nguvu, badala yake utajitawala kwa kudhibiti mawazo yako na hisia zako.