Sunday, October 7, 2018

KABLA YA KULALA IPIME SIKU YAKO

Kila siku tunayoishi ni nafasi nzuri kwetu kuwa bora zaidi, kwa sababu kuna mengi tunakutana nayo ya kujifunza, kuna makosa tunayoyafanya na yapo mazuri tunayafanya pia. Wengi wamekuwa wanakosa nafasi ya kuzitumia siku zao kuwa bora zaidi kwa sababu hawapati muda wa kutafakari kila siku yao.
Kupitia Ustoa, tunashauriwa kuipima na kutafakari kila siku yetu kabla ya kulala. Na hapa ndipo tunapata nafasi ya kujifunza na kujiandaa kuwa bora zaidi kwenye siku inayofuata.
Jioni unapoimaliza siku yako, usikimbilie tu kulala na kuona siku imeisha, badala yake unahitaji kuwa na tahajudi ambayo utaipitia siku yako yote.
Kwenye tahajudi hii, pitia siku yako nzima, kwa kufikiria kila ulichofanya kwenye siku yako, kila uliyekutana naye na mawazo na hisia ulizokuwa nazo siku nzima.
Kisha jiulize na kujijibu maswali haya matatu;
Moja; vitu gani umefanya vibaya? Katika yale uliyofanya kwa siku nzima, je vitu gani umefanya kwa ubaya au kwa njia ambazo siyo sahihi?
Mbili; vitu gani umefanya vizuri? Katika vitu vyote ulivyofanya kwa siku nzima, vipi ambavyo umevifanya kwa uzuri, ni kwa namna gani umeishi misingi na tabia za ustoa?
Tatu; Vitu gani utakwenda kufanya tofauti? Ni vitu gani unahitaji kuvifanya kwa utofauti ili kuweza kuishi kulingana na msingi na tabia za ustoa?
Kwa kujiuliza na kujipa majibu ya maswali hayo matatu, utaweza kujipima kwa kila siku yako, na pia kujiandaa vyema kwa siku inayofuata. Pia utaepuka kurudia makosa uliyofanya kwa siku husika.
Kauli ya Epictetus kwenye tahajudi ya jioni;
“Allow not sleep to close your wearied eyes, Until you have reckoned up each daytime deed: “Where did I go wrong? What did I do? And what duty’s left undone?” From first to last review your acts and then Reprove yourself for wretched [or cowardly] acts, but rejoice in those done well.”
(Discourses, 3.10.2–3)
Anasema usikubali usingizi ufumbe macho yako kabla hujahesabu kila tendo ulilofanya kwenye siku yako. kipi umekosea, kipi umefanya vizuri na kipi ambacho hujakamilisha. Kuanzia tendo la kwanza mpaka la mwisho, jikaripie kwa yale uliyofanya vibaya na jisifie kwa yale uliyofanya vizuri.

TEGEMEA KUKUTANA NA WATU WABAYA KATIKA MAISHA YAKO YA KILA SIKU

Huwa tunazianza siku zetu tukitegemea kutekeleza yale tuliyopanga na kufanya mambo makubwa sana. Lakini siku zetu zimekuwa haziendi kama ambayo tumepanga, yamekuwa yanatokea mambo ambayo hatukutegemea yatokee, hasa kwa wale ambao tulitegemea wafanye vitu fulani na wasifanye.

Hili limekuwa linawanyima wengi furaha, lakini kwa falsafa ya ustoa, hupaswi kukosa furaha kwa mambo kama hayo, kwa sababu unapaswa kuyategemea yakitokea kabla hata hayajatokea.
Mstoa Marcus Aurelius ana hili la kutuambia pale tunapoianza siku yetu;
“Say to yourself first thing in the morning: I shall meet with people who are meddling, ungrateful, violent, treacherous, envious, and unsociable. They are subject to these faults because of their ignorance of what is good and bad.” (Meditations, 2.1)
Jiambie unakwenda kuianza siku ambayo utakutana na watu wachafu, wasio na shukrani, wenye fujo, wasaliti, wenye wivu na wasiojali mambo ya wengine. Na wanafanya mambo hayo kwa sababu hawajui mazuri na mabaya.
Kwa kuianza asubuhi yako kwa tafakari yenye nguvu namna hii, hakuna chochote kitakachokutokea ambacho kitakushangaza, maana ulishakitegemea.

WHAT IS A HAPPY LIFE ??

Kauli ya Seneca kuhusu kuishi kwa furaha;

“What is a happy life? It is peacefulness and lasting tranquillity, the sources of which are a great spirit and a steady determination to hold fast to good decisions. How does one arrive at these things? By recognizing the truth in all its completeness, by maintaining order, moderation and appropriateness in one’s actions, by having a will which is always well-intentioned and generous, focused on reason and never deviating from it, as lovable as it is admirable.” – Seneca, Letters, 92.3

Seneca anauliza maisha ya furaha maana yake nini? Ni maisha ambayo yana amani na utulivu, ambayo chanzo chake ni imani kuu na maamuzi ya kushikilia maamuzi sahihi. Na je mtu anawezaje kufikia hili? Ni kwa kugundua ukweli kamili, kwa kuenda kulingana na mipango, kuwa na kiasi katika matendo na kuwa na nia njema na ukarimu, kuongozwa na fikra sahihi na kutokupotoka.

FALSAFA YA USTOA NI NINI ???

USTOA ni falsafa ya matendo, ni falsafa ambayo imelenga kumwezesha mtu kuwa na maisha bora, kwa kufikiri sahihi na kuchukua hatua sahihi kwenye maisha yake. Falsafa ya ustoa siyo kama falsafa nyingine za kubishana na kutaka kuonekana unajua zaidi, badala yake ni falsafa ya kufikiri sahihi na kuchukua hatua sahihi. Falsafa ya ustoa inalenga kudhibiti hisia zetu na kuishi kulingana na asili. Kwa njia hiyo, tunakuwa na maisha bora wakati wote.

Falsafa ya ustoa ilianzishwa na Zeno wa Citium miaka ya 301 K.K na baadaye kupokelewa na kukuzwa na wanafalsafa Cato, Seneca, Epictetus na Marcus Aurelius. Hawa wote ni wanafalsafa walioishi zaidi ya miaka 2000 iliyopita, wakati wa utawala wa Roma.

Saturday, September 22, 2018

KILA MTU APAMBANE NA HALI YAKE,USINUNUE MATATAIZO YA WATU.

Chukua mfano una ndugu wa karibu au mtoto ambaye bado hajaweza kutengeneza maisha yake vizuri, lakini wewe maisha yako yameshakaa vizuri. Yeye hana kazi na ni mlevi. Hivyo unaamua kumsaidia awe na kipato, kwa sababu maisha yake siyo mazuri. Unampa mtaji wa kuanzisha biashara, anatumia vibaya na biashara inakufa. Unaona kwa kuwa una uwezo, basi unaweza kuwa unampa fedha ya kujikimu, lakini ukimpa fedha anaenda kulewa. Unakwama, usipompa fedha maisha yake yanakuwa magumu na unaonekana umemtenga ndugu yako, ukimpa anaenda kulewa na kuzitumia vibaya.

Wawezeshe watu kutatua matatizo yao wenyewe, na usisukumwe kufanya vitu kwa sababu unataka kuonekana una roho nzuri. Wale utakaowawezesha kutatua matatizo yao, utawasaidia hata wakati wewe haupo. Ila wale unaobeba matatizo yao, utawaandaa kuanguka vibaya pale ambapo wewe hutakuwepo. Na nikukumbushe tu, haijalishi unampenda mtu kiasi gani, hutakuwa naye kwa maisha yako yote, hivyo mpende kwa kumfanya aweze kutatua matatizo yake mwenyewe.

Katika kukazana kwetu kuwasaidia wengine, hasa wale wa karibu kwetu, watoto, wenza, ndugu tuliozaliwa nao, tumekuwa tunakazana kuwaibia matatizo yao. Tunayachukua kabisa matatizo yao na kuyafanyia kazi na wao wanabaki hawana cha kufanya.



Hii ni njia mbovu sana ya kutaka kumsaidia mtu, kwa sababu unakuwa humsaidii, badala yake unamsababishia matatizo zaidi. Kwa sababu unapomchukulia matatizo yake, anabaki hana cha kufanya, hivyo anaenda kutengeneza matatizo zaidi.

Kwa sababu ukikimbilia kuyabeba ili uonekane una roho nzuri, utaishia kumharibu zaidi yule mwenye matatizo. Kwa sababu maisha yetu yanatoa maana kwenye matatizo na changamoto tunazokutana nazo mara kwa mara na kuzitatua.

Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

Friday, September 21, 2018

JE, WAIJUA AKAUNTI YA FEDHA YA SAIKOLOJIA ?

Unahitaji kujizoesha kifikra na kisaikolojia kuwa na fedha nyingi, hata kama bado hujazishika kwenye mikono yako au kuwa nazo kwenye akaunti yako ya benki. Na unaweza kuanza kwa kufikiria mara kumi ya kipato unachopata sasa, kisha kufikiria kipato hicho mara kwa mara, kukiwekea mipango na kuweka lengo lako la kipato liwe ni kukua kufikia mara kumi ya kipato chako cha sasa. Kwa njia hii utaongeza kiwango chako cha fedha kisaikolojia.

 Watu wengi wanajua aina moja ya akaunti ya kifedha, ambayo ni akaunti ya benki, au akiba na uwekezaji ambao wamekuwa wamefanya. Hivyo ukitaka kuangalia utajiri wa mtu, unaangalia ni kiasi gani cha fedha anacho kwenye akaunti zake za benki na uwekezaji kiasi gani amefanya.

 Aina ya pili ya akaunti ya kifedha, ukiacha akaunti ya benki, ni akaunti ya fedha ya kisaikolojia. Kila mmoja wetu, ana kiwango chake cha kifedha kwenye fikra zake, ambacho ndiyo ameshajiambia anapaswa kupata kiwango hicho. Yaani kila mmoja wetu, kuna kiwango chake cha fedha, ambacho ameshakiweka kwenye fikra na mawazo yake, na akishapata kiwango hicho basi akili yake inatulia na hakazani tena kupata fedha zaidi.

Waangalie watu wote ambao wamepata fedha nyingi kwa mkupuo, kiasi kikubwa cha fedha ambacho hawajawahi kukishika kwenye maisha yao. Waangalie watu ambao wameshinda bahati nasibu, waangalie watu ambao wamerithi mali, waangalie watu ambao wamepokea mafao. Wengi haiwachukui muda wanakuwa wameshapoteza fedha nyingi walizopata na kurudi kwenye maisha yao ya kawaida.
Wanakuwa wamepata fedha nyingi kwenye akaunti ya benki, lakini akaunti yao ya kisaikolojia inasoma kiwango cha chini. Hivyo wanaacha kufikiria kabisa kuhusu fedha, wanaanza kupoteza fedha, mpaka zinapofika kwenye kile kiwango chao cha kisaikolojia ndiyo wanastuka na kuanza kufikiria kuhusu fedha.

 Pia unaweza kufikiria mara 100, mara 1000 na hata zaidi ya kipato unachopata sasa. Fikra zote hizo zitaiandaa akili yako kupokea fedha zaidi na kuweza kutulia na fedha zaidi unazopata. Unapofikiria mara elfu moja ya kipato unachopata sasa, ongezeko kidogo halitakusumbua kama linavyokusumbua sasa.


Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com

Sunday, September 16, 2018

JE, WAJUA NJIA ZA KUONGEZA THAMANI YA MAISHA YA WATEJA WAKO ?? JIFUNZE HAPA .

Wateja wako wanapokaa na wewe kwa muda mrefu ndivyo unavyonufaika zaidi. Hivyo unahitaji kuweka juhudi kuhakikisha wateja wanabaki na wewe kwa muda mrefu. Yafuatayo ni mambo muhimu ya kuzingatia ili wateja wakae na wewe kwa muda mrefu.

  1. Toa huduma bora sana kwa wateja wako, ambazo hawawezi kuzipata sehemu nyingine yoyote ila kwako tu.
  2. Kutengeneza mahusiano mazuri na wateja wako, wafanye wateja kuwa rafiki kwako na kwa biashara yako, waone siyo tu wanakuja kununua, bali wanakuja kwa rafiki yao, anayewajali na kuwapa kile kilicho sahihi kwao.
  3. Weka mbele maslahi ya wateja wako na siyo faida unayotaka kupata.
  4. Waelimishe wateja wako, washauri vizuri, hata kama utapoteza mauzo, lakini hilo litawajengea imani zaidi na hivyo kuendelea kununua zaidi.
  5. Wafanye wateja wako kuwa mashabiki wa biashara yako.
Zipo hatua saba ambazo wateja wanapitia mpaka kufikia ngazi ya ushabiki.

Hatua ya kwanza ni wapitaji tu, wanaisikia au kiona biashara yako lakini hawajawahi kuuliza chochote.

Hatua ya pili ni wateja tarajiwa, wamesikia na wamefuatilia kutaka kujua zaidi kuhusu biashara yako.

Hatua ya tatu ni wanunuaji, hapa wamejua, wakafuatilia na wakajaribu kununua kile unachouza.

Hatua ya nne ni wateja, hapa mtu amejaribu kununua kwa mara ya kwanza, na amerudi tena kununua. Mtu kununua mara moja haimfanyi kuwa mteja, na wala haikufanyi wewe kuwa mjanja. Ni mpaka mtu atakaporudi tena kununua ndiyo utajua umefanya kazi nzuri.

Hatua ya tano ni mwanachama, hapa mteja anakuwa mnunuaji wa mara kwa mara na unaweza kumpa manufaa ya kadiri anavyonunua. Labda akifika kiwango fulani anapata zawadi, au akinunua mara tano, ya sita anapata bure. Hapa mwanachama anakuwa na kielelezo cha kuonesha idadi ya manunuzi yake.

Hatua ya sita ni mtetezi wa biashara yako, hapa mteja anakuwa tayari kuwaambia watu wengine kuhusu biashara yako, anatoa shuhuda kwa wengine na hasiti kuwaalika wengi waje kununua.
Hatua ya saba ni shabiki kindakindaki, hawa ni wale wateja ambao hawaambiwi chochote kuhusu biashara yako, yaani wao wameshachukulia biashara yako kama sehemu ya maisha yako. Hawa ni wateja ambao wanaiongelea biashara yako muda wote, na wakikutana na mtu ambaye hanunui kwako wanaona anakosa kitu kikubwa sana.
Katika kuboresha thamani ya maisha ya wateja wako, kazana kuwapandisha wateja wako ngazi mpaka wafikie kiwango cha watetezi na mashabiki wa biashara yako.
 
Na  Mwl  Japhet  Masatu , Dar  es  salaam , Tanzania,  Afrika Ya  Mashariki ---Mwl  wa  Maisha Na  Mafanikio, Mshauri, Public Speaker(MC), Mwandishi, Mjasiriamali /
Tuwasiliane kwa :+ 255 755 400 128 / + 255 716 924136(WhatsApp ).  EMAIL: japhetmasatu@gmail.com