Rafiki yangu mpendwa,
Nimekuwa
naamini na kusema hili mara kwa mara na nilirudie tena hapa, kukosa
mtaji siyo sababu ya kushindwa kuingia kwenye biashara. Ni kisingizio
tu.
Sasa visingizio vyote huwa ni vya uongo, kwa sababu vinaficha kile ambacho mtu hataki kukikabili.
Wengi
wanaotumia kisingizio cha mtaji, hawapo tayari kuukabili ukweli kwamba
ni wavivu, wazembe, wasio tayari kujitoa na wanaopenda mazoea. Ni vigumu
sana mtu kukiri una tabia hizo, hivyo kisingizio cha mtaji au muda
kinakuwa rahisi.
Kwa
zama tunazoishi sasa, hakuna kinachoweza kumzuia mtu aliyejitoa kweli
kuingia kwenye biashara. Siyo wazo, siyo mtaji na wala siyo muda.
Kinachomzuia mtu hakitoki nje, bali kipo ndani yake.
Na yule ambaye hana kizuizi cha ndani, anaweza kuyafanya makubwa mno.
Chukua mfano wa biashara ya genge la mahitaji muhimu ya kila siku kwenye familia.
Ni biashara yenye uhitaji, kwa sababu watu kila siku wanakula.
Ni biashara unayoweza kuanza kwa mtaji kidogo.
Ni biashara ambayo huhitaji kuwa na eneo la gharama kubwa kuifanyia.
Na ni biashara ambayo haina vitu vingi, hivyo unaweza kuisimamia vizuri.
Hii
ni biashara ambayo mtu ambaye hana shughuli nyingine ya kufanya anaweza
kuianzisha, akaiendesha vizuri na ikawa sehemu ya yeye kupiga hatua na
kuelekea kwenye biashara kubwa zaidi.
Unapochagua
kufanya biashara kama hii, unapaswa kuifanya kwa tofauti, ili ikue na
kuweza kuzalisha biashara nyingine kubwa zaidi.
Huenda
unawajua wauza genge ambao miaka yote unawaona wakiwa pale pale. Siyo
kwamba biashara hailipi, ila wanaifanya kwa viwango vya chini.
Kwenye
makala hii unakwenda kujifunza jinsi ya kuifanya biashara ya genge kwa
viwango vya juu sana na ikawa na manufaa makubwa kwako.
Kabla hatujaingia kwenye ushauri, tusome aliyotuandikia msomaji mwenzetu aliyeomba ushauri kwenye hili.
“Nahitaji
kufungua genge la matunda na mboga mboga napenda kuelimishwa namna ya
kuboresha iliniweze kukuza biashara yangu na wateja wavutiwe na huduma
yangu.” – Hussein B. M.
I. MAONO MAKUBWA.
Anza
kidogo lakini fikiri kwa ukubwa. Japo unafanya biashara ya genge,
kwenye fikra zako usione genge, bali ona biashara kubwa kabisa.
Ona ukiwa na maduka mengi ya kuuza mahitaji hayo ya msingi na ona ukifanya kwa kiwango kikubwa zaidi.
Ni maono makubwa unayokuwa nayo ndiyo yanakusukuma kupiga hatua kubwa pia.
Tunapata kile tunachoona, hivyo kuwa na maono makubwa na jisukume kuyafikia.
II. BIDHAA BORA.
Kwenye
biashara ya genge wateja wanaangalia vitu vikuu viwili, bidhaa bora na
kwa bei nafuu. Pambana kuwapatia wateja vitu hivyo viwili na watakuwa
wako kwa muda mrefu.
Chagua bidhaa zilizo bora kabisa ndiyo uweke kwenye biashara yako.
Jua maeneo unayoweza kupata bidhaa hiyo bora kwa bei nafuu ili pia uweze kuwauzia wateja wako kwa bei nzuri.
Jiwekee viwango vya ubora wa bidhaa utakazouza ili wateja waweze kujenga imani kwako na kwa biashara yako.
III. ENEO ZURI.
Biashara yako inapaswa kuwa eneo ambalo ni rahisi kuwafikia wateja wako na hata wateja kuifikia pia.
Kwa kuwa unachouza ni mahitaji muhimu ya maisha ya kila siku, biashara itafanya vizuri pale inapokuwa eneo lenye watu wengi.
Lakini pia mazingira ya eneo lako la biashara yanapaswa kuwa safi na mazuri, yamfanye mteja aiamini na kuithamini biashara yako.
Wengi
wanaofanya biashara ya genge hawaweki maeneo yao ya biashara kwenye
mwonekano mzuri, ukifanyia kazi hilo unajitofautisha kabisa na wengine.
IV. HUDUMA BORA KWA WATEJA.
Wahudumie
vizuri saba wateja wako ili waweze kurudi tena na tena. Wasikilize kwa
umakini na wajali pia. Jua mahitaji yao na uwatimizie.
Usiuze tu na kuishia hapo, jenga mahusiano mazuri na wateja wako na hayo yataiwezesha biashara kukua zaidi.
Pale wateja wanapopata huduma nzuri, wanaendelea kuja na wanawaleta wengine pia.
V. KUWEKA MAFUNGU.
Unayajua
mahitaji ya wateja wako, unaweza kutengeneza mafungu ya vitu
vinavyonunuliwa kwa pamoja na kisha kumshawishi mteja anunue kama fungu
badala ya kununua kimoja kimoja.
Kumsukuma kuchukua hatua, hakikisha bei ya fungu inakuwa na unafuu kuliko mteja akinunua kimoja kimoja.
Njia hii itakuwezesha kuuza zaidi kwa wateja ambao tayari unao, ambao ni wateja wazuri tayari.
VI. KUWAFIKIA WATEJA.
Usisubiri
tu wateja waje, badala yake watuate kule walipo. Watu sasa wametingwa
na mambo mengi wanaweza kusahau kabisa hata uwepo wako.
Hivyo watembelee wateja wako maeneo walipo na kuwashawishi kuja kununua.
Hapa pia unaweza kutoa huduma ya mteja kuagiza na kupelekewa bidhaa zake.
Na
kama umeziweka bidhaa kwa mafungu na bidhaa zako ni bora, mteja
anaagiza na kupelekewa, akijua anapata anachotaka na ambacho ni bora
pia.
VII. KUWASILIANA NA WATEJA.
Omba mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao mara kwa mara.
Unajua
wateja wa genge wanapanga mahitaji yao ya siku asubuhi. Unaweza
kuwatumia ujumbe asubuhi kuwasalimia na kuwaomba oda pia. Mteja
anapopata ujumbe wako, anakufikiria kwa muda mrefu na hilo linamshawishi
kuja kununua kwako.
Tumia kila sababu na ushawishi kupata mawasiliano ya wateja wako na wasiliana nao kwa njia ambayo siyo ya usumbufu kwako.
VIII. KUWEKA AKIBA.
Kwa
lengo lako la kufika kwenye mafanikio makubwa kibiashara, unapaswa
kuweka akiba kwenye kila faida unayoingiza kwenye biashara yako.
Wakati biashara inafanya vizuri, usibweteke na kuona mambo yataenda hivyo wakati wote.
Weka akiba ambayo itakusaidia wakati biashara haiendi vizuri.
Akiba hiyo ndiyo itakusaidia kwenye ukuaji wa biashara yako.
IX. KUKUZA BIASHARA.
Kwa kuwa una maono makubwa ya biashara yako, kila wakati angalia fursa za ukuaji zaidi.
Kila wakati piga hatua kuikuza biashara yako zaidi.
X. KUJIFUNZA KILA SIKU.
Kujifunza kila siku ni hitaji muhimu la ukuaji wa biashara yako.
Kila siku hakikisha unajifunza kitu kwenye kuikuza biashara yako.
Biashara inahitaji ubobezi maeneo mbalimbali kama masoko, mauzo, fedha, ushawishi na uongozi.
Soma vitabu mbalimbali vya biashara yako na unayojifunza yafanyie kazi.