Zama tunazoishi sasa ni zama ngumu mno ambapo mtu usipokuwa na msingi imara utaishia kuanguka vibaya.
Fursa ni nyingi mno, lakini nyingi siyo fursa za kweli.
Fursa hizo zinahamasisha na kutamanisha kwa sababu unaona kabisa wengine wakinufaika nazo.
Kumbe hiyo ni sehemu ya mtego wa kukunasa ili uweze kuingia kwenye fursa hizo na utapeliwe.
Siku
chache zilizopita nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama
msomaji ambaye amekuwa anafuatilia kazi zangu kwa muda mrefu.
Akaendelea
kueleza kwamba kuna fursa nzuri angependa kunishirikisha. Ana watu
anaofahamiana nao ambao wako nchi za nje na wapo tayari kumfadhili kiasi
kikubwa cha fedha (mabilioni) ila hajui afanye nini.
Hivyo
anataka tushirikiane, tuandike mradi wa mabilioni na kuwatumia hao watu
wake na wapo tayari kutoa fedha hizo kama mradi ukionekana ni mzuri.
Kama tukifanya hivyo na mimi nitakuwa sehemu ya mradi huo na hivyo kunufaika nao.
Baada
ya kumsikiliza akijieleza kwenye hayo nilimjibu HAPANA, SITAWEZA.
Alionekana kushangaa kwa nini nakataa fursa kubwa hivyo. Nikamwambia
atafute watu wengine.
Rafiki,
kama kwa kusoma hapo umeshangaa iweje nikatae fursa kubwa ya mabilioni,
kama umeiona hiyo ni fursa basi jua wewe ni rahisi sana kutapeliwa.
Kwenye
makala hii nitakushirikisha mbinu za kuwajua matapeli na fursa zao za
kukunasa ili uepuke kutapeliwa. Kisha mwisho nitakuonesha utapeli ulio
kwenye hiyo 'fursa' niliyoshirikishwa.
(1). UTAINGIZA PESA BILA KUFANYA KAZI.
Kiashiria
cha kwanza cha utapeli ni ahadi kwamba utaingiza pesa bila kufanya kazi
yoyote ile. Na katika maelezo ya fursa husika, huoni jinsi fedha
unayoweka inakwenda kufanya kazi.
Wewe
unaambiwa tu weka kiasi fulani na baadaye utavuna faida kubwa. Huelezwi
jinsi gani fedha hiyo uliyoweka inakwenda kuzalisha thamani ambayo
ndiyo inaleta faida.
Rafiki,
hii dunia imekuwepo kwa miaka mingi na katika kipindi chote hicho
pamoja na wagunduzi wakubwa waliowahi kuishi, haijawahi kujulikana njia
ya kupata pesa bila kufanya kazi, bila kuzalisha thamani kubwa kwa
wengine.
Hivyo
usidhani wewe una akili sana kuweza kujua fursa za aina hiyo, kama
unaambiwa weka tu fedha na uje uvune faida, hapo kuna utapeli.
(2). UNAELEZWA FAIDA TU ,HUELEZWI HASARA.
Kila kazi, biashara na hata uwekezaji huwa una faida na hasara.
Ukipata kazi inayolipa sana inakunyima muda kabisa. Ukipata kazi inayokupa muda haikulipi vizuri.
Huwezi
kupanda shamba la mahindi au maharage na mbegu zote ulizoweka zikaota
na kuzaa vizuri, haijawahi kutokea hata kwa sayansi ya juu kiasi gani.
Hivyo ndivyo asili ilivyo na ndivyo itaendelea kuwepo. Kuna faida na hasara, kuna kupata na kupoteza. Iko hivyo.
Wanaokuja
kwako na fursa za kitapeli wanakueleza kitu kimoja tu, faida. Hadithi
zao zimetengenezwa vizuri mno kiasi kwamba ukizisikiliza unaona pesa nje
nje.
Umewahi
kusikia hadithi za kulima matikiti au mapapai na ukapigiwa hesabu ya
heka moja inaingia miche mingapi na kila mche unatoa matunda mangapi na
ukapigiwa bei ya kila tunda ukauona utajiri si ndiyo huu?
Nenda shambani ndiyo utakutana na asili isiyokuwa na huruma na ndiyo utaelewa kwamba umetapeliwa.
(3). UNAONESHWA MIFANO YA WACHACHE WALIOFANIKIWA.
Ni vizuri kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, lakini ni vizuri zaidi kujifunza kutoka kwa walioshindwa.
Maana huwa unafundishwa siri nyingi za mafanikio, ila kubwa kabisa moja umekuwa hufundishwi, ambayo ni; BAHATI.
Ndiyo, kuna wengi ambao wamefanikiwa kwa bahati tu, japo wanaweza wasijue hilo na wakaona ni ujanja au juhudi zao.
Kama
watu 100 wanafanya kitu kimoja, kwa namna moja na eneo moja, halafu
mmoja akafanikiwa huku 99 wakishindwa, mafanikio ya mtu huyo ni bahati
zaidi kuliko juhudi binafsi.
Matapeli
huwa wana mifano michache ya watu waliotumia njia zao wakafanikiwa
lakini huwa wanaficha mifano ya wengi waliotumia njia zao na wakashindwa
vibaya.
Hivyo
unapopewa hadithi za waliofanikiwa, usikimbilie kuziamini kwa sababu
wanaonekana wazi, bali kazichimbe zaidi na ona kama kuna kitu cha
tofauti kimewawezesha kufanikiwa. Angalia wengine wengi ambak pia
walikuwa wanafanya kama wao lakini hawajafanikiwa.
Tenganisha bahati na juhudi ili uweze kujua kweli kinacholeta mafanikio.
4. Unapaswa kuchukua hatua haraka la sivyo utaikosa fursa.
Fursa za kitapeli huwa hazitaki upate muda wa kutafakari kitu, hivyo unalazimishwa uchukue hatua haraka la sivyo utaikosa fursa.
Huwa
wanafanya hivyo kwa makusudi, wakati wanakuambia kuhusu fursa, wanaibua
hisia kali za tamaa ndani yako na tamaa ikishakuwa juu ni rahisi kwako
kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Hilo ndiyo wanataka.
Wanajua ukipata muda hisia zako zitashuka, utaweza kufikiri kwa usahihi na utaona utapeli ulio kwenye fursa husika.
Richard Branson amewahi kusema fursa ni kama daladala, ukikosa moja jua kuna nyingine inakuja.
Hivyo
unapoelezwa kuhusu fursa yoyote ile, jibu lako la kwanza linapaswa kuwa
ni wakupe muda uifikirie na kuitafiti kwa kina. Ukiona wanakuambia
unapaswa kuchukua hatua sasa au hupaswi kufikiria sana kwa sababu kuna
wengine waliofanikiwa tayari wameichukua fursa hiyo, jua hapo kuna
utapeli, kaa mbali.
(5 ). UNALAZIMISHWA UPTAE MANUFAA.
Tangu
kugunduliwa kwa fedha na kutumika kama njia ya kubadilishana thamani,
hakuna mtu amewahi kutaka mtu mwingine apate fedha kuliko yeye.
Ndiyo maana ukienda kununua kitu na ukaambiwa bei, huwa unauliza kama kuna punguzo.
Ukipewa kazi na kutajiwa malipo, huwa unaomba upewe nyongeza.
Sasa anakuja mtu kwako, ambaye hata siyo ndugu au rafiki yako, ila ana fursa nzuri kwako ya kukuwezesha kupata fedha nyingi.
Unapokuwa humuelewi anaonekana kuumia sana kwa sababu anaona jinsi unavyokosa fedha nyingi.
Na wewe unaamini na kuingia kwenye mtego huo.
Huwa nasema ukiona mtu anakulazimishia sana fursa, jua wewe ndiyo fursa kwake.
Hakuna anayekupenda sana kwenye fedha kiasi cha kuumia pale anapoona huchangamkii fursa.
Swali jingine la kujiuliza kwa hao waleta fursa, je ndugu zao na watu wao wa karibu wameshawapa fursa hiyo ili wanufaike?
Jibu huwa ni hapana, sasa wanawezaje kukupenda wewe mtu wasiyekujua kuliko wanavyowapenda watu wao wa karibu?
Umeshapata jibu hapo, hawawezi kuwatapeli watu wa karibu.
( 6 )KILA MTU ANAIZUNGUMZIA FURSA.
Ukishaanza kusikia kila mtu anazungumzia kitu fulani ni fursa nzuri, jua tayari umeshachelewa.
Hata kama fursa ni ya kweli kabisa, kama unaisikia kwa kila mtu, dirisha la kunufaika kwa kiwango kikubwa limeshakupita.
Inakuwa imebaki kuwa fursa kwa wale wapiga debe ambao wanashawishi wengine wajiunge na fursa hiyo maana wao ndiyo watanufaika.
Na hapa ndipo njama kubwa ya utapeli unaofanana na ukweli inapotengenezwa.
Chukua
mfano wa fursa kama ya sungura. Mtu anaanza kufuga sungura kwenye
mazingira ambayo ufugaji wa sungura siyo wa kiwango kikubwa.
Kwa kuwa upatikanaji ni mdogo, uhitaji unakuwa mkubwa.
Hivyo mtu huyo anaweza kuuza sana kwa sababu hakuna mwingine anayezalisha kama yeye.
Na hapo anaanza kutangaza hiyo ni fursa nzuri na inayolipa.
Anakuonesha wazi kwamba uhitaji upo, soko lipo na faida ni nzuri.
Wewe
kwa kuona hivyo unashawishika kuingia kwenye fursa, sasa basi mbegu
utanunua kwake, chakula kwake, madawa kwake na ushauri mwingine kutoka
kwake.
Mpaka
inakuja kufika wakati wa kwenda sokoni, unakuta wenzako wengi
walioingia kama wewe nao wanapeleka bidhaa sokoni. Upatikanaji unakuwa
mkubwa kuliko uhitaji na bei inapungua sana.
Unajipa moyo ni soko halijakaa vizuri, usichoweza kukiri ni umetapeliwa kwa njama ya hali ya juu kabisa.
Rafiki
yangu mpendwa, umepata mwanga mkubwa kuhusu utapeli kwa haya
niliyokushirikisha hapa. Haya ni ya msingi kabisa na ambayo huwa yako
wazi kwenye kila aina ya utapeli kama utatumia fikra zako badala ya
hisia zako kufanya maamuzi.
Ili uepuke kuingia kwenye utapeli mbalimbali, endelea kujifunza na kujijenga kuwa imara.
Ndimi KOCHA MWL. JAPHET MASATU , DAR ES SALAAM ,
WhatsApp + 255 716924136 /