Tuesday, June 1, 2021

JISUKUME UANZE LEO , UJITOSE LEO , UMALIZE LEO UTAREKEBISHA MBELE YA SAFARI

Imekuwa ni jambo rahisi kwa watu wengi kughairisha vitu nami nikiwa mmojawapo ya watu ambao nimewahi kupitia hali za kughairisha vitu na baadaye ikawa ni ngumu kufanya tena. Kughairisha kunafariji pale ambapo kitu ulichopaswa kufanya wakati huo unakisogeza mbele au kusema nitafanya baadaye na hilo kushindwa kulifanya. Kughairisha kumeiba ndoto zetu na zimefanya tusiishi kitoshelevu wakati ambao tulikuwa na nafasi ya kufanya.

Unapoghairisha mambo unavuta hali ya kuzembea kuanza kitu ambacho kilikuwa kinawezekana kuanza. Unapofika wakati ujao kile ulichofikiria ungekianza kinaanza kuwa kigumu kukifanya na kadri muda uendavyo unapata ukinzani mkubwa zaidi na hilo linafanya usifanye chochote kile. Wakati unaofaa kuanza kufanya kitu ni wakati huo huo unaosema siwezi sasa nifanye baadaye.

Mara nyingi tunapotaka kuanza kitu basi ndani yetu tunapata sauti ambazo zinatufanya tujishauri kuwa ngoja nitafanya wakati mwingine si sasa. Ile nafasi ya kuamua sasa inapopotea ndivyo wakati unaokuja baadaye inakuwa ngumu kweli kweli kuanzisha kitu. Au wakati mwingine gharama ya jambo ambalo ungelifanya sasa inaweza kuwa mara mbili kwa baadaye. Kumbe kuanzisha kitu sasa kunasaidia kupata matokeo ya haraka zaidi kuliko kujichelewesha.

Kila kitu katika maisha kinahitaji safari na kadri unavyojishauri usianze kufanya kitu ndivyo unavyochelewa katika safari ya kitu hicho. Utakuwa umekutana na watu ambao walikuwa na nafasi ya kuanzisha biashara mapema wakiwa na nguvu ila wanangoja hadi wanapostaafu ndo wanataka kuanzisha biashara ambapo kupata mafanikio kunakuwa kugumu kuliko wale ambao walianza mapema wakaujua mchezo wa biashara na kujua namna ya kuendesha biashara. Unapochelewa kuanza kitu ndivyo unavyochelewa kujifunza mengi zaidi juu ya hicho kitu.

Kuna faida tele za kuanza sasa, wakati ambao wengine wanasema wataanza baadaye wewe jisukume uanze leo, umalize leo na ujitose leo maana muda utakapopita utakuwa upo mbali sana kuliko wengine. Unapojifunza kuchukua hatua leo ndivyo unavyoweza kufanikiwa mapema katika maisha.

Ndimi   Rafiki  Yako

 KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM, TANZANIA

WhatsApp + 255 716 924 136 /  + 255 755 400  128 /   0688 361 539  /  +255 629 748 937

EMAIL :   japhetmasatu@gmail.com

 

KILA TATIZO HATA LIWE KUBWA KIASI GANI LITAPITA TU NA KUSAHAU VUTA TU SUBIRA.

Maisha hupokezana kwa mambo nayo huja na kupita. Yote haya yanakuja ili kutupima na kutufungua akili ilivyo wazi kuwa hakuna jambo zito kubwa kuliko lingine. Mambo mazito tunayapa majina pale ambapo hatuoni njia namna gani tuweze kutoka au kupata suluhisho.

Suluhisho ni njia ambayo jambo lilokuwa likionekana ni zito na gumu kuwa jepesi. Ugumu wa maisha ni pale ambapo tunakutana na nyakati ambazo mbele yetu hatuoni njia, hatuoni nafasi ya kushinda au hatuoni upenyo wa kupita. Magumu huja kutufundisha kuna njia nyingi unazoweza kuzitumia kupita gumu lolote linapojitokeza.

Nyakati ngumu zinazojitokeza mara kwa mara katika maisha yetu haziji kutudumaza bali kutuchangamsha akili tufikiri zaidi, tujichunguze na kutafakari namna ya kuvuka. Changamoto zinapojitokeza hazituachi namna tulivyo awali bali zinatuimarisha na kujigundua kuwa tuna uwezo mkubwa zaidi wa kuvuka vikwazo na kilichokuwa kinatukwamisha ni kihunzi kidogo cha kuruka tu.

Mtu ambaye mara kwa mara anakutana na changamoto na kuzishinda anajitengenezea uimara na uzoefu unaompa nafasi ya kukabiliana na jambo lolote linaloweza kujitokeza katika safari ya maisha. Wale ambao huwa tunawaona wamefanikiwa kwa kitu fulani iwe ni biashara, uongozi, elimu na mahusiano basi moja kwa moja utakuta wamekuwa ni washindi wa changamoto nyingi ambazo zimewakuta.

Changamoto zinazompata mtu zinaweza kuzaliwa katika ugeni wa mambo kunakoweza kuchangiwa na uhafifu wa maarifa, uzoefu na utambuzi. Changamoto zinaumiza pale ambapo mtu anakutana na uhalisia unaovunja kuona kwake kitu katika hali alofikiria ingekuwa hivyo. Hili limepelekea changamoto ziwaangushe wengine, waanguke katika walichokianzisha na kufeli kabisa katika hatua ambazo walikusudia wangeweza kuvuka.

Muda hutusaidia kupisha changamoto ambazo huwa tunapitia. Ukitulia na kufikiria maisha yako utaona kuna nyakati ambazo uliwahi pitia changamoto nyingi na ukafikiria huenda zingekumaliza au zisingeisha na kupita. Ila muda ukazipitisha na kuzigeuza leo yawe mafunzo na kukufanya uwe imara zaidi. Hili ndivyo linavyotokea katika maisha kuwa kila kitu ambacho unakiona ni kizito si kizito kiuhalisia kitakuwa chepesi kadri muda unavyopita na kukivunja vunja kiwe hakina nguvu tena kama ya awali.

Ndimi  Rafiki   yako 

KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA

WhatsApp + 255 716924136  /  + 255 755 400128

 

Thursday, May 20, 2021

MATAPELI NI WENGI SANA JIFUNZE MBINU ZAO NA UWAKIMBIE NA FURSA ZAO FEKI KAMA UKOMA.

Zama tunazoishi sasa ni zama ngumu mno ambapo mtu usipokuwa na msingi imara utaishia kuanguka vibaya.

Fursa ni nyingi mno, lakini nyingi siyo fursa za kweli.

Fursa hizo zinahamasisha na kutamanisha kwa sababu unaona kabisa wengine wakinufaika nazo.

Kumbe hiyo ni sehemu ya mtego wa kukunasa ili uweze kuingia kwenye fursa hizo na utapeliwe.

Siku chache zilizopita nilipokea simu kutoka kwa mtu aliyejitambulisha kama msomaji ambaye amekuwa anafuatilia kazi zangu kwa muda mrefu.

Akaendelea kueleza kwamba kuna fursa nzuri angependa kunishirikisha. Ana watu anaofahamiana nao ambao wako nchi za nje na wapo tayari kumfadhili kiasi kikubwa cha fedha (mabilioni) ila hajui afanye nini.

Hivyo anataka tushirikiane, tuandike mradi wa mabilioni na kuwatumia hao watu wake na wapo tayari kutoa fedha hizo kama mradi ukionekana ni mzuri.

Kama tukifanya hivyo na mimi nitakuwa sehemu ya mradi huo na hivyo kunufaika nao.

Baada ya kumsikiliza akijieleza kwenye hayo nilimjibu HAPANA, SITAWEZA. Alionekana kushangaa kwa nini nakataa fursa kubwa hivyo. Nikamwambia atafute watu wengine.

Rafiki, kama kwa kusoma hapo umeshangaa iweje nikatae fursa kubwa ya mabilioni, kama umeiona hiyo ni fursa basi jua wewe ni rahisi sana kutapeliwa.

Kwenye makala hii nitakushirikisha mbinu za kuwajua matapeli na fursa zao za kukunasa ili uepuke kutapeliwa. Kisha mwisho nitakuonesha utapeli ulio kwenye hiyo 'fursa' niliyoshirikishwa.

(1). UTAINGIZA  PESA  BILA  KUFANYA  KAZI.

Kiashiria cha kwanza cha utapeli ni ahadi kwamba utaingiza pesa bila kufanya kazi yoyote ile. Na katika maelezo ya fursa husika, huoni jinsi fedha unayoweka inakwenda kufanya kazi.

Wewe unaambiwa tu weka kiasi fulani na baadaye utavuna faida kubwa. Huelezwi jinsi gani fedha hiyo uliyoweka inakwenda kuzalisha thamani ambayo ndiyo inaleta faida.

Rafiki, hii dunia imekuwepo kwa miaka mingi na katika kipindi chote hicho pamoja na wagunduzi wakubwa waliowahi kuishi, haijawahi kujulikana njia ya kupata pesa bila kufanya kazi, bila kuzalisha thamani kubwa kwa wengine.

Hivyo usidhani wewe una akili sana kuweza kujua fursa za aina hiyo, kama unaambiwa weka tu fedha na uje uvune faida, hapo kuna utapeli.

(2). UNAELEZWA  FAIDA  TU ,HUELEZWI    HASARA.

Kila kazi, biashara na hata uwekezaji huwa una faida na hasara.

Ukipata kazi inayolipa sana inakunyima muda kabisa. Ukipata kazi inayokupa muda haikulipi vizuri.

Huwezi kupanda shamba la mahindi au maharage na mbegu zote ulizoweka zikaota na kuzaa vizuri, haijawahi kutokea hata kwa sayansi ya juu kiasi gani.

Hivyo ndivyo asili ilivyo na ndivyo itaendelea kuwepo. Kuna faida na hasara, kuna kupata na kupoteza. Iko hivyo.

Wanaokuja kwako na fursa za kitapeli wanakueleza kitu kimoja tu, faida. Hadithi zao zimetengenezwa vizuri mno kiasi kwamba ukizisikiliza unaona pesa nje nje.

Umewahi kusikia hadithi za kulima matikiti au mapapai na ukapigiwa hesabu ya heka moja inaingia miche mingapi na kila mche unatoa matunda mangapi na ukapigiwa bei ya kila tunda ukauona utajiri si ndiyo huu?

Nenda shambani ndiyo utakutana na asili isiyokuwa na huruma na ndiyo utaelewa kwamba umetapeliwa.

(3). UNAONESHWA  MIFANO  YA  WACHACHE  WALIOFANIKIWA.

Ni vizuri kujifunza kutoka kwa waliofanikiwa, lakini ni vizuri zaidi kujifunza kutoka kwa walioshindwa.

Maana huwa unafundishwa siri nyingi za mafanikio, ila kubwa kabisa moja umekuwa hufundishwi, ambayo ni; BAHATI.

Ndiyo, kuna wengi ambao wamefanikiwa kwa bahati tu, japo wanaweza wasijue hilo na wakaona ni ujanja au juhudi zao.

Kama watu 100 wanafanya kitu kimoja, kwa namna moja na eneo moja, halafu mmoja akafanikiwa huku 99 wakishindwa, mafanikio ya mtu huyo ni bahati zaidi kuliko juhudi binafsi.

Matapeli huwa wana mifano michache ya watu waliotumia njia zao wakafanikiwa lakini huwa wanaficha mifano ya wengi waliotumia njia zao na wakashindwa vibaya.

Hivyo unapopewa hadithi za waliofanikiwa, usikimbilie kuziamini kwa sababu wanaonekana wazi, bali kazichimbe zaidi na ona kama kuna kitu cha tofauti kimewawezesha kufanikiwa. Angalia wengine wengi ambak pia walikuwa wanafanya kama wao lakini hawajafanikiwa.

Tenganisha bahati na juhudi ili uweze kujua kweli kinacholeta mafanikio.

4. Unapaswa kuchukua hatua haraka la sivyo utaikosa fursa.

Fursa za kitapeli huwa hazitaki upate muda wa kutafakari kitu, hivyo unalazimishwa uchukue hatua haraka la sivyo utaikosa fursa.

Huwa wanafanya hivyo kwa makusudi, wakati wanakuambia kuhusu fursa, wanaibua hisia kali za tamaa ndani yako na tamaa ikishakuwa juu ni rahisi kwako kufanya maamuzi yasiyo sahihi. Hilo ndiyo wanataka.

Wanajua ukipata muda hisia zako zitashuka, utaweza kufikiri kwa usahihi na utaona utapeli ulio kwenye fursa husika.

Richard Branson amewahi kusema fursa ni kama daladala, ukikosa moja jua kuna nyingine inakuja.

Hivyo unapoelezwa kuhusu fursa yoyote ile, jibu lako la kwanza linapaswa kuwa ni wakupe muda uifikirie na kuitafiti kwa kina. Ukiona wanakuambia unapaswa kuchukua hatua sasa au hupaswi kufikiria sana kwa sababu kuna wengine waliofanikiwa tayari wameichukua fursa hiyo, jua hapo kuna utapeli, kaa mbali.

(5 ). UNALAZIMISHWA   UPTAE  MANUFAA.

Tangu kugunduliwa kwa fedha na kutumika kama njia ya kubadilishana thamani, hakuna mtu amewahi kutaka mtu mwingine apate fedha kuliko yeye.

Ndiyo maana ukienda kununua kitu na ukaambiwa bei, huwa unauliza kama kuna punguzo.

Ukipewa kazi na kutajiwa malipo, huwa unaomba upewe nyongeza.

Sasa anakuja mtu kwako, ambaye hata siyo ndugu au rafiki yako, ila ana fursa nzuri kwako ya kukuwezesha kupata fedha nyingi.

Unapokuwa humuelewi anaonekana kuumia sana kwa sababu anaona jinsi unavyokosa fedha nyingi.

Na wewe unaamini na kuingia kwenye mtego huo.

Huwa nasema ukiona mtu anakulazimishia sana fursa, jua wewe ndiyo fursa kwake.

Hakuna anayekupenda sana kwenye fedha kiasi cha kuumia pale anapoona huchangamkii fursa.

Swali jingine la kujiuliza kwa hao waleta fursa, je ndugu zao na watu wao wa karibu wameshawapa fursa hiyo ili wanufaike?

Jibu huwa ni hapana, sasa wanawezaje kukupenda wewe mtu wasiyekujua kuliko wanavyowapenda watu wao wa karibu?

Umeshapata jibu hapo, hawawezi kuwatapeli watu wa karibu.

 ( 6 )KILA   MTU  ANAIZUNGUMZIA  FURSA.

Ukishaanza kusikia kila mtu anazungumzia kitu fulani ni fursa nzuri, jua tayari umeshachelewa.

Hata kama fursa ni ya kweli kabisa, kama unaisikia kwa kila mtu, dirisha la kunufaika kwa kiwango kikubwa limeshakupita.

Inakuwa imebaki kuwa fursa kwa wale wapiga debe ambao wanashawishi wengine wajiunge na fursa hiyo maana wao ndiyo watanufaika.

Na hapa ndipo njama kubwa ya utapeli unaofanana na ukweli inapotengenezwa.

Chukua mfano wa fursa kama ya sungura. Mtu anaanza kufuga sungura kwenye mazingira ambayo ufugaji wa sungura siyo wa kiwango kikubwa.

Kwa kuwa upatikanaji ni mdogo, uhitaji unakuwa mkubwa.

Hivyo mtu huyo anaweza kuuza sana kwa sababu hakuna mwingine anayezalisha kama yeye.

Na hapo anaanza kutangaza hiyo ni fursa nzuri na inayolipa.

Anakuonesha wazi kwamba uhitaji upo, soko lipo na faida ni nzuri.

Wewe kwa kuona hivyo unashawishika kuingia kwenye fursa, sasa basi mbegu utanunua kwake, chakula kwake, madawa kwake na ushauri mwingine kutoka kwake.

Mpaka inakuja kufika wakati wa kwenda sokoni, unakuta wenzako wengi walioingia kama wewe nao wanapeleka bidhaa sokoni. Upatikanaji unakuwa mkubwa kuliko uhitaji na bei inapungua sana.

Unajipa moyo ni soko halijakaa vizuri, usichoweza kukiri ni umetapeliwa kwa njama ya hali ya juu kabisa.

Rafiki yangu mpendwa, umepata mwanga mkubwa kuhusu utapeli kwa haya niliyokushirikisha hapa. Haya ni ya msingi kabisa na ambayo huwa yako wazi kwenye kila aina ya utapeli kama utatumia fikra zako badala ya hisia zako kufanya maamuzi.

Ili uepuke kuingia kwenye utapeli mbalimbali, endelea kujifunza na kujijenga kuwa imara.

Ndimi  KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES SALAAM , 

WhatsApp + 255 716924136 / 

 

Saturday, May 15, 2021

NAFASI YA BAHATI KATIKA MAFANIKIO----NA MUNGA TEHENAN---( PDF )

JIFUNZE IMANI SAHIHI ITAKAYOKUSAIDIA ULIPWE ZAIDI. USITEGEMEE MSHAHARA PEKEE UTAKUFA MASKINI.

 Sio siri tena kwenye hii karne ya 21,

Mambo yamebadilika sana.

Sahau kila kitu ulichowahi kusikia kuhusu kulipwa.

Sasa kuna njia bora ya kulipwa zaidi kuliko ilivyokuwa imezoeleka karne ya 20.

Ni njia ambayo haizungumzwi sana lakini inafanya kazi kwenye hii karne ya 21.

Haijalishi umeajiriwa au umejiajiri,

Inafanya kazi kwenye hali zote mbili.

Ukweli ni kwamba,

Kwa sasa haulipwi kutokana na masaa unayofanya kazi,

Bali unalipwa kulingana na matokeo unayozalisha.

Unapozalisha matokeo makubwa zaidi unalipwa kiasi kikubwa cha fedha.

Unapozalisha matokeo madogo zaidi unalipwa kiasi kidogo cha fedha.

Angalia huu u tofauti hapa chini,

Kuhusu imani walizonazo matajiri na masikini kuhusu kulipwa.

Matajiri huwa wanachagua kulipwa kwa matokeo wanayozalisha na hapo wanazalisha matokeo makubwa zaidi na kulipwa kiasi kikubwa cha fedha.

Masikini wanachagua kulipwa kwa muda wanaotumia kufanya kitu na kwa kuwa muda una ukomo,

Wanajiwekea ukomo kwenye kipato chao.

Matajiri wote wamepata utajiri wao kupitia njia ambazo hazitegemei muda wao.

Kwa mfano kumiliki biashara inayojiendesha yenyewe ,

Kufanya uwekezaji maeneo yanayozalisha na kadhalika.

Kulipwa kwa muda ni kupitia mshahara au huduma binafsi ambazo mtu anatoza gharama kwa muda.

Hakuna mtu amewahi kufikia utajiri mkubwa kwenye maisha yake kwa kutegemea mshahara pekee.

Hata mshahara uwe mkubwa kiasi gani, bado unakuwa na ukomo.

Na mbaya zaidi, kadiri mshahara unavyokuwa mkubwa, ndivyo makato yanavyokuwa makubwa pia.

Kulipwa kwa muda ni kujiwekea ukomo na kanuni ya kwanza na muhimu kwenye fedha ni kuhakikisha huweki ukomo kwenye kipato chako.

Chagua kulipwa kwa matokeo na thamani unayozalisha ambayo haina ukomo,

Badala ya kutaka ulipwe kwa muda ambao una ukomo.

Je, ungependa ulipwe zaidi kwa kile unachofanya?

Kama ni ndio, KARIBU  UJIUNGE , " DARASA ONLINE "

Ujifunze njia na hatua za kuchukua ili ulipwe zaidi.

Utajiri ni mchezo,

Mchezo ambao una kanuni zake na sheria zake,

Na ili uweze kushinda mchezo huu,

 Lazima uzijue kanuni na uzishike sheria.

Haiwezekani kabisa kwa mtu ambaye hajui kanuni za mpira wa miguu,

Hana mazoezi akaenda uwanjani na kushinda.

Wengi wamekuwa wanaingia kwenye mchezo wa utajiri kama vile ni kitu cha kubahatisha,

Hawajui kanuni wala sheria,

Hawana maandalizi na kinachotokea ni kushindwa vibaya sana.

Karibu sana  UJIUNGE  " DARASA  ONLINE " UJIFUNZE  TABIA ZA KITAJIRI ILI  KUFIKIA  MAFANIKIO  MAKUBWA.

Ujifunze kwa kina na kuyaelewa maarifa haya muhimu sana kwako,

 Kisha uchukue hatua ili maisha yako yaweze kubadilika, ufike kwenye utajiri, mafanikio na furaha.

 

TUWASILANE  SASA, 

Ndimi  Rafiki   yako

Kocha  Mwl  Japhet  Masatu , Dar es  salaam , Tanzania.

 (WhatsApp + 255 716 924136 ) / + 255 755 400128  / + 255 688  361  539 / + 255 629748 937

EMAIL : japhetmasatu@gmail.com