Mafanikio yetu yanajengwa au kubomolewa na tabia tunazoziishi kila siku.
Siku zetu zinaendeshwa zaidi na tabia ambazo tayari tumeshajijengea.
Ndiyo maana huwa unasikia huwa tunajenga tabia na kisha tabia zinatujenga.
Kwa siku 30 za mwezi, unakwenda kufanya jaribio la kuziishi tabia 10 ninazokwenda kukushirikisha hapa.
Kila siku kamilisha tabia hizo kumi bila kuacha hata siku moja, kisha siku 30 zinapoisha, jifanyie tathmini ya mabadiliko unayoyaona kwenye maisha yako.
TABIA KUMI ZA KUISHI KWA SIKU 30.
1. Kila siku amka mapema, saa moja kabla ya muda wako uliozoea kuamka. Ukishaamka usiangalie simu wala usumbufu wowote, bali anza kwa kufanya sala na/au tahajudi (meditation) kisha chukua notebook yako na andika vipaumbele vya siku hiyo, mambo ambayo utakwenda kufanyia kazi (To Do List). Hayo ndiyo mambo utakayoyapa kipaumbele kwenye siku yako, usifanye mengine kabla hayo hayajaisha.
2. Kila siku fanya mazoezi kwa dakika zisizopungua 30, mazoezi mazuri ni ya kukimbia.
3. Kila siku soma kitabu kwa angalau dakika 30, chagua kitabu chochote unachotaka kusoma, iwe ni cha maendeleo binafsi au maendeleo ya kitaaluma kisha soma kwa angalau dakika 30 kila siku.
4. Kila siku pangilia na dhibiti ulaji wako, punguza kabisa vyakula vya wanga na sukari, kula mboga mboga na matunda kwa wingi, kula nyama kwa kiasi na kunywa maji mengi. Pia dhibiti sana vilevi unavyotumia.
5. Kila siku mpigie simu mteja mmoja ambaye amewahi kunufaika na biashara au kazi yako na ongea naye kuhusiana na biashara au kazi yako na changamoto alizonazo unazoweza kumsaidia kutatua. Pia mpigie mteja tarajiwa mmoja, ambaye bado hajanunua ila ana uhitaji ambao unaweza kumsaidia, mwoneshe jinsi unavyoweza kutatua tatizo lake.
6. Kila siku mpigie simu mtu mmoja wa karibu, ndugu jamaa na marafiki na kuwa na maongezi naye ya kuboresha mahusiano yenu.
7. Kila siku jaribu kitu kipya na ambacho umekuwa unahofia kufanya au umekuwa unaona huwezi, hata kama ni kidogo, fanya. Hii inajenga ujasiri wako na kukuwezesha kuvuka hofu.
8. Kila siku kuwa na fikra chanya, fikra za mafanikio na utajiri mkubwa. Pata muda wa kuwa peke yako na jenga taswira ya ndoto kubwa ulizonazo, jione kama tayari umeshazifikia na amini ni kitu ambacho tayari kipo. Jenga taswira hii kwenye fikra zako na pia kuwa na picha ya ndoto ulizonazo unayotembea nayo au iliyo kwenye simu yako na iangalie mara kwa mara.
9. Kwa kila kipato unachoingiza, iwe ni kwa siku, wiki au mwezi, weka pembeni angalau asilimia kumi ya kipato hicho na iweke mahali ambapo huwezi kuitumia. Fedha ya ziada unayoipata ambayo hukuitegemea, yote iweke kwenye fungu hilo.
10. Kila siku unapoimaliza siku yako, jipe muda wa kutafakari jinsi siku hiyo ilivyokwenda. Jua yapi umefanya vizuri, yapi umekosea na wapi unapaswa kuboresha zaidi. Andika kwenye notebook yako yale uliyojifunza kwenye tafakari hiyo ya jioni. Kwa kufanya tafakari hii kila siku, utaendelea kuwa bora zaidi kwa kila siku mpya unayokwenda kuanza.
Rafiki, ni mambo hayo kumi tu ya kufanya kila siku kwa siku 30 bila kuacha hata siku moja, kisha siku 30 zikiisha jifanyie tathmini, kama matokeo ni mazuri fanya hiyo kuwa sehemu ya maisha yako.
NA KOCHA MWL. JAPHET MASATU