( 1 ).FEDHA SIYO MAKARATASI.
Watu
wengi wamekuwa wanafikiria fedha ni yale makaratasi au sarafu ambazo
tunazishika. Na hapa ndipo wengi wanapokwama, kwa sababu wanakosa ule
msingi muhimu kuhusu fedha. Kwa kukosa msingi muhimu kuhusu fedha, watu
wanashindwa kuzipata kwa wingi na hata kuzitumia vizuri.
Fedha
ni wazo ambalo lina thamani. Fedha ni matokeo ya mtu kuwa na wazo
ambalo linaongeza thamani kwa wengine. Bila ya thamani hakuna fedha.
Hivyo kama unataka fedha zaidi, lazima ujue thamani gani unatoa kwa
wengine.
( 2 ).KIPATO KIMOJA NI UTUMWA.
Kuwa
na chanzo kimoja cha kipato pekee ni utumwa. Huwezi kuondoka kwenye
umasikini kama unategemea kipato chako kitoke sehemu moja pekee. Kama
umeajiriwa pekee, hata kama unalipwa kiasi kikubwa cha fedha, bado
unabaki kwenye umasikini. Kama unafanya biashara na unategemea wateja
wachache nayo pia inakuweka kwenye umasikini.
Utaondoka
kwenye umasikini kwa kuwa na vyanzo vingi vya kipato. Bahari huwa
haikauki kwa sababu mito mingi inaishia kwenye bahari. Hiyo kama unataka
usikaukiwe na fedha, kuwa na vyanzo vingi vya kipato.
(3) MATUMIZI NI BOMU.
Watu
wengi wamekuwa wanaanza maisha na kipato kidogo, na yanaenda. Kipato
kinaongezeka na matumizi yanaongezeka, kila kipato kinapoongezeka na
matumizi pia yanaongezeka. Matumizi ni bomu kama hayatadhibitiwa.
Matumizi yana tabia ya kuongezeka pale tu kipato kinapoongezeka.
Huwezi
kuondoka kwenye umasikini kama huwezi kuyadhibiti matumizi yako.
Haijalishi unatengeneza kipato kikubwa kiasi gani, matumizi ni bomu,
usipolitegua litakulipua.
( 4 ).MADENI NI UTUMWA.
Umesikia
hapo, na najua huenda kimoyomoyo unakataa, unajiambia siyo kweli, kwa
sababu huenda umeshalishwa sumu kwamba bila madeni maisha hayawezi
kwenda. Unajua nini, wale wanaonufaika na madeni ndiyo wanasambaza
propaganda za aina hiyo. Madeni ni utumwa, na huwezi kuondoka kwenye
umasikini kama huwezi kuondokana na madeni.
Kuna
madeni mazuri na mabaya, na masikini wote huwa wapo kwenye madeni
mabaya. Madeni mabaya ndiyo yanawafanya watu kuwa watumwa, wanajikuta
wanafanya kazi sana kulipa madeni, halafu wanakopa tena. Kwa hiyo maisha
yao yote yanakuwa mzunguko wa kopa, lipa, kopa tena.
( 5 ).BIASHARA NI MKOMBOZI.
Zile
zama za nenda shule, soma kwa bidii, faulu na utapata kazi nzuri na
inayolipa zimeshapitwa na wakati. Kila mtu anaona wingi wa watu wenye
sifa za kuajiriwa, lakini hakuna nafasi za ajira. Na hata walioajiriwa,
mazingira ya kazi na hata kipato wanachoingiza hakiridhishi.
Kwa
zama tunazoishi sasa, mkombozi pekee, kitu pekee kitakachokuwezesha
kuwa na maisha mazuri ni kuwa na biashara yako. Hivyo ni muhimu sana uwe
na biashara kama unataka kutoka kwenye umasikini.
( 6 ). UWEKEZAJI NI KIJAKAZI WAKO.
Inapokuja
kwenye fedha, kuna mambo mawili, kuna kuifanyia kazi fedha, pale ambapo
inabidi ufanye kazi ndiyo fedha iingie. Halafu kuna fedha kukufanyia
kazi wewe, ambapo fedha inaingia hata kama hufanyi kazi moja kwa moja.
Ili
kuondoka kwenye umasikini na kufikia uhuru wa kifedha, ni lazima fedha
ziwe zinakufanyia kazi wewe. Na hapa ndipo unapohitaji kuwa na
uwekezaji, ambao unafanya kazi ya kuuzalishia fedha, hata kama wewe
umelala.
( 7 ). KODI NI UWEKEZAJI.
Kodi
ni gharama unayolipa kwa kuishi kwenye jamii iliyostaarabika. Ni kodi
tunazolipa ndiyo zinazoleta huduma mbalimbali tunazozitegemea kwenye
jamii. Huduma za afya, huduma za elimu, ulinzi na usalama, miundombinu
kama barabara na mengineyo ni matokeo ya kodi tunazolipa.
Hivyo
kodi ni uwekezaji ambao kila mmoja wetu anapaswa kuufanya ili tuwe na
jamii bora. Tunapaswa kuondokana na dhana potofu kwamba kodi ni kitu
kibaya. Kwa sababu hebu pata picha, umekazana kutafuta fedha na ukawa
tajiri, halafu unaishi sehemu isiyo salama, je utaweza kufurahia utajiri
wako?
( 8 ).BIMA NI MKOMBOZI.
Kuna
hatari mbalimbali ambazo zinatuzunguka kwenye maisha, na kadiri
unavyopiga hatua kifedha, ndivyo hatari zinakuwa kubwa zaidi. Hili
limekuwa linazua hofu kwa wengi na wakati mwingine kuwazuia hata
kufanikiwa.
Ili
kuondokana na hatari zinazokuzunguka na kukuzuia kuanguka pale
unapokutana na changamoto kubwa, unapaswa kuwa na bima. Kwa bima
unachangia kiasi kidogo cha fedha, lakini unapopata tatizo, unalipwa
kiasi kamili cha fedha au mali ulizopoteza.
( 9 ). WATOTO WAKO HAWAHITAJI FEDHA ZAKO.
Wazazi
wengi wamekuwa wanakazana kutafuta fedha na mali kwa wingi, ili
kuwaachia watoto wao urithi na wasiwe na maisha magumu. Lakini wote
tumekuwa tunaona nini kinatokea baada ya wazazi hao kufariki, utajiri na
mali zote zinapotea, kwa kutumiwa vibaya na watoto walioachwa.
Watoto
wako hawahitaji sana fedha wala mali zako, bali kikubwa wanachohitaji
ni msingi muhimu wa kufuata na kusimamia inapokuja kwenye swala la
fedha. Kuliko uwape watoto fedha bila ya misingi, ni bora uwape misingi
bila ya fedha. Kwa sababu misingi itawawezesha kupata fedha zaidi wakati
fedha pekee bila misingi zitapotea.
( 10 ). KUTOA NI UWEKEZAJI.
Mmoja
wa watu matajiri sana kuwahi kuwepo hapa duniani, John D. Rockefelar
amewahi kunukuliwa akisema unatumia nusu ya kwanza ya maisha yako
kukusanya fedha, halafu nusu ya pili unaitumia kuzigawa fedha hizo
kwenda kwa wengine.
Moja
ya vitu vinavyowafanya matajiri kuendelea kuwa matajiri ni utoaji.
Matajiri wengi wamekuwa watoaji wa misaada mbalimbali ya kijamii na hilo
limekuwa linawasukuma kufanikiwa zaidi kifedha. Hivyo kutoa ni
uwekezaji ambao unamlipa sana mtu baadaye.