Thursday, June 20, 2019

ISHI MAISHA YAKO, USIWE MTU WA CHUKI, SAMBAZA UPENDO

Kuna  watu wenye chuki, ambao kwa sababu tusizozijua, wanaamua kutuchukia, kwa jinsi tulivyo au kwa kile tunachofanya.
 
Wengi wamekuwa wanashangaa inakuwaje watu wawachukie, na hili ni kupoteza muda. Watu wenye chuki huwa wanachukia, na huna lolote unaloweza kufanya kuwafanya wasikuchukie.
 
Watu wenye chuki hawabadiliki na kuacha kuwa na chuki kwa sababu wewe umefanya kitu fulani, bali wataendelea kupata sababu za kuwa na chuki zaidi.
 
Hivyo badala ya kuishi maisha ya kutaka kuwaridhisha wengine, hasa wale wenye chuki, ishi maisha yako, fanya kile ambacho ni muhimu kwako na simamia kile unachoamini.
 
Wenye chuki watachukia iwe unaishi maisha yako au unafanya wanachotaka wao.
 
Usiyumbishwe na wenye chuki, chagua kuyaishi maisha yako.
 
Na kwa upande wa pili, usiwe mtu wa chuki, sambaza upendo.

FURSA YA MUZIKI---STADI ZA KAZI--DARASA LA SITA ( STD 6 )---SHULE ZA MSINGI---TANZANIA-------- " Fursa Afrika Mashariki Blog "

Friday, June 14, 2019

KILA HATUA UNAYOPIGA HUZALISHA KIKWAZO

Kwenye fizikia, kuna kanuni tatu kuu za mwendo ambazo mwanasayansi Isaac Newton alizigundua.
 
Kanuni ya kwanza inasema kitu kilichopo kwenye mwendo kinaendelea kuwa kwenye mwendo mpaka nguvu ya nje itakapotumika kukizuia.
 
Kanuni ya pili inasema nguvu ya kitu kilichopo kwenye mwendo inategemea uzito wake na mwendokasi wake.
 
Na kanuni ya tatu inasema kila mwendo huwa unazalisha upinzani.
 
Ni kanuni ya tatu ambayo tunakwenda kuijadili hapa kwenye dakika moja ili uelewe kwa nini baadhi ya vitu vinatokea kwenye maisha yako na hatua sahihi kwako kuchukua.
 
Kila mwendo unaoanzisha, kuna mwendo mwingine utakaoanzishwa kuzuia mwendo huo.
 
Unapojaribu kwenda mbele, kuna mtu atajitokeza kukurudisha nyuma.
 
Hii ndiyo inasababisha mafanikio kuwa magumu. Kwa sababu siku unayoamua kwamba unataka kufanikiwa, zitaibuka kila aina ya nguvu kukupinga, kutaibuka kila kikwazo kwenye njia yako ya mafanikio.
 
Unapojua hili, unajipanga kwa upinzani kwa kila hatua unayopanga kupiga na hujidanganyi kwamba mambo yataenda vizuri yenyewe kama wengi wanavyofanya.
 
Usishangae pale ambapo marafiki ulionao sasa watageuka kuwa maadui zako pale unapotangaza kwamba unataka kufanikiwa sana. ulipokuwa kawaida mlikuwa marafiki, unapopanga kupiga hatua zaidi wanakuwa maadui, hiyo ni kanuni ya asili, huwezi kupingana nayo.
 
Usikubali kipingamizi chochote kikuzuie wewe kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako, jua kwa kila hatua utakayopanga kuchukua kuna kipingamizi kitaibuka na hivyo jiandae kukivuka.

KILA MTU ATAKUFA , NI BORA UULIWE NA KAZI !


Kila mtu atakufa, hilo halina ubishi. Hii ni hukumu uliyoipata siku unayozaliwa, ambacho hujui ni siku gani hukumu hiyo itakamilika.
 
Lakini kuna kitu kingine muhimu sana kuhusu kifo ambacho wengi tumekuwa hatukitafakari, ambacho tukikielewa kitatusaidia sana.
 
Kila mtu kuna kitu kitakachomuua. Ndiyo, kuna kitu ambacho kitakuua, yaani kitachangia kwenye kifo chako.
 
Kuna ambao ulevi utawaua, kwa kuendekeza sana ulevi mwili unachoka na kupata magonjwa ambayo yanachangia kifo chao.
 
Kuna ambao chakula kitawaua, kwa kushindwa kula kwa nidhamu wanakuwa na afya mbovu ambayo inaleta magonjwa yanayowaua.
 
Kuna ambao wasiwasi na hofu vitawaua, kwa kuwa na wasiwasi na hofu mara zote kunaufanya mwili uwe haifu na hivyo kushindwa kuhimili magonjwa mbalimbali.
 
Kuna ambao mapenzi yatawaua, kwa kushindwa kudhibiti hisia zao za mapenzi na ngono wanajikuta kwenye hatari zinazoondoa maisha yao.
 
Kuna ambao kazi zitawaua, kwa kuweka muda na nguvu zao nyingi kwenye kazi zao kunachosha miili yao na kuibua magonjwa yatakayowaua.
 
Kuna ambao uvivu utawaua, kwa kukaa muda mrefu na kutokuwa na majukumu makubwa, mwili unakuwa mzembe na kushindwa kupambana na magonjwa na hilo kupelekea kifo.
 
Ndugu  yangu, hakuna atakayetoka hapa duniani akiwa hai, na kila mtu kuna kitu ambacho kitamuua.
 
Wito wangu kwako, chagua sumu yako vizuri, kile ambacho kitakuua, basi kiwe na maana kwako na hata wengine pia. Kuliko uuliwe kwa pombe, ulevi au ngono, ni bora uuliwe na kazi, maana kazi hiyo itakuwa na maana kwako na kwa wengine pia.