Sunday, May 5, 2019

CHANGAMOTO TANO ZINAZOKABILI KILA AINA YA BIASHARA.

Zipo changamoto kubwa tano ambazo zinakabili kila aina ya biashara, changamoto hizi tano ndiyo zinapelekea biashara nyingi kufa na hata zinazopona kushindwa kukua zaidi.
 
(1). KUKOSA  UDHIBITI .  Huna udhibiti wa kutosha kwenye muda wako, soko na hata biashara yako. Badala ya kuiendesha biashara, biashara inakuendesha wewe.
 
(2). WATU. Unavurugwa na wafanyakazi, wateja, wabia na hata wanaokusambazia huduma mbalimbali. Watu hao hawaonekani kukuelewa na wala hawazingatii yale unayowataka wazingatie.
 
(3). FAIDA. Faida unayopata haitoshi kuendesha biashara.
 
(4). UKOMO. Ukuaji wa biashara yako umefika ukomo, kila ukikazana kuweka juhudi zaidi hakuna ukuaji unaopatikana, unajikuta unachoka zaidi lakini hakuna cha tofauti unachopata.
 
( 5 ). HAKUNA  KINACHOFANYA  KAZI. Umeshajaribu mbinu mbalimbali za kuiwezesha biashara yako kukua na watu kukuelewa, lakini hakuna hata moja ambayo imeleta matokeo mazuri. Unaelekea kukata tamaa na kuona labda biashara siyo bahati yako.
 
Changamoto hizi tano zinaikabili kila aina ya biashara, lakini habari njema ni kwamba, changamoto hizi siyo mwisho wa biashara, unaweza kuzivuka na kuiwezesha biashara yako kukua zaidi kama utazingatia nguzo sita muhimu za ukuaji wa biashara yako.

FANYA KAZI NJE YA BIASHARA YAKO.

Kama unataka kufurahia biashara yako, basi unapaswa kufanya kazi nje ya biashara na siyo ndani ya biashara. Kufanya kazi ndani ya biashara ni pale ambapo unakuwa bize na shughuli za kila siku za biashara hiyo, kuuza, kuwahudumia wateja na kuzalisha au kuandaa bidhaa na huduma unazouza. Japokuwa unaweza kuona hilo ni muhimu na hata kupenda sana kulifanya, linakuzuia kuikuza zaidi biashara yako, maana unapofanya kazi ndani ya biashara, unachoka sana na hupati nafasi ya kuona mbali zaidi ya kile unachofanyia kazi kwenye biashara hiyo.
 
Kufanya kazi nje ya biashara yako ni pale ambapo unaiangalia biashara yako kama mtu baki, kuangalia kila kitu kinavyofanyika na kuona uimara na udhaifu wako. Ni sawa na kupanda juu angani kisha kuangalia biashara yako kwa chini, na kutathmini kila kinapofanyika. Unapofanya kazi nje ya biashara, hufikirii yale majukumu ya kila siku ya biashara, bali unaangalia kule ambako biashara inakwenda na uwezo wa kufika huko.
 
Kama unataka biashara yako ikue, lazima uweze kufanya kazi nje ya biashara yako, uweze kuiangalia biashara kama mtu wa pembeni na kupata picha ya pale ilipo sasa na inapoweza kufika.
 

WEWE NA BIASHARA YAKO NI VITU VIWILI TOFAUTI

Hiki ni kitu ambacho kila mfanyabiashara anapaswa kuambiwa, tena kupigiwa kelele kila mara mpaka aelewe. Kwa sababu kama wafanyabiashara wakielewa hili, nusu ya matatizo ya biashara yatatoweka yenyewe.
 
Sehemu kubwa ya matatizo ya biashara yanasababishwa na mfanyabiashara kufikiri yeye ni biashara yake, kitu ambacho siyo kabisa.
 
Biashara nyingi hazikui kwa sababu hakuna mpaka baina ya biashara na mmiliki wa biashara. Mtu anaweza kutoa fedha kiholela kwenye biashara kwa sababu anaona biashara ni yake. Kitu ambacho kinakuwa na athari kubwa sana kwenye ukuaji wa biashara hiyo.
 
Ndugu , naomba nikusisitizie hili, na liandike mahali ambapo utaweza kulisoma kila siku; WEWE SIYO BIASHARA YAKO, wewe na biashara yako ni vitu viwili tofauti kabisa.
 
Wewe una maisha yako, ndoto zako na mahusiano yako, biashara ina maisha yake, ndoto zake na mahusiano yake. Kinachowaunganisha wewe na biashara yako ni mtaji ambao umeuweka kwenye biashara hiyo, mtaji huo umeikopesha biashara, na njia pekee ya kunufaika kupitia biashara hiyo ni pale inaopata faida baada ya kufanyika kwa biashara.
 
Ukiweza kuelewa hili, kwamba wewe siyo biashara yako, ukaiheshimu biashara yako na kuiacha ikue bila ya kuiingilia, ukaiendesha kwa misingi ya ukuaji wa biashara, utaiwezesha biashara hiyo kukua zaidi.

FURSA 20 ZA KUFANYA KIPINDI CHA MVUA----Maisha Na Mafanikio Blog ( Life & You )

Saturday, May 4, 2019

FURSA ZA KUFANYA UKIWA NYUMBANI KWAKO ( A ) / BIASHARA ZA KUFANYA NYUMBANI-------Maisha Na Mafanikio Blog ( Life & You )

KILA BIASHARA INA CHANGAMOTO ZAKE . USIPUUZE AU KUKWEPA IKABILI KILA CHANGAMOTO INAPOJITOKEZA.

Ni changamoto zipi unazokutana nazo na unazoweza kukutana nazo mbeleni?
Kila biashara ina changamoto zake, hakuna biashara isiyokuwa na changamoto kabisa. Lakini watu wengi huwa hawapendi kukutana na changamoto, na hivyo huwa hawapo tayari kuzikabili.
Wanachofanya wafanyabiashara wengi pale wanapokutana na changamoto ni kuzipuuza au kuziacha wakiamini zitaondoka zenyewe. Changamoto hizo huwa haziondoki, badala yake zinakua na kuota mizizi, na hizo ndiyo huja kuua biashara.
Unapaswa kujua zipi changamoto kubwa zinazoikabili biashara yako sasa na hata siku za mbeleni. Kisha kuwa na mkakati sahihi wa kukabiliana na kila changamoto pale inapojitokeza. Usijaribu kupuuza au kukwepa changamoto, badala yake ikabili kila changamoto inapojitokeza, na siyo tu utaitatua, bali pia utapiga hatua zaidi kwenye biashara yako.