Sunday, January 6, 2019

PELEKA MAWAZO NA AKILI ZAKO ZOTE KWENYE UTAJIRI.

Huwezi kutengeneza na kutunza maono ya utajiri kama unahamisha mawazo yako kwenda kwenye picha inayokinzana mara kwa mara. Hupaswi kufikiria kitu kinachopingana na utajiri unaotaka kwenye maisha yako. Muda wako wote fikiria ile picha ya utajiri uliyojitengenezea.
 
Usizungumzie kuhusu umasikini uliokuwa nao au wazazi wako waliokuwa nao, usizungumzie kuhusu hali mbaya ya uchumi au mabaya yoyote yanayoendelea. Hata kama mambo ni magumu kiasi gani, hayo yanapita, hayadumu milele. Hivyo usiharibu fikra zako kwa kuyafikiria au kuyazungumzia.
 
Peleka mawazo na akili zako zote kwenye utajiri na ipe picha unayotaka kufikia na waache wengine wahangaike na hayo mengine.

NAMNA FULANI YA KUFIKIRI NA KUTENDA / KUCHUKUA HATUA ILI KUVUTIA UTAJIRI..

Fikra zina nguvu kubwa sana ya kuumba, pale unapofikiri kwa namna fulani, unatumia nguvu ya mfumo wa fikra unaoongoza dunia katika kukuletea kile unachotaka. Lakini kile unachotaka hakitatokea kwa muujiza, badala yake kitatokana na matendo na hatua unazochukua.
Ipo namna fulani ya kutenda ambayo inakuwezesha kupata kila unachotaka kwenye maisha yako. Na bila ya kuchukua hatua kwa namna fulani, hata kama ungekuwa na fikra bora kiasi gani, hazitaweza kuleta unachotaka.
Chochote unachokitaka sasa, kipo kwenye mikono ya wengine, na ili hao wengine wakupe hicho unachotaka, lazima wewe uwape kwanza kile wanachotaka. Hivyo lazima uwe na namna bora ya kuchukua hatua, namna inayoendana na fikra ulizonazo na kuchukua hatua ukiwa na imani na uhakika wa kupata unachotaka na utakipata.
Unapaswa kuchukua hatua sasa, kwa kuweka nguvu zako zote kwenye kile unachofanya kwa wakati huo, usifikirie kuhusu jana wala kesho, badala yake fikiria kuhusu kile unachofanya kwa wakati husika, hili litakuwezesha kufanya vizuri kile unachofanya.

CHUKUA HATUA ZENYE UFANISI ILI KUVUTIA UTAJIRI.

Kama pale ulipo sasa hapakuridhishi, kama unataka kupiga hatua zaidi kwenye maisha yako na kwa kile unachofanya, unapaswa kukua zaidi ya pale ulipo sasa. Unapaswa kuijaza ile sehemu uliyopo sasa kiasi kwamba hakuna tena nafasi kwa ajili yako na hivyo inakubidi ukue zaidi.
 
Chochote unachofanya sasa kifanye kwa viwango vya juu sana kuliko ilivyozoeleka. Na unapofanya kwa viwango vya juu, mfumo wa fikra unaoendesha dunia utakupeleka kwenye hatua za juu kuliko hapo ulipo sasa.
 
Kila siku fanya kile unachopaswa kufanya bila ya kuahirisha, na kifanye kwa ufanisi mzuri. Usifanye kitu chochote kwa haraka au njia ya mkato. Mafanikio kwenye maisha ni kufanya vitu kwa ufanisi wa hali ya juu.
 
Kwa kila hatua unayochukua, kuwa na picha ya matokeo unayotaka kupata na fikiria picha hiyo mara zote. Hili litaweka fikra zako kwenye kile unachofanya na utaweza kupata matokeo bora.

INGIA KWENYE BIASHARA SAHIHI KWAKO ILI KUVUTIA UTAJIRI.

Biashara au kazi yoyote inayo uwezo wa kutengeneza utajiri mkubwa kwa mtu yeyote. Lakini siyo kila aina ya biashara au kazi itaweza kutengeneza utajiri kwako.
 
Utapata utajiri na kufanikiwa kwa kuingia kwenye kazi au biashara ambayo inaendana na wewe. Biashara ambayo inatumia vipaji na uwezo mkubwa uliopo ndani yako.
 
Utafanikiwa zaidi kwa kufanya kile unachopenda na unachojali, kwa sababu utafanya kwa kupenda na siyo kufanya kama kazi.
 
Jua kipi unapenda na kujali na jua vipaji na uwezo mkubwa uliopo ndani yako kisha chagua kazi au biashara inayoendana na vitu hivyo. Hii ndiyo itakayokuletea utajiri mkubwa.

MWONEKANO WA UKUAJI KATIKA KUVUTIA UTAJIRI.

 
Kwa kazi au biashara unayoifanya, usifanye kwa mazoea au kufanya vile vile kila wakati. Badala yake fanya kwa ukuaji kila siku. Kila siku kazana kupiga hatua kubwa zaidi ya ulizopiga siku zilizopita.
 
Ni mwonekano huu wa ukuaji ndiyo unaowavutia watu kwako. Watu wanapenda kujihusisha na wale ambao wanakua zaidi, wanatoa thamani kubwa zaidi kila siku.
 
Mazoea yanaharibu na kuua kabisa kile ambacho kipo ndani ya mtu. Lakini ukuaji unakuza zaidi kile ambacho kipo ndani ya mtu.

UKUAJI BINAFSI KATIKA KUVUTIA UTAJIRI.

 
Ili kuvutia utajiri kupitia kile unachofanya na ili kuziona fursa mpya kila mara, lazima wewe binafsi uwe unakua. Kwa chochote unachofanya sasa, hata kama ni kidogo kiasi gani, unapaswa kukua zaidi ya kitu hicho.
 
Hata kama upo kwenye kazi au biashara ambayo ni ndogo, ifanye kama kubwa na tekeleza majukumu yako kwa ukubwa. Tekeleza majukumu yako kwa ufanisi wa hali ya juu na wahudumie watu kwa namna ambayo inaongeza thamani kubwa kwao.

SAYANSI / KANUNI YA KUPATA UTAJIRI


1. Kuna mfumo wa kufikiri ambao kutoka ndani yake vitu vyote vinatengenezwa na ambao kwa uhalisia wake unaruhusu, kupenyeza na kuujaza ulimwengu wote.
 
2. Fikra kwenye mfumo huu inazalisha ile taswira inayotengenezwa na fikra.
 
3. Mtu anaweza kutengeneza vitu kwenye fikra zake na kwa kuziweka kwenye mfumo huu wa kufikiri kile anachofikiri kinaumbwa.
 
4. Ili kufanya hivi, mtu anapaswa kuondoka kwenye fikra za ushindani na kwenda kwenye fikra za ubunifu. Vinginevyo hataweza kuendana na mfumo wa fikra ambao mara zote upo kwenye hali ya ubunifu na siyo ushindani.
 
5. Mtu yeyote anaweza kuendana na mfumo huu wa fikra kwa kuwa mtu wa shukrani kwa baraka ambazo amezipata. Shukrani inaunganisha fikra za mtu na mfumo wa fikra unaoendesha ulimwengu.
 
6. Mtu lazima atengeneze picha ya kifikra ya vitu anataka kuwa navyo na kuifikiria picha hii mara zote huku akiwa na imani kwamba ataipata na kushukuru kwamba mfumo wa fikra unamwandalia mazingira ya kupata kile anachotaka. Tumia muda wako wa mapumziko kufikiria picha ya utajiri unaotaka kuwa nao na mfumo wa fikra utaipanga dunia kwa namna ambayo itakuletea kile unachotaka.
 
7. Mfumo wa kufikiri unafanya kazi kupitia njia za asili za ukuaji na za kijamii. Kila ambacho kinafikiriwa kwa muda mrefu kwa imani na bila ya shaka, ndiyo kinacholetwa kwenye uhalisia.
 
8. Ili kupokea kile ambacho mtu anataka, lazima mtu achukue hatua kwa namna fulani ambayo inamwezesha kujaza pale alipo sasa. Lazima afanye zaidi, lazima atoe thamani kubwa kwa wengine kuliko thamani anayopokea na lazima akue zaidi na akuze zaidi kile anachofanya.