Friday, November 2, 2018

TENGENEZA UHURU KAMILI KWENYE MAISHA YAKO UTAPATA FURAHA YA KWELI

Wapo watu ambao wameajiriwa na wanalipwa mshahara mkubwa sana, kipato chao kinawawezesha kupata chochote wanachotaka, kwa upande wa kipato, lakini bado wanakosa furaha kwenye maisha yao. Na sababu kubwa ni kukosa uhuru wa maisha yao. Kwa sababu kadiri mtu anavyolipwa, ndivyo anavyotumika zaidi. Kadiri kipato cha ajira kinavyokuwa kikubwa, ndivyo majukumu yanakuwa mengi na kutegemewa kuwa tayari na kazi wakati wowote. Mtu hawezi kuchagua afanye nini na maisha yake, ni mpaka aombe ruhusa kwanza.

Uhuru ni kiungo muhimu sana cha furaha, huwezi kuwa na furaha kama huna uhuru.
Na uhuru siyo kwenye eneo la fedha na kazi pekee, bali hata kwenye fikra za wengine. Kama una chuki na wengine haupo huru, hivyo huwezi kuwa na furaha. Kama unashindana na wengine huwezi kuwa huru, kwa sababu muda wote utakuwa unawaangalia wanafanya nini.
Ili kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako, lazima uwe na uhuru na maisha yako. Kadiri unavyokuwa huru, ndivyo unavyokuwa na furaha.

UFUNGUO  WA  FURAHA:Tengeneza uhuru kamili kwenye maisha yako, ondoa utegemezi wako kwa wengine au vitu fulani ndiyo maisha yako yakamilike. Hata kama huna kila unachotaka, kitendo cha kuwa huru na muda wako na maisha yako, kinakuwezesha kuwa na furaha ya kudumu kwenye maisha yako.

JENGA MAHUSIANO CHANYA UTAPATA FURAHA YA KWELI KATIKA MAISHA YAKO

Mahusiano yetu na wengine yana mchango mkubwa sana wa namna maisha yetu yanavyokuwa. Kama utakuwa na mahusiano chanya, mahusiano ya kuelewana na wale watu unaojihusisha nao, mahusiano ya kujaliana, mahusiano ya kuwa tayari kutoa zaidi, kwa kuhusiana na wanaotoa zaidi, basi maisha yako yatakuwa ya furaha.

Kitendo cha kujua kuna watu wapo kwa ajili yako, na wewe upo kwa ajili ya wengine kinakufanya uridhike na maisha na kuwa na furaha.
Kwa upande mwingine mahusiano hasi, yasiyo na maelewano, yenye msuguano mara zote, ni chanzo cha kukosa furaha kwa wengi.

UFUNGUO WA FURAHA:Tengeneza mahusiano chanya kwenye maisha yako, chagua wale watu ambao ni wa muhimu kwako na unapenda kuwa na mahusiano bora na wao, kisha wape muda na wajali zaidi. Kuwa tayari kujitoa zaidi kwa ajili yao, na wao watakuwa tayari kujitoa kwa ajili yako.

KUWA STADI UTAPATA FURAHA YA KWELI KATIKA MAISHA YAKO.

Umahiri katika jambo fulani unalofanya kwenye maisha yako. Mtu unakuwa na furaha pale unapojua kwamba kuna kitu unaweza kukifanya vizuri na kikawa na msaada kwenye maisha ya wengine.

Mtu unakuwa na furaha pale unapofanya kitu chenye maana kwako na kuweza kukifanya kwa ustadi na umahiri wa hali ya juu. Hata kama kitu ni kigumu kiasi gani, unapoweza kukifanya vizuri, unajijengea kuridhika ndani yako na hiyo ndiyo inakufanya uwe na furaha ya kudumu.

Ukitaka kudhibitisha hili angalia watu ambao wanapata fedha nyingi bila ya kufanya kazi. Labda wameshinda bahati nasibu au wamepata urithi, maisha yao huwa mabovu sana licha ya kuwa na fedha nyingi. Ni kwa sababu wanakuwa hawajafanya kitu kikubwa kupata fedha hizo, na wengi huishia kuzipoteza.

UFUNGUO  WA   FURAHA: Chagua kitu au eneo utakalokuwa na ustadi nalo kwenye maisha yako, eneo ambalo utafanya vizuri na utaongeza thamani kwenye maisha ya wengine. Kama ni mwalimu fundisha vizuri sana, kama daktari tibu vizuri, kama mwandishi andika vizuri vitu vinavyowasaidia watu. Kadhalika kwenye kilimo, ufundi, uwakili na ujuzi mwingine wowote.

Monday, October 22, 2018

KABLA HUJAINGIA BIASHARA YOYOTE JIULIZE MASWALI HAYA

Yapo maswali mawili muhimu sana kwa kila mtu kujiuliza kabla ya kuingia kwenye biashara yoyote ile. Kwa kujiuliza maswali haya, utaingia kwenye biashara ukiwa na uelewa sahihi, na ukijua ni hatua zipi sahihi kwako kuchukua ili kufanikiwa zaidi kwenye biashara unayofanya.

 (1). NI   NANI  MWENYE  FEDHA  ZANGU?

Nilishakuambia siku za nyuma kwamba hutafuti fedha bali unakusanya fedha. Fedha unayoitaka sasa, ipo kwenye mikono ya mtu mwingine. Hivyo hatua ya kwanza kabisa kwenye kufikiria biashara yako ni kujiuliza nani mwenye fedha zako.
Hapa unahitaji kuwajua wateja halisi wa biashara yako, watu ambao wana shida, wana changamoto, wana uhitaji ambao unaweza kuutimiza. Pia watu hao wana fedha ya kuweza kukulipa wewe kwa kile ambacho unawapa.
Kama hujawajua watu wenye fedha zako, ukianzisha biashara utakuwa unapoteza muda wako. Kwa sababu hata kama unaona wengine wanauza sana, utashangaa unakaa kwenye biashara na hupati mauzo makubwa kama wengine.
Kwa sababu unakua hujajua nani mwenye fedha zako na kumfuatilia huyo zaidi.
Kama uliingia kwenye biashara bila kujiuliza swali hili, kaa chini sasa hivi na jiulize nani mwenye fedha zako? Orodhesha sifa za watu ambao wanaweza kunufaika na aina ya biashara unayofanya, na wenye uwezo wa kulipia kile unachouza.
Ukishajua kwa hakika nani mwenye fedha zako, ni rahisi kumlenga huyo na ukaweza kumhudumia vizuri na wote mkanufaika sana.

(2).JUA  NI  KITU  GANI  UNABADILISHANA  NAO  ILI  WAKUPE  FEDHA.
Baada ya kuwajua wenye fedha zako, unahitaji kujua kitu gani unahitaji kuwapa ili nao wakupe fedha walizonazo. Kwa sababu kila mtu amepata fedha yake ka uchungu, na hivyo hataki kuipoteza. Lazima uwe na sababu kubwa ya kumshawishi mtu akupe fedha zako. Kumbuka akishakupa fedha wewe, hawezi tena kuitumia kwa mambo yake mengine.
Hapa unahitaji kujua kwa hakika ni thamani gani unatoa kwa wateja wa biashara yako. Hapa unahitaji kujua kwa hakika ni mahitaji gani waliyonayo wateja wako ambayo unayatimiza, ni maumivu gani ambayo unayatuliza.
Kama huna sababu ya kutosha, ya kumshawishi mteja akupe fedha yake aliyoipata kwa shida, hutaweza kufanikiwa kwenye biashara yako.
Kwa sababu kumbuka mteja hanunui kwa sababu wewe unauza, wala hanunui kwa sababu anakuonea huruma. Bali mteja ananunua kwa sababu ana uhitaji, ana maumivu ndani yake ambayo hawezi kuendelea nayo na kuna mtu amemshawishi kwamba ana kitu cha kutimiza mahitaji yake au kutuliza maumivu yake.
Hivyo baada ya wewe kujua ni nani mwenye fedha zako, jua maumivu yake ni yapi, kisha mweleze jinsi kile unachouza kinavyoweza kutuliza maumivu aliyonayo.

Sunday, October 21, 2018

KUFANIKWA HUHITAJI KUFANYA KILA KITU AU KUJUA KILA KITU.

Ili kufanikiwa huhitaji kufanya kila kitu au kujua kila kitu. Badala yake chagua eneo lako ambalo unaweza kufanya vizuri, kisha kazana kufanya vizuri, kuwa bora kuliko wengine wote na utaweza kufanikiwa zaidi. Kadiri unavyochagua vizuri eneo lako na kuweka juhudi kubwa, ndivyo unavyotumia nguvu zako na umakini wako vizuri.

NI ASILIMIA KUMI TU NDIO MUHIMU.

Jifunze kutofautisha kati ya mawazo na mawazo mazuri, bidhaa na bidhaa bora, uwekezaji na uwekezaji mzuri. Asilimia 90 ya vitu vyote unavyokutana navyo, siyo muhimu, yaani ukiachana navyo hutakosa chochote. Ni asilimia 10 tu ndiyo muhimu, jua hiyo asilimia kumi na ukazane nayo huku ukipuuza mengine yote.

ISHI MAISHA YAKO., USIJIONYESHE WEWE NI BORA KULIKO WENGINE.

Kuwa na kiasi, haijalishi umefanikiwa kiasi gani, miaka 200 ijayo, huenda hakuna atakayejua hata kama uliishi hapa duniani. Kila unapoanza kujiona wewe ni muhimu kuliko wengine, kumbuka kitakachotokea miaka 200 ijayo, dunia itakuwa imekusahau kabisa. Ishi maisha yenye maana kwako na siyo maisha ya kujionesha na kutaka wengine waone wewe ni muhimu kuliko wao.