Yapo maswali mawili muhimu sana kwa kila mtu kujiuliza kabla ya kuingia
kwenye biashara yoyote ile. Kwa kujiuliza maswali haya, utaingia kwenye
biashara ukiwa na uelewa sahihi, na ukijua ni hatua zipi sahihi kwako
kuchukua ili kufanikiwa zaidi kwenye biashara unayofanya.
(1). NI NANI MWENYE FEDHA ZANGU?
Nilishakuambia siku za nyuma kwamba hutafuti fedha bali unakusanya
fedha. Fedha unayoitaka sasa, ipo kwenye mikono ya mtu mwingine. Hivyo
hatua ya kwanza kabisa kwenye kufikiria biashara yako ni kujiuliza nani
mwenye fedha zako.
Hapa unahitaji kuwajua wateja halisi wa biashara yako, watu ambao
wana shida, wana changamoto, wana uhitaji ambao unaweza kuutimiza. Pia
watu hao wana fedha ya kuweza kukulipa wewe kwa kile ambacho unawapa.
Kama hujawajua watu wenye fedha zako, ukianzisha biashara utakuwa
unapoteza muda wako. Kwa sababu hata kama unaona wengine wanauza sana,
utashangaa unakaa kwenye biashara na hupati mauzo makubwa kama wengine.
Kwa sababu unakua hujajua nani mwenye fedha zako na kumfuatilia huyo zaidi.
Kama uliingia kwenye biashara bila kujiuliza swali hili, kaa chini
sasa hivi na jiulize nani mwenye fedha zako? Orodhesha sifa za watu
ambao wanaweza kunufaika na aina ya biashara unayofanya, na wenye uwezo
wa kulipia kile unachouza.
Ukishajua kwa hakika nani mwenye fedha zako, ni rahisi kumlenga huyo na ukaweza kumhudumia vizuri na wote mkanufaika sana.
(2).JUA NI KITU GANI UNABADILISHANA NAO ILI WAKUPE FEDHA.
Baada ya kuwajua wenye fedha zako, unahitaji kujua kitu gani
unahitaji kuwapa ili nao wakupe fedha walizonazo. Kwa sababu kila mtu
amepata fedha yake ka uchungu, na hivyo hataki kuipoteza. Lazima uwe na
sababu kubwa ya kumshawishi mtu akupe fedha zako. Kumbuka akishakupa
fedha wewe, hawezi tena kuitumia kwa mambo yake mengine.
Hapa unahitaji kujua kwa hakika ni thamani gani unatoa kwa wateja wa
biashara yako. Hapa unahitaji kujua kwa hakika ni mahitaji gani
waliyonayo wateja wako ambayo unayatimiza, ni maumivu gani ambayo
unayatuliza.
Kama huna sababu ya kutosha, ya kumshawishi mteja akupe fedha yake
aliyoipata kwa shida, hutaweza kufanikiwa kwenye biashara yako.
Kwa sababu kumbuka mteja hanunui kwa sababu wewe unauza, wala hanunui
kwa sababu anakuonea huruma. Bali mteja ananunua kwa sababu ana
uhitaji, ana maumivu ndani yake ambayo hawezi kuendelea nayo na kuna mtu
amemshawishi kwamba ana kitu cha kutimiza mahitaji yake au kutuliza
maumivu yake.
Hivyo baada ya wewe kujua ni nani mwenye fedha zako, jua maumivu yake
ni yapi, kisha mweleze jinsi kile unachouza kinavyoweza kutuliza
maumivu aliyonayo.
BADILI FIKRA.FIKIRI TOFAUTI .BADILI MAISHA.JITAMBUE .JIFUNZE ELIMU YA SAIKOLOJIA,TEOLOJIA , FEDHA ,UTAMBUZI(SELF HELP EDUCATION),FALSAFA YA MAISHA,MAISHA NA MAFANIKIO,BIASHARA / UJASIRIAMALI.FURAHIA WASAA WAKO NA MAISHA NA MAFANIKIO BLOGU.THIS IS THE COMMUNITY CAPACITY BUILDING BLOG.ENJOY THE BLOG.STRETCH YOUR MIND. YOU CAN CHANGE YOUR LIFE FOR EVER. YOU CAN ACHIEVE EXCELLENCE.YOU CAN MAKE A DIFFERENCE.
Monday, October 22, 2018
Sunday, October 21, 2018
KUFANIKWA HUHITAJI KUFANYA KILA KITU AU KUJUA KILA KITU.
Ili kufanikiwa huhitaji kufanya kila kitu au kujua kila kitu. Badala
yake chagua eneo lako ambalo unaweza kufanya vizuri, kisha kazana
kufanya vizuri, kuwa bora kuliko wengine wote na utaweza kufanikiwa
zaidi. Kadiri unavyochagua vizuri eneo lako na kuweka juhudi kubwa,
ndivyo unavyotumia nguvu zako na umakini wako vizuri.
NI ASILIMIA KUMI TU NDIO MUHIMU.
Jifunze kutofautisha kati ya mawazo na mawazo mazuri, bidhaa na bidhaa
bora, uwekezaji na uwekezaji mzuri. Asilimia 90 ya vitu vyote
unavyokutana navyo, siyo muhimu, yaani ukiachana navyo hutakosa
chochote. Ni asilimia 10 tu ndiyo muhimu, jua hiyo asilimia kumi na
ukazane nayo huku ukipuuza mengine yote.
ISHI MAISHA YAKO., USIJIONYESHE WEWE NI BORA KULIKO WENGINE.
Kuwa na kiasi, haijalishi umefanikiwa kiasi gani, miaka 200 ijayo,
huenda hakuna atakayejua hata kama uliishi hapa duniani. Kila unapoanza
kujiona wewe ni muhimu kuliko wengine, kumbuka kitakachotokea miaka 200
ijayo, dunia itakuwa imekusahau kabisa. Ishi maisha yenye maana kwako na
siyo maisha ya kujionesha na kutaka wengine waone wewe ni muhimu kuliko
wao.
MAFANIKIO YA KWELI NI MAFANIKIO YA NDANI .KAZANA KUWA BORA KILA SIKU.
Kuna orodha nyingi za watu waliofanikiwa, kuanzia ndani ya nchi mpaka
dunia nzima. Lakini jinsi mafanikio hayo yanavyopimwa inaweza isiwe
sahihi kwako. Mafanikio ya kweli kwako ni mafanikio ya ndani yako,
ambayo siyo rahisi kupimwa kwa nje. Mafanikio ya ndani utayapata kwa
kuweka juhudi kwenye yale maeneo uliyochagua, kuweka umakini wako kwenye
mambo yaliyo ndani ya uwezo wako na kuachana na mengine yote. fedha,
madaraka na umaarufu ni vitu vya nje, ambavyo huwezi kuvidhibiti,
unachoweza kudhibiti ni hatua unazochukua. Kazana kuwa bora kila siku na
weka juhudi zaidi kwenye kile ulichochagua kufanya.
Tuesday, October 16, 2018
WAZAZI HUKWAMISHA AU KUENDELEZA VIPAJI VYA WATOTO WAO.
Lulu A. Sanga BBC Swahili
Kipaji ni uwezo wa kuzaliwa nao wa kufanya jambo fulani kwa ngazi ya juu bila kufundishwa au baada ya kufundishwa kidogo tu. Kipaji kinaweza kuwa cha kimwili au cha kiakili lakini pia kinaweza kuendelezwa au kudumazwa.
Baadhi ya wazazi hutambua vipaji vya watoto mapema na kuanza kuviendeleza kwa kuwapatia nyenzo mbali mbali ambazo huwasaidia katika kuboresha uwezo walio nao.
Lakini pia wapo wazazi ambao wanamalengo yao juu ya ni kitu gani wanapenda watoto wao wafanye. Ama yamkini hawana ufahamu wa nini cha kufanya ili kumwendeleza mtoto mwenye kipaji .Hata hivyo vipo baadhi ya vipaji ambavyo wazazi huona ni upotevu tu wa maadili mfano kuimba na kucheza mziki.
BBC imezungumza na mama Ritha, mama mwenye watoto wanne. Anasema kwa kiasi kikubwa baadhi ya wazazi na hata yeye mwenyewe kipindi cha nyuma walikwamisha sana watoto sababu walikuwa hawatambui kama kipaji pia ni njia salama ya kumwezesha mtoto kimaisha.
"Wazazi wengi huwa hawajuagi tena zamani tulikuwa tunaona watoto wanapotea kabisa. Mi binti yangu wa kike alikua anapenda kuandika nyimbo za wasanii wa marekani na hata za kwake mwenyewe kwenye daftari lake afu kukiwa na sherehe yeye ndo mwimbaji. Nikaona anapotea nlikua na mchapa na nlimwambia akifika chuo kikuu ndo afanye uo mziki lakini si nyumbani kwangu maana hata baba yake alikuwa hapendi kabisa," Mama Ritha anaiambia BBC
Hata hivyo ameongeza kuwa wazazi pia huwanyima fursa za kujifunza watoto kwani kila akishika kitu mzazi hupiga kelele mtoto aache kwa madai kwamba ataumia.
Hata hivyo wapo baadhi ya watoto ambao wamepewa msaada mkubwa na wazazi wao katika kuboresha na kuendeleza vipaji vyao.
BBC imezungumza na mwanadada mpambaji Plaxeder Jumanne au baby precious kama anavyojulikana katika kazi zake za upambaji, anasema mama yake ndio mtu wa kwanza kumshauri ageuze kipaji chake kuwa biashara huku akimnunulia vifaa orijino vya urembo.
"Mie nlikuwa nawachukua watoto wenzangu nawapamba nlikua napenda sana urembo kama mama yangu. Hata nilipo kuwa nikaanza kuwapamba watu. Nilikuwa natumia vifaa feki hivi vya bei rahisi lakini mama yangu alianza kwa kuninunulia vifaa orijino kabisa. Na huwezi amini nilikua nampamba yeye na kumfuta kabla sijapata wateja tena nimejifunza kufunga maremba ya kinaijeria kichwani kwa mama na alikuwa ananisaidia sana, sasa hivi nasafiri hadi mikoani na kupamba watu mbali mbali hadi watu maarufu na nimepata pesa nikanunua vifaa vingi sana Orijino," Plaxeda anaiambia BBC.
Hata hivyo manadada huyo anasema kwa sasa mama yake ametangulia mbele za haki tangu mwaka jana ila bado anamshukuru kwa sababu hivi sasa kazi ya upambaji inampa pesa kuliko ajira yake na imemwezesha kufungua biashara zingine.
"Mimi sijajitangaza sana ila kupitia vifaa alivyonianzishia navyo mama yangu nikawa napamba hadi maharusi na wasimamizi wao. Na kipaji hiki kimenipa pesa ninafanya biashara ya kutengeneza nywele hasa mawigi na pia kufungua biashara ya nguo. Mama yangu angekuwepo angefurahi sana ila naamini anaona. Nimewaremba baadhi ya wasanii wa Tanzania. Safari ndo inaanza," Plaxeder anaiambia BBC.
Mwanaharakati wa masuala mbali mbali ya kibinadamu Shahista Alidina maarufu kama Shaykaa, anasema baadhi ya wazazi hupenda kutimiza ndoto zao kupitia watoto na mwishowe huwakwamisha.
"Unakuta mzazi kama alishindwa kuwa mwanasheria au daktari kama alivyotaka huko nyuma atataka mtoto wake afuate ndoto hiyo. Hawataki kuwapa uhuru watoto wafuate wanavyopenda. Unakuta kipaji cha mtoto kinaweza mletea kipato cha kutosha tu ila mzazi anampa mtoto shinikizo la kufaulu tu shule awe namba moja, mbili au tatu na ndiomaana unaona watoto wengine hadi wanajiua. Wanawanyima fursa watoto kufanya vitu wanavyovipenda," Shaykaa anaiambia BBC.
Hata hivyo anaongeza kuwa kunachangamoto nyingine kwa wazazi kupangia kazi watoto kuwa hii ni ya wanawake au hii ni ya wanaumena kujenga uoga kwa watoto na kuwanyima fursa ya kujituma zaidi.
"Kusoma kwa mtoto ni muhimu ila kuna muda wa ziada na kuna maisha nje ya darasa. Unakuta mtoto wa kike anapenda kucheza mpira, lakini mzazi atapinga kuwa huu ni mchezo wa wanaume mwanamke hatakiwi, sasa hapo moja kwa moja mzazi atakuwa ameua kabisa kipaji cha mtoto kama mtoto atakosa fursa ya kujiendeleza huko mbele," anasema Shaykaa
Mwanaharakati huyo pia amewaasa wazazi kuhakikisha wanawasaidia watoto kujiendeleza kijamii.
"Mtoto ni muhimu awe na maisha yake pia, na tutambue kuwa na wao ni binadamu wala si wafungwa. Ni muhimu ndio kufuata dini na misingi bora ya maisha pamoja na mila na desturi lakini tusisahau kuwa mtoto anapofikia umri wa kujielewa anahaki ya kufanya maamuzi kuwa anapenda nini ilimradi ni jambo jema kisheria, kidini, kiafya na kijamii. Tuwe marafiki kwao lakini tusiwapotoshe watoto wetu, Shaykaa anaiambia BBC.
JE, TUWAPE WATOTO WETU SIMU ZETU ZA MKONONI WACHEZEE ??
14 Oktoba 2018, BBC SWAHILI
Hivi karibuni
imekuwa kawaida sana kumkuta mtoto anatumia simu ya mkononi ya mzazi
wake na mara nyingine wanatumia bila hata kupata ridhaa ya mzazi
mwenyewe.
Baadhi ya watoto huonyesha utaalamu wa hali ya juu katika kufungua kurasa mbalimbali za simu hizo.Na inadaiwa kuwa kuna watoto ambao huwa wanajifunza mambo mengi kupitia simu za mkononi.
Hata hivyo si wazazi wote ambao hukubali simu zao zitumiwe na watoto, baadhi huwa wakali na kuweka kila aina ya nywila ingawa wengine huwa hawaoni shida kuwapatia watoto wao simu punde tu wanaporejea kutoka kwenye majukumu yao ya kila siku.
Baadhi ya wazazi huwa wanaona kuwa simu ndio njia pekee inayoweza kuwafanya watoto wao watulie na wao wapate muda wa kupumzika ama hata kufanya shughuli zao za nyumbani.
Je,kuna faida yeyote endapo mtoto atatumia simu?
BBC imezungumza na baadhi ya wazazi ili kufahamu ni kwa kiasi gani watoto wao hutumia simu zao na wanawadhibiti vipi vitu anavyoangalia mtoto?
"Kwa kweli simu yangu hata sina uhuru nayo huwa nikifika tu nyumbani wanangu huwa wananipokea kwa mbwembwe zote na cha kwanza kubeba ni simu na nikihitaji lazima niwaombe wao.
Simu ikiita utakuta wao ndio wanapokea,mara nyingi wanaangalia video za kartoon au za watoto wenzao zilizopo you tube," Mama Brian anaeleza
Alex Kayetta ambaye ni baba wa mtoto mmoja, anasema simu yake huwa haimiliki punde tu anapofika nyumbani ,
"Mwanangu akishashika simu yangu yani kuipata lazima nimbembeleze, na akichukua mara nyingine huwa lazima nimtafute alipo ,kuna siku nilimkuta amejificha ndani ya beseni akicheza michezo ya kwenye simu'game' nikampiga picha".
Freddie Kyara ni mwanasaikolojia kutoka nchini Tanzania ambaye anaeleza kuwa hali hii huwa inafanana na jinsi mzazi anapokua kwenye simu muda mrefu na hupoteza fursa ya kuwa karibu jamii na ndivyo hivyo inavyotokea kwa mtoto.
Na kwa upande wa mtoto kutumia simu huwa kuna madhara pia "Kukua kwa mtoto kunahitaji awe na mbinu za kijamii, kama vile kucheza na watoto wenzake na kujifunza mambo mbalimbali kutoka kwa wenzake, lakini siku hizi unaweza kukuta mtoto anashindwa kucheza na watoto wengine kwa sababu amezoea yeye rafiki yake ni simu tu.
Ubunifu wa mtoto unaweza kupungua. Sisi wakati tunakuwa hatukuwa tunajua habari za simu, ilikuwa ni kucheza mpira na kujishughulisha na shughuli mbalimbali za nyumbani na hali hiyo ilitufanya tuweze kujenga urafiki na watu na kujua tabia za watu tofautitofauti.
Mtoto anaweza kujifunza pia kwenye simu lakini lazima uthibiti uwepo kwa sababu sio kila kilichopo kwenye simu kina maudhui mazuri kwa watoto na wanapaswa kutengewa muda" Kyara ,mtaalamu wa saikolojia alieleza.
Hata hivyo jumbe mbalimbali zimekuwa zikisambaa kuonya madhara ya mionzi ya simu kwa watoto wadogo na kudai kuwa umri sahihi wa kupewa simu ni kuanzia miaka kumi na sita.
Jambo ambalo Daktari Fredrick Mashili anasema madhara ya namna hiyo huwa inategemeana zaidi na umri wa mtoto japo kwa upande mwingine macho yanaweza kupata shida ingawa hakuna ushahidi wa kutosha kuthibitisha madhara hayo ya mionzi.
"Kuna wasiwasi kwamba mtu akianza kutumia simu mapema anaongeza muda wa kuyashughulisha macho yake katika mionzi kwa muda mrefu zaidi kitu ambacho si kizuri kwa afya ya macho," Dkt.Mashili alieleza.
Subscribe to:
Posts (Atom)