Friday, October 12, 2018

EPUKA MADENI ILI KUEPUKA KUJIWEKA KWENYE WAKATI MGUMU KIFEDHA.

Kiasi cha fedha unachodaiwa na wengine kutokana na vitu ulivyonunua bila ya kuwa na fedha ni kipimo cha maamuzi yako ya kifedha kwa siku za nyuma. Kadiri madeni yako yanavyokuwa makubwa, ndivyo sehemu kubwa ya kipato chako inavyoelekea kwenye kulipa madeni hayo na wewe kubaki na kiasi kidogo ambacho hakiwezi kukutosheleza.

Unahitaji kutokuwa na deni binafsi kabisa, na madeni mazuri unayopaswa kuwa nayo ni yale yanayojilipa yenyewe. Madeni yanayojilipa yenyewe ni yale ambayo yanazalisha faida na faida hiyo unatumia kulipa deni. Haya ni madeni ambayo hayakuumizi.

Lakini madeni ambayo unalipa kwa fedha zako unazopata kwenye shughuli zako binafsi, ni utumwa ambao utakutesa kwa muda mrefu. Kama upo kwenye madeni ya aina hii kazana kuondoka na usiingie tena ili kuepuka kujiweka kwenye wakati mgumu kifedha.

WEKEZA SASA KWA AJILI YA BAADAYE , WAKATI UNA NGUVU ZA KUFANYA KAZI.

Kiwango ambacho umekiwekeza kwenye maeneo ambayo yanazalisha riba au faida ni kipimo muhimu kwa maandalizi yako ya kifedha ya baadaye. Kama hapo ulipo hujafanya uwekezaji wote kwa ajili ya baadaye, kama hujawa na maandalizi ya kukuwezesha kuingiza kipato bila ya wewe kufanya kazi moja kwa moja, huna maandalizi ya kifedha ya baadaye, na haupo eneo zuri kifedha.

Unahitaji kufanya uwekezaji kwa ajili ya baadaye, kwa sababu utakuja wakati ambapo huna uwezo wa kufanya kazi kama unavyofanya sasa, lakini una mahitaji muhimu kwa maisha yako. Unapokuwa umewekeza na uwekezaji unazalisha, maisha yako yanakwenda vizuri.

Kiwango sahihi cha uwekezaji unachopaswa kuwa nacho ni kile ambacho kinazalisha faida au riba ambayo inakuwezesha wewe kuendesha maisha yako kwa kadiri ya mahitaji yako.

Wednesday, October 10, 2018

TATIZO NI TAFSIRI YA MATUKIO YANAYOTUTOKEA.

Watu wawili wanaweza kushindwa kwenye kitu kimoja, mmoja akachukulia kushindwa huko kama kichocheo cha kufanya zaidi na akafanikiwa. Mwingine anaweza kuchukulia kushindwa huko kama sababu ya kukata tamaa na kushindwa kabisa.

Tukio ni moja, tafsiri tofauti na matokeo tofauti kabisa.
Siyo kinachotokea, bali namna unavyotafsiri kinachotokea ndiyo inaleta madhara kwako.
Kwenye Falsafa ya Ustoa pia kuna dhana inayoitwa upili wa udhibiti. Dhana hii inaeleza kwamba vitu vyote vinavyotokea kwenye maisha yako, vinagawanyika katika makundi mawili, kundi la kwanza ni vitu unavyoweza kuviathiri, hivi vipo ndani ya uwezo wako. Kundi la pili ni vitu usivyoweza kuviathiri, hivi vipo nje ya uwezo wako.

Hivyo unapokutana na chochote na ukajiambia ni kigumu au kinakushinda, huna haja ya kusumbuka, badala yake jiulize je kipo ndani ya uwezo wako au nje ya uwezo wako. Kama kipo ndani ya uwezo wako chukua hatua sahihi, kama kipo nje ya uwezo wako kikubali kama kilivyo au kipuuze. Hakuna namna bora ya kuendesha maisha yako kama hii, kwa sababu hakuna chochote kitakachotokea, ambacho kitakuvuruga kabisa.

Ndugu  yangu , nikukumbushe tena ya kwamba kama unataka kuitawala dunia, kuna mtu mmoja unayepaswa kumtawala, na mtu huyo ni wewe mwenyewe. Hutaweza kujitawala wewe mwenyewe kwa mabavu au nguvu, badala yake utajitawala kwa kudhibiti mawazo yako na hisia zako.

JINSI YA KUJENGA IMANI KWA WATEJA WAKO KWENYE KILE UNACHOUZA.KUWA MUUZAJI MZURI.


Moja; penda kile unachofanya, usifanye kwa sababu ya fedha pekee, fanya kwa sababu unapenda kufanya, fanya kwa sababu unajali, fanya kwa sababu kuna mchango unaotoa kwa wengine.

Mbili; kuwa mtumiaji wa kwanza wa kile unachouza, hakikisha wewe mwenyewe unaweza kutumia, au unaweza kumshauri mtu wako wa karibu kabisa, unayempenda sana atumie. Kwa maneno mengine usiuze kitu ambacho wewe mwenyewe huwezi kutumia au huwezi kumpa mtu wako wa karibu atumie.

Tatu; toa uhakika wa unachouza na mpe mteja nafasi ya kurudisha iwapo alichonunua hakitamfaa au hakitafanya kazi kama alivyotegemea. Mfanye mteja aone hana cha kupoteza anaponunua kwako.
Nne; jua tatizo la mteja unalotatua na elezea kile unachouza kwa namna kinavyotatua tatizo hilo. Usieleze sifa za kitu pekee, bali eleza namna zinatatua tatizo la mteja wako.

Tano; usiwaseme vibaya washindani wako, usihangaike kuwashinda wengine, kama unachouza ni kizuri kweli, huna haja ya kuhangaika na wengine wanauza au kusema nini. Lakini kama huamini kwenye unachouza, itabidi uanze kuwakosoa na kuwasema vibaya wengine, ili kumfanya mteja wako aone wewe upo sahihi, lakini hata unapowasema vibaya wengine, mteja anajua kuna shida kwenye biashara yako.

Monday, October 8, 2018

KWANINI UISHIE KUPATA PESA YA KULA TUU ??? UHA HAKI YA KUPATA PESA YA KUTOSHA.


“Pesa ya kula ni sumu ya maendeleo na utajiri” – Cypridion Mushongi 

Kila mmoja anajitahidi kutafuta pesa popote anakojua. Habari njema ni kwamba kila anayetafuta pesa hii ya KULA anapata. Lakini.. pamoja na kuipata, wengi wamekuwa wakilalamika kuwa ni ndogo na kwamba inatosha kula tu! Wengi wanatamani kupata pesa nyingi zaidi ya hiyo wanayoipata kwasasa. Kwaujumla, wengi wanashangaa ni kwanini hawapati pesa ya kutosha kuweza kufanya mambo makubwa zaidi ya KULA na kulipa ADA za watoto. 

Sababu mojawapo ya kushindwa kupata pesa ya kutosha ni malengo mahususi tunayojiwekea kabla ya kutafuta pesa. Watu wengi wakiamka asubuhi, malengo yao makubwa kabisa ni kutafuta pesa ya KULA, ADA na kujenga NYUMBA ya makazi. Wengine akijikakamua kidogo analenga kununua GARI la kutembelea. Malengo ya watu yanabainishwa kwenye maongezi yao ya kawaida. Pindi ukiwasikiliza watu, utasikia wakiambizana kuwa “mimi natafuta pesa ya kula basi! Wengine utawasikia wakisema “natafuta pesa kwaajili ya watoto” wengine wamekwenda mbali na kusema kuwa wanatafuta pesa, “ili watoto wao angalau waweze kwenda choo” Ni wazi kuwa maongezi ya namna hii, yanakupa jibu la moja kwa moja kuwa watu wengi wana malengo ya kutafuta kiasi kinachotosha KULA, kulipa KARO na kujenga NYUMBA ya makazi basi! kwamba zaidi ya hapo ni bahati tu. 

Wengi wa wale wanaolalamika kupata pesa kidogo ni wale walioweka malengo ya kutafuta pesa ya KULA. Ukiweka malengo ya KULA, ujue malengo hayo ni madogo sana na kwa vyovyote vile yatavutia pesa kidogo sana kwako. Mtu yeyote mwenye malengo ya kupata pesa ya KULA, hawezi kuweka utajiri kama kipaumbele chake. Na mwisho wake ujikuta hana ndoto yoyote ya kutajirika maisha yake yote. 

Ukweli ni kwamba, pesa ya KULA siku zote huwa ni ndogo japokuwa inapatikana kila ikitafutwa. Pamoja na kupatikana kila siku, tatizo lake ni moja; kwamba, ikishapatikana muhusika anakuwa tayari ana njaa na hivyo kuitumia mara moja. Ikishaisha muhusika uenda kutafuta tena, na huo ndio unakuwa mzunguko na mtindo mzima wa maisha ya kila siku. 

Kujiwekea malengo ya kutafuta pesa ya KULA na ADA siyo jambo baya! Ubaya unakuja pale utakapofanya suala la kutafuta pesa ya KULA kama lengo lako kuu. Mara nyingi watu waliofanikiwa wanatushauri kuyaweka malengo ya KULA na ADA ndani ya malengo makubwa zaidi (Utajiri). Tunahimizwa kuachana na utamaduni wa kuweka KULA na ADA kama malengo makuu katika maisha, kwasababu, kwa kufanya hivyo tutazidi kupoteza muda mwingi na matokeo yake hututakaa tupate muda wa kufanya mambo makubwa. 

Kwa mfano: “Ikiwa wewe unaishi DAR-ES-SALAAM na lengo lako kuu ni kwenda KARAGWE, maana yake, inabidi ujipange kutafuta jinsi ya kupata pesa itakayokuwezesha kufika KARAGWE. Pesa ya kufika KARAGWE ikishapatikana, maana yake ni kwamba sehemu zote za njiani kabla ya kufika mwisho wa safari yako kwa vyovyote vile, utafika sehemu zote za njiani japo hilo halikuwa lengo lako kuu. Sehemu za njiani ambazo kwa vyovyote vile lazima upite ni pamoja na Morogoro, Dodoma, singida, Tabora, Kahama n.k. Sehemu zote hizi utaweza kufika kwa kutumia nauli ile ile ya DAR-ES-SALAAM hadi KARAGWE” 

Mfano huo hapo juu, unatufundisha kwamba tunahitaji kuweka juhudi na maarifa yetu kwenye vitu vikubwa kama vile miradi ya maendeleo (majumba ya kupangisha, kilimo biashara, viwanda, biashara kubwa n.k). Tukiwekeza akiri zetu kwenye mambo kama hayo ni wazi kwamba pesa ya KULA na ADA za watoto zitapatikana humo humo ndani ya miradi hiyo. Kitu cha msingi hapa ni kuhakikisha tunajizuia kufanya kazi ya kutafuta pesa ya KULA na ADA kama malengo yetu makuu. Tusifanye KULA na ADA kuwa mwisho wa safari yetu BALI suala la pesa ya kula na ADA liwe ni sehemu za njiani kuelekea Kwenye ndoto kubwa (Utajiri). 

Wito wangu kwako msomaji ni wewe kuiambia akili yako na nafsi yako mwisho wa safari yako, yaani safari ya kuelekea kwenye maisha unayotamani kuishi. Naamini ukiweza kuiambia ukweli akili na nafsi yako, basi ujue hapo utakuwa umefikia hatua ya kutafuta pesa nyingi zaidi ya hiyo ya KULA na kulipa ADA. Ili linawezekana, limewezekana kwangu, limewezekana kwa wengine na hakuna sababu yoyote ya kutowezekana kwako.

ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO, JILIPE WEWE KWANZA

 Wapo watu wengi ambao wanakuwa na mipango mizuri sana kabla hawajawa na fedha, wanajua kabisa wakipata fedha watafanya nini na nini. Na tena watawashangaa sana wale wanaopata fedha na kuzitumia vibaya. Lakini subiri watu hao hao wazipate fedha, mipango yote inayeyuka, fedha zinatumika hovyo na mpaka zinapoisha ndiyo akili zinawarudia.

Kitu kimoja ambacho nataka kushauri leo kwa wale wote wenye shida ya kukaa na fedha, ni hiki; ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO.
Watu wengi linapokuja swala la fedha, hawana tofauti na makarani, ambao wanapokea fedha na kuzipelekeka zinapopaswa kwenda. Ukienda benki kuweka fedha na ukamkabidhi karani wa benki fedha zako, utaona kama anashika fedha nyingi, lakini mwisho wa siku fedha hizo habaki nazo yeye, bali anakabidhi zinapohusika.

Sasa watu wengi wamekuwa wanayaishi maisha yao kama makarani wa fedha zao. Kinachotokea ni hiki, mtu anafanya kazi au biashara na analipwa mshahara au kupata faida kama kipato chake. Anachukua kipato hicho na kwenda kulipia vitu na kununua vitu mbalimbali. Mwisho anabaki hana fedha kabisa.

Alichokifanya mtu huyu ni kuchukua fedha kwenye kazi au biashara na kwenda kuitoa kwa wale wanaomdai au wanaouza vitu mbalimbali. Mwisho wa siku anabaki hana hata senti moja.

Acha mara moja kuwa karani wa fedha zako, kwa kuzihamisha kutoka unakozipata na kuzipeleka kwenye matumizi na wewe kubaki huna kitu.
Na ipo njia moja rahisi kwako kuacha kuwa karani wa fedha zako, njia hiyo ni KUJILIPA WEWE MWENYEWE KWANZA.

Kwa kila kipato unachoingiza kwenye maisha yako, kabla hujapeleka kwenye matumizi yoyote, toa sehemu ya kipato hicho na iweke pembeni. Sehemu hiyo ya kipato uliyoitoa ndiyo malipo yako kwako na hupaswi kuitumia kwa shughuli nyingine yoyote ya matumizi. Hichi ni kipato ambacho utakiwekeza zaidi ili uweze kufanikiwa zaidi.

Sasa najua ni vigumu kukaa na fedha, kwa sababu kama wanavyosema watu, fedha huwa hazikosi matumizi. Ukishakua na fedha, dunia itahakikisha unazitumia kwa namna yoyote ile. Hivyo vitu vitaharibika, watu wataumwa utashangaa unapokuwa na fedha ndiyo unapokea simu nyingi zikitaka utoe msaada fulani.

Hivyo kuna njia nyingine bora kabisa ya kuhakikisha kile unachojilipa hakipati matumizi na ukakipoteza. Njia hiyo ni KUJENGA GEREZA LA AKIBA YAKO. Kile kiasi ambacho unajilipa wewe mwenyewe, kitengenezee gereza, ambapo ukishaingiza, huwezi kutoa tena, hata itokee nini. Hata uwe na dharura kiasi gani, gereza hilo halikuruhusu uondoe fedha ulizoweka.

Gereza la fedha zako ni mfumo wowote unaokuruhusu kuweka fedha lakini kutoa inakuwa siyo rahisi. Na unaweza kufanya hivyo kwa kuwa na akaunti maalumu ya benki ambayo inakuruhusu kuweka lakini siyo kutoa. Unaweza pia kufanya uwekezaji wa moja kwa moja ambao utafanya kupata fedha yako kuchukue muda. Lakini pia unaweza kuweka mpango na mtu au watu wengine, na mkawa mnaweka fedha lakini hamtoi.
Angalia njia inayokufaa wewe, ambapo ukiweka fedha, inakuwa vigumu sana kwako kuitoa, na hilo litakusaidia kujiwekea fedha zako kulingana na mipango uliyonayo.

Hivyo nimalize kwa kukumbusha mambo muhimu sana tuliyojadili hapa;
ACHA KUWA KARANI WA FEDHA ZAKO.
JILIPE WEWE MWENYEWE KWANZA.
TENGENEZA GEREZA LA FEDHA ZAKO.
Fanya hayo matatu na fedha yako itaweza kutulia, na utaweza kufanya makubwa. Ukishaweza kuituliza fedha yako, utaweza kuiwekeza na kupitia uwekezaji ndiyo utaweza kufikia utajiri na uhuru wa kifedha.

USIRUHUSU HISIA ZAKO ZIKUTAWALE , THIBITI HISIA ZAKO, USITAFSIRI TUKIO.

Moja ya changamoto kubwa zinazowapelekea wengi kushindwa kwenye maisha ni kuendeshwa na hisia badala ya wao kuendesha hisia zao. Wote tunajua kwamba pale tunaporuhusu hisia zitutawale, tunakuwa tumeondoa kabisa uwezo wetu wa kufikiri. Kwa sababu hisia kali na fikra haviwezi kukaa pamoja.

Kupitia falsafa ya ustoa, tunajifunza kwamba hisia ni kitu ambacho tunakitengeneza sisi wenyewe na hakuna anayetupa, hivyo tunaweza kuchagua kutoruhusu hisia zitawale maamuzi yetu.
Epictetus ana maneno mazuri ya kutuambia kuhusu hisia;
It isn’t the things themselves that disturb people, but the judgements that they form about them. Death, for instance, is nothing terrible, or else it would have seemed so to Socrates too; no, it is in the judgement that death is terrible that the terror lies. Accordingly, whenever we are impeded, disturbed or distressed, we should never blame anyone else but only ourselves, that is, our judgements. It is an act of a poorly educated person to blame others when things are going badly for him; one who has taken the first step towards being properly educated blames himself, while one who is fully educated blames neither anyone else nor himself. – Epictetus, Handbook, 5
Kinachotusumbua siyo kile kinachotokea, bali tafsiri yetu kwa kile kinachotokea. Kwa mfano kifo, siyo kitu cha kutisha, kama ingekuwa hivyo wanafalsafa kama Socrates wangekiogopa. Ni tafsiri yetu kwamba kifo ni kitu kibaya ndiyo inatusumbua. Hivyo hivyo, tunapokuwa tumekwazika, tumesumbuka au kupata msongo, hatupaswi kumlaumu mtu yeyote bali sisi wenyewe, kwa sababu hivyo vinatokana na tafsiri zetu wenyewe. Kwa asiyekuwa na elimu, huwalaumu wengine pale mambo mabaya yanapomtokea, anayeanza kujifunza hujilaumu mwenyewe wakati yule aliyeelimika hamlaumu yeyote wala hajilaumu yeye mwenyewe.