Maisha
ni malengo. Hakuna maisha ya mkato. Ishi kwa malengo. Tusiishi kwa sababu
tunaishi. Tuishi kwa malengo, kwa sababu Mungu ametuumba tuishi kwa malengo.
Ungana na Henry James kuamini maneno haya; “Ni muda mwafaka wa kuishi maisha
ambayo umeyafikiria kwa muda mrefu.’’
Binadamu
wengi wanaishi ni kwa sababu wanaishi. Hawaishi kwa malengo. Tunaishi maisha
yasiyo na utafiti. Tunapenda majibu mepesi kwa maswali magumu. Karne ya 21 siyo
karne ya kutafuta miujiza makanisani. Siyo karne ya kutafuta ushirikina kwa
waganga wa kienyeji ili kutajirika.
Si
karne ya ubabe wa kimadaraka. Si karne ya wizi wa mali za umma. Si karne ya
dharau na kebehi. Hii ni karne ya utafiti, ugunduzi na ushindani katika nyanja
zote zinazomhusu binadamu kama vile teknolojia inayoendana na wakati na tafiti
mbalimbali za kisomi. Kupanga ni kuchagua. Mwanafalsafa Benjamin Franklin
anasema, “Ukishindwa kujiandaa, umejiandaa kushindwa.”
Hakuna
anayepanga kushindwa ila wengi wanashindwa kupanga. Mwandishi Vicent Lombardi
anasema, “Kila mtu anapenda kufanikiwa ila ni wachache wanaopenda kujiandaa
kufanikiwa’’. Mantiki inatunong’oneza ukweli kwamba fikra zilizotufikisha
katika mazingira tuliyomo kwa sasa na hali tuliyonayo leo, fikra hizo kwa
uhalisia wake hazitaweza kututoa kwenye matatizo tuliyonayo kwa sasa.
Ukweli
wa niyasemayo hapo juu alipata kuusema mwanafizikia wa Kijerumani, Albert
Einstein [1879-1955], kwa maneno haya, “Hatuwezi kutatua matatizo kwa kutumia
namna ile ile ya kufikiri tuliyotumia katika kuyaanzisha matatizo’’. Tunahitaji
fikra tofouti. Tunahitaji fikra mbadala. Yatufaa kubadili gea sasa ili tuweze
kuupanda mlima wa mafanikio kwa usalama, uhakika na weledi. Gea hiyo ni kuanza
kuishi maisha kwa malengo.
Kuna
methali ya Kifaransa inayosema hivi; “Yeye anayengoja kuvaa viatu vya marehemu
anaweza kutembea pekupeku kwa muda mrefu’’.
Watanzania
tusisubiri viatu vya marehemu. Kusubiri maendeleo yatokee pasipo kufanya kazi
kwa bidii ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu. Kulalamika kwa kila
jambo pasipo kubuni mbinu na mikakati ya kukuinua kiroho, kimaadili, kisiasa,
kiafya na kiuchumi ni kama unaishi kwa kusubiri viatu vya marehemu.
Kukaa
na ukimsubiri mwanaume mwenye pesa ajitokeze kukuoa ni kama unaishi kwa
kusubiri viatu vya marehemu. Methali ya Kiswahili inaupambanua ukweli huo kwa
maneno haya, “Mtegemea cha ndugu hufa maskini.’’ Mtu anayeweza kukuokoa wewe ni
wewe. Ni wewe unayeweza kujiandikia historia nzuri au mbaya. Ni wewe unayeweza
kuwa chachu ya mabadiliko au mhanga wa mabadiliko. Ishi kadri ya uwezo wako,
usiishi kama watu wengine wanavyotaka uishi. Methali ya Kiswahili inatukumbusha
maneno haya, “Miluzi mingi humpoteza mbwa’’.
Watu
wengi walioshindwa kufanikiwa kimaisha, kiroho, kimaadili ni wale walioishi
kadri ya watu walivyowapendekezea waishi. Usijaribu kuishi kwa kumfurahisha
mwanadamu, ishi kwa kumfurahisha Mungu. Ukiishi kwa kumfurahisha mwanadamu, ipo
siku huyo mwanadamu uliyeishi kwa kumfurahisha atakusaliti. Mhubiri wa Injili,
Israel Ayivor, alipata kusema, “Yule aliyekusaidia kuzungumza mambo mabaya
kuhusu mwenzako, ndiye atakayemsaidia mtu mwingine kuzungumza uovu juu
yako’’.
Maneno
haya yana ukweli ndani yake. Yapo na si kwamba hayapo. Maisha hayaongozwi kwa
mihemko na papara zisizo na dira. Maisha hayaongozwi kwa dhuluma. Maisha
yanaongozwa kwa hekima, busara, maono na jitihada binafsi.
Huwezi
ukawa kama unavyotaka uwe kama hujawa na dhamira ya dhati ya kubadilika. George
Benerd Shaw alipata kuandika haya, “Maendeleo hayawezekani bila mabadiliko ya
fikra na wale ambao hawawezi kubadilika namna wanavyofikiri hawawezi kubadili
chochote”. Stephen Richards anaamini kwamba “Namna yetu ya kufikiri
inatengeneza matokeo mazuri au mabaya’’.
Ukosefu
wa fikra sahihi na bainifu kwa maisha ya mwanadamu yeyote yule ni ugonjwa. Ni
ugonjwa usioonekana kwa vipimo vya kisayansi lakini ni ugonjwa unaoua kwa
haraka sana kuliko magonjwa mengine. Ni ugonjwa unaoonekana kwa vitendo na kwa
uamuzi mbalimbali wa mhusika. Fikra sahihi zinaishi. Badilika kwanza.
Badili mtazamo wako katika kufikiri. Badili mtazamo wako kwa kuupenda ukweli
ulivyo na uhalisia wake. Badili mtazamo wako kwa kusoma tafiti za wasomi
mbalimbali, vitabu, magazeti, na majarida mbalimbali. Lisilowezekana
linawezekana kwa kubadili namna ya kufikiri. Maisha ni malengo. Baba wa kiroho,
Sai Baba, alipata kuyatafsiri maisha kwa namna hii:
“Maisha
ni wimbo, uimbe,
Maisha
ni mchezo, ucheze,
Maisha
ni changamoto, ikabili,
Maisha
ni ndoto, ielewe,
Maisha
ni sadaka, itoe,
Maisha
ni upendo, ufaidi,
Maisha
ni lengo, lifikie,
Maisha
ni kengele, igonge,
Maisha
ni barabara, ipite,
Maisha
ni mti, upande.’’
Kwa
hakika maisha ni wimbo, imba kadri ya uwezo wako. Maisha ni mchezo, cheza kadri
uwezavyo. Maisha ni changamoto, kabiliana na changamoto unazokutana nazo katika
maisha yako. Maisha ni ndoto, timiza ndoto ulizonazo katika maisha yako.
Msanii
wa nyimbo za ‘Hip-hop’ ambaye pia ni Mbunge wa Tanzania, Jimbo la Mbeya
Mjini, Joseph Osmund Mbilinyi, katika kibao chake cha ‘Muziki na Maisha’
anatufundisha falsafa inayosema, “Maisha ni ubishi’’.
Maisha
ni kuanguka na kuinuka. Ukianguka inuka. Ukianguka amini unaweza bado
kufanikiwa kwa kiasi kikubwa. Virgil anasema, “Wanashinda wale wanaoamini
wanashinda.’’ Mungu ni dereva wa maisha yetu. Tumwamini yeye na hakika
tutashinda. Jinsi uyaonavyo maisha yako huumba maisha yako. Maisha tunayaona
kama kitendawili kisicho na jibu kwa sababu tulio wengi tunaishi maisha yasiyo
na malengo. Umefika wakati sasa wa kuacha kuishi maisha ya kimazoea.
Kama
unataka maisha yako yawe na mvuto mkubwa yape mhuri wa malengo. Maisha bila
malengo ni kama suruali isiyo na zipu!. Katika filamu ya ‘’Chariotos of fire’’,
mkimbiaji wa Olimpiki aitwaye Eric Liddell anasema, “Mungu aliniumba kwa
malengo.’’ Kama anavyosema kwa ufasaha kabisa Ethel Waters kwamba, “Mungu
haumbi takataka.’’
Kuna
watu wanaofikiri kwamba wapo duniani kwa bahati mbaya. Sio kweli. Hapa duniani
hakuna binadamu aliyeumbwa kwa bahati mbaya. Mchungaji Rick Warren anasema,
“Hapo zamani kabla hujawa katika tumbo la mama yako ulikuwa katika mawazo ya
Mungu’’. Kuzaliwa kwako hakukutokana na makosa wala bahati mbaya. Mungu hana
sifa ya kukosea. Mungu hana sifa ya kubuni. Mungu ana sifa za uhakika. Mungu
ana sifa ya umilele. Uko hai kwa sababu Mungu alitaka kukuumba ili uwe sehemu
ya viumbe walioumbwa na Mwenyezi Mungu.
Upo
ukweli unaopendwa kutumiwa na watu wengi sana, ukweli huo unasema hivi, “Kazi
ya Mungu haina makosa.’’ Ni ukweli kwamba hujaumbwa kwa makosa wala kwa bahati
nasibu. Mwanasayansi Albert Einstein anasema, “Mungu hachezi bahati nasibu’’.
Mshairi Russel Kelfer anasema,‘’Wewe ni wewe kwa kusudi. Wewe ni sehemu ya
mpango wa ajabu. Wewe ni wa thamani na chombo maalumu kikamilifu. Unaitwa mtu
mwanaume au mwanamke maalumu wa Mungu’’. Biblia Takatifu inasema, ‘’Umeumbwa
kwa namna ya ajabu.’’
ITAENDELEA---MAKALA toka GAZETI LA JAMHURI , 08/06/2016