Saturday, May 14, 2016

DC KINONDONI ANUSA JIPU MSD


AlihapydcNA TUNU NASSOR, DAR ES SALAAM

MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, Ally Hapi, ameituhumu Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kwamba imechangia kudhoofisha huduma za afya katika hospitali zilizopo wilayani kwake.
Mbali na hilo, mkuu huyo wa wilaya alisema MSD wanafanya udalali kwa kuchukua fedha za hospitali za Serikali na kwenda kununua dawa katika maduka ya jumla ya watu binafsi na kuwauzia kwa bei kubwa.
“Mganga Mkuu wa Wilaya amesema baadhi ya maduka hayo yanauza dawa ya Panadol kwa Sh 7,000 kwa kopo, moja, lakini MSD wanakwenda kununua huko na kuwauzia wateja wake (hospitali) kwa Sh 14,000,  haiwezekani taasisi ya Serikali kufanya udalali halafu tuangalie tu,” alisema Hapi.
Akizungumza na watoa huduma za afya katika manispaa hiyo, Hapi alisema utafiti alioufanya katika baadhi ya hospitali za manispaa hiyo, amegundua MSD imekuwa ikikwamisha huduma kwa kuchelewesha dawa.
Alisema sambamba na hilo, pia MSD hawatoi taarifa kwa hospitali husika kama dawa walizoagizwa zipo ama la, matokeo yake hospitali zinakaa muda mrefu bila kuwa na dawa na kusababisha malalamiko kwa wananchi.
“Mfano Hospitali ya Palestina (Sinza) nimekuta wameagiza dawa za Sh milioni 18, lakini MSD wamekaa kimya kwa wiki tatu na baadaye walileta dawa za Sh milioni 2 tu,” alisema Hapi.
“Licha ya kutoa dawa kidogo, MSD hawarudishi fedha walizopewa na kubaki nazo hivyo kuzifanya hospitali zishindwe kuagiza dawa kutoka vyanzo vingine.
“Namwomba Katibu Tawala wa Wilaya amwandikie Mkuu wa Mkoa kuhusu hili ili amjulishe Rais ikibidi atumbue jipu la MSD,” alisema.
Aidha Mkuu huyo wa Wilaya alizungumzia uhaba mkubwa wa vyandarua na mashuka katika hospitali za Palestina na Mwananyamala.
“Wanawake wanakwenda kujifungua na kukosa vyandarua hospitalini ina maana mna mpango wa kuwaambukiza malaria wakiwa hospitali?” alihoji.
Hapi alishangazwa pia na idadi kubwa ya  watumishi wa Hospitali ya Mwananyamala kwenda kusoma na kusababisha upungufu mkubwa katika hospitali hiyo.
“Hospitali ya Mwananyamala watumishi 50 wapo masomoni, ninataka kujua ni nani anayetoa ruhusa hii bila kuzingatia mahitaji yaliyopo,” alisema.
Hapi pia alitaka kila mwezi kupata taarifa ya mapato na matumizi kwa Mkurugenzi wa Manispaa.
“Nasikia kuna watu wanalipana posho na fedha zinaisha…lazima tuwe wawazi katika hili,” alisema.
Aidha Hapi alimtaka Ofisa Biashara wa Manispaa ya Kinondoni kuangalia upya vibali vilivyotolewa kwa vilabu vya pombe vilivyozunguka baadhi ya hospitali na kupiga muziki kwa sauti kubwa hadi usiku wa manane.

CHANZO   CHA  HABARI :   GAZETI  LA  MTANZANIA, JUMATANO , 11 ,MAY ,2016.

MATIBABU YA WATOTO WENYE VICHWA VIKUBWA SHAKANI MOI

watoto wenye  vichwa vikubwaNA HADIA KHAMIS, DAR ES SALAAM

MATIBABU kwa watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi yapo shakani kutokana na kupungua kwa vifaa vya kusaidia matibabu yao.
Kwa sababu hiyo, Taasisi ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu (MOI) inaomba wahisani kujitokeza kuisadia vifaa  hivyo vijulikanavyo kama shanty, kwa ajili ya kutolea maji yaliyomo kichwani hadi tumboni kwa njia ya kawaida.
Akizungumza na MTANZANIA   Dar es Salaam jana, Meneja Uhusiano wa Taasisi hiyo, Almas Jumaa alisema mahitaji ya shanti ni makubwa kwa watoto wenye matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa.
“Vifaa hivi vina bei sana kwa wazazi wanaotoka mikoani hawawezi kuvinunua kwa vile  shanti moja inauzwa kati ya Sh 150,000 hadi Sh 120,000 ambayo hutegemea duka la dawa ambalo huenda kununua,”alisema Jumaa.
Wodi ya watoto wenye vichwa vikubwa hulaza watoto 50 ambao kama watafanyiwa upasuaji, shanti zilizopo haziwezi kutosheleza.
Jumaa alisema shanti moja inaokoa maisha ya mtoto mmoja hivyo kama jamii itajitokeza kusaidia shanti 10 na kuendelea maisha ya watoto wengi yanaweza kuokolewa.
Wakati huohuo, Jumaa alisema kwa sasa taasisi hiyo, haijaelemewa na wagonjwa kama ilivyokuwa kwa miaka iliyopita.
Alisema hadi jana wagonjwa waliokuwa wamelazwa   ni 304 ambako kuna   vitanda 340 huku kukiwa na upungufu mkubwa wa wagonjwa.

CHANZO  CHA  HABARI :  GAZETI  LA  MTANZANIA , JUMATANO, 11, MAY ,2016.

SARATANI YA KIZAZI TISHIO KWA WANAWAKE NCHINI


NA HERIETH FAUSTINE, DAR ES SALAAM

ZAIDI ya asilimia 69 ya wanawake walio katika umri wa kuzaa wana virusi vya Human Papilloma Virus (HPV) vinavyosababisha ugonjwa wa saratani ya shingo ya kizazi.
Pia zaidi ya asilimia 80 ya wanawake wenye ugonjwa huo hufariki dunia ndani ya miaka mitano kutokana na kutopatiwa matibabu mapema.
Hayo yalisemwa juzi na mtaalamu wa magonjwa ya saratani kutoka katika Asasi isiyo ya Kiserikali ya Tanzania Social Outreach Initiative (TASOI), Dk. Walter Kweka, wakati akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya magonjwa ya saratani.
Alisema ugonjwa huo huwashambulia wanawake ambao walianza mahusiano katika umri mdogo pamoja na wanawake wenye mpenzi zaidi ya mmoja ambao wanafanya ngono bila kutumia kinga pamoja na kansa ya kurithi kutoka katika ukoo.
“Kwa Tanzania inakadiriwa kuwa na wanawake zaidi ya milioni 14 walioko katika umri wa kuzaa ambao ni kati ya miaka 18 hadi 45, wako katika hatari kubwa ya kupata saratani ya shingo ya kizazi.
“Tafiti mbalimbali zinaonyesha kila mwaka kuna wagonjwa wapya 7,304 na 4,216 kati yao hufariki dunia kwa ugonjwa huo kutokana na virusi vya HPV, hivyo kila mwanamke aliyefanya ngono bila kutumia kinga ana hatari ya kupata saratani hii kama hana utaratibu wa kuchunguza afya yake,” alisema Dk. Kweka.
Kuhusu saratani ya matiti, alisema ugonjwa huo huwashambulia zaidi wanawake, na kwamba inakadiriwa kuwa katika Afrika Mashariki wagonjwa wapya kwa mwaka hufikia 18,000 na kati yao 10,000 hufariki dunia.
“Utafiti uliofanywa mwaka 2008 hapa nchini kulikuwa na wagonjwa wapya 2,500 ambao waligundulika na saratani ya matiti, lakini 300 ndio waliopatiwa tiba katika Hospitali ya Ocean Road Dar es Salaam,” alisema.
Alisema zaidi ya asilimia 90 ya wagonjwa wanaofika hospitali wanakuwa wamechelewa ambapo hufika katika hatua ya 3B na hivyo kushindwa kupona.
Dk. Kweka alisema katika idadi hiyo asilimia mbili hadi saba ya saratani ya matiti huwakumba wanaume.
Kuhusu saratani ya tezi dume ambayo imekuwa ikiwashambulia wanaume wenye umri wa miaka 55 hadi 70, alisema husababishwa na ulaji wa vyakula vyenye mafuta mengi pamoja na nyama nyekundu.
“Kwa hapa nchini tafiti zinaonyesha kuwa kati ya wanaume 1,200 na 1,300 hugundulika na ugonjwa wa saratani ya tezi dume kwa mwaka na wanaume waliokuwa na shida za mkojo waligundulika kuwa na ugonjwa huu,” alisema Dk. Kweka.

CHANZO  CHA  HABARI:  GAZETI  LA  MTANZANIA ,  Alhamisi , 12, May, 2016.

BASHE AWASHA MOTO BUNGENI

bashe
Na Bakari Kimwanga, Dodoma

WABUNGE wameendelea kuchangia mjadala wa bajeti ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, huku Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (CCM), akiitaka Serikali kutenga Sh bilioni 7.5 kwa ajili ya kuwakatia bima ya afya wajawazito kote nchini.
Amesema hatua hiyo itasaidia mkakati wa kupunguza vifo vya mama na mtoto kama ilivyo katika mkakati wa Serikali kuliko ilivyo sasa.
Bashe aliyasema hayo jana bungeni mjini Dodoma, akichangia bajeti ya wizara hiyo.
Alisema takwimu zinaonyesha wajawazito 42 hupoteza maisha kwa siku jambo ambalo ni hatari kwa Taifa.
“Mheshimiwa Spika, naliomba Bunge hili tupitishe kwa kuitaka Wizara ya Fedha na Mipango impatie Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu Sh bilioni 7.5 mwaka huu ili wajawazito wote wakatiwe bima ya afya kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF),” alisema.
Alisema takwimu zinaonyesha Tanzania ina wanawake milioni 1.2 ambao hujifungua kila mwaka chini ya mwamvuli wa NHIF kwa wastani wa Sh 50,400 kwa kila mwanamke.
Alisema wanawake ambao wanakwenda kliniki wanajulikana kwa kuwa taarifa zao zipo, hivyo wakikatiwa bima ya afya baada ya miezi tisa anakwenda kujifungua bila kwenda na kiwembe ama ‘glovsi’.
Akizungumzia suala la ukagutuaji wa madaraka (D by D), alisema kwamba sera ya afya inasimamiwa na Wizara ya Afya, lakini inashangaza suala hilo kupelekwa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).
“Mimi ninachotaka kusema katika nchi yetu tuna matatizo makubwa katika sekta mbili, sekta ya afya na elimu, haiwezekani sera wanaosimamia wizara utekelezaji TAMISEMI, sasa Bunge ni vema tuangalie suala hili la D by D, ni tatizo katika nchi yetu. Ni vema tuondoe hili TAMISEMI wabaki na miundombinu tu,” alisema huku akishangiliwa na wabunge wa pande zote.
Alisema haiwezekani wizara tatu zisimamie wizara moja ikiwemo Tamisemi na Utumishi kwani haitawezekana kupatikana kwa ufanisi.
Bashe alisema kwa mwaka huu wa fedha akabidhiwe waziri hospitali zote za mkoa na si tu za rufaa, itasaidia katika usimamizi wa sera, kusimamia utendaji katika hospitali husika, itasimamia uendeshaji na Tamisemi waachiwe jukumu la kuendeleza miundombinu peke yake.

CHANZO   CHA   TAARIFA :  GAZETI LA  MTANZANIA,   IJUMAA, 13 ,  MAY , 2016.

MZIMU WA GPA WAIBUKA BUNGENI


Mzimu wa GPA waibuka bungeni  

Profesa Joyce Ndalichako

Na Elizabeth Hombo, Dodoma

SERIKALI imesema itaendelea kuvitambua vyeti vya wanafunzi waliomaliza na kupangiwa madaraja katika mfumo wa GPA licha ya kurudi katika mfumo wa divisheni kwa sasa.
Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako ambaye alikiri kuwepo changamoto nyingi ambazo hutokea kulingana na mahitaji ya wakati husika na maoni ya wadau.
Akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara (Chadema), Profesa Ndalichako alisema mpango wa Serikali ni kupokea maoni kutoka kwa wanajamii kulingana na mahitaji ya wakati huo na mfumo wa marekebisho nayo hufanywa kulingana na nyakati.
Katika swali lake la msingi, Waitara alitaka kujua lini Serikali itapeleka bungeni marekebisho ya sheria ya NECTA kwenye kifungu hicho ili kuondoa nguvu ya waziri kutoa maelekezo bila kuhoji wala kushirikisha wataalamu wa elimu.
Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Stella Manyanya, alisema kifungu hicho kinampa mamlaka waziri mwenye dhamana ya elimu kufanya maamuzi kwa niaba ya Serikali pale inapolazimu.
Alisema maamuzi hayo huzingatia wakati, mazingira halisi na matokeo ya tafiti mbalimbali kutoka kwa wataalamu pamoja na maoni ya wadau wa elimu ambapo Baraza la Mitihani hutakiwa kuyatekeleza.
“Serikali kwa sasa haina mpango wa kukifanyia marekebisho kifungu hicho cha Baraza kwa kuwa kinamwezesha waziri kutekeleza mahitaji ya wakati huo.

CHANZO    CHA  HABARI :   GAZETI  LA   MTANZANIA, Ijumaa, 13 , May, 2016.

JPM : WALIOUA FAMILIA WAKAMATWE HARAKA


1*Ataka wananchi wamwabudu Mungu maovu kama hayo yasitokee
Anna Luhasha na Judith Nyange, Sengerema
RAIS Dk. John Magufuli amesema amesikitishwa na mauaji ya kinyama ya watu saba wa familia moja waliokatwa mapanga katika Kijiji cha Sima wilayani Sengerema mkoani Mwanza.
Kutokana na hali hiyo, Rais Magufuli ameviagiza vyombo vya dola kuwasaka kwa nguvu zote, watu waliohusika na mauaji hayo na kuhakikisha wanatiwa mbaroni ndani ya kipindi kifupi.
Akitoa salamu za pole nyumbani kwa wafiwa jana, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, alisema Rais Magufuli ameguswa na tukio hilo na kusema umefika wakati wa wananchi kumwabudu Mungu ili maovu kama hayo yasitokee.
“Wakati nakuja huku, Rais Magufuli amenituma nimfikishie salamu zake za rambirambi kwa ndugu, jamaa na marafiki mliofiwa.
“Ameagiza vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha vinawasaka na kuwatia mbaroni watu waliohusika na tukio la kinyama ili wafikishwe kwenye vyombo vya sheria,” alisema.
Alisema Rais Magufuli ametaka wahusika wote wakamatwe ndani ya kipindi kifupi, kwa sababu mauaji ya aina hiyo hayakubaliki hata kidogo.
Samia alisema Rais Magufuli amewataka wananchi kumcha Mungu kwa kuwa wakishika imani na kumwabudu maovu yatapungua.
Alisema jamii ya wacha Mungu haina maovu mengi kama hayo.
Kuwasili kwa Samia katika msiba huo, kuliamsha vilio vingi kutoka kwa wananchi waliokuwapo.
Samia alitembelea sehemu ambayo ujenzi wa makaburi matano ulikuwa unaendelea kwa gharama za Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema.

MAZISHI
Miili ya watu hao watano inatarajia kuzikwa leo kijijini Sima.
Akizungumza na MTANZANIA jana, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Sengerema, Yanga Makaga, alisema halmashauri inagharamia gharama zote za mazishi kama alivyoagiza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella.
Alisema miili ya marehemu wawili itasafirishwa kwenda wilayani Ngara mkoani Kagera kwa mazishi kwa sababu walikuwa wafanyakazi wa mashamba.
“Jukumu letu tunagharamia usafiri, kuandaa majeneza na kuwasafirisha marehemu Samson na Donald ambao watazikwa Ngara. Tumekamilisha taratibu zote,” alismea Makaga.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Sengerema, Julius Chalya, alisema shughuli ya utayarishaji wa majeneza na ujenzi wa makaburi kwa ajili ya kuhifadhi miili ya marehemu imekamilika.
Watu hao waliuawa kinyama kwa kukatwakatwa mapanga usiku wa manane, kuamkia Aprili 11, mwaka huu baada ya familia hiyo kuvamiwa na watu ambao idadi yao haijafahamika wakiwa wamelala katika nyumba tofauti.
Taarifa zilizopatikana wilayani Sengerema na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi, zinasema mauaji hayo huenda yamefanywa na watu wawili au mmoja na chanzo chake hakijajulikana.
Mmoja wa wanafamilia, Patrick John akielezea tukio hilo mbele ya Kamati ya Ulinzi na Usalama, aliwataja waliouawa kuwa ni pamoja na Augenia Kutega (64), mama wa familia hiyo ambaye kabla ya kushambuliwa na mapanga hadi kupoteza uhai, alilazimishwa kutoa Sh 40,000.
Wengine ni Mariam Philipo ambaye ni mdogo wa Augenia, watoto Leonard Alloys na Leonard Thomas ambao ni wanafunzi wa Shule ya Msingi Sima, Donald na Samson ambao walikuwa wafanyakazi wa shambani.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella alifika kijijini hapo akiwa na wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa na kuagiza Jeshi la Polisi kuwasaka wahusika na ndani ya saa 48 wawe wamekamatwa wakiwa hai au marehemu.


CHANZO   CHA  HABARI :  GAZETI  LA MTANZANIA , Ijumaa , 13,  Mei , 2016.

MBUZI WA TAMBIKO AUA WATU WATANO WA FAMILIA MOJA


NA WAANDISHI WETU
VILIO, simanzi na hofu vimetanda kwa wakazi wa Kitongoji cha Lotii, Kijiji cha Mwitikira, Tarafa ya Olboloti, Wilaya ya Kiteto mkoani Manyara baada ya watu watano wa familia moja kufariki dunia kwa namna ya kutatanisha.

Watu hao wanadaiwa kufikwa na mauti baada ya kula nyama ya mbuzi iliyotolewa kutekeleza mila ya kutatua mgogoro uliojitokeza katika familia mbili zilizopo Kijiji cha Kaachini kilichopo wilayani humo.
Akisimulia tukio hilo la aina yake kijijini hapo, mmoja wa majirani wa familia hiyo, Juma Kijaji, aliliambia  MTANZANIA kwa simu jana kuwa chanzo cha tukio hilo ni ugomvi kati ya familia ya Kilangazi Mbao na majirani zao (majina tunayo).
Kijaji alisema kuwa awali familia hizo zilikubaliana kulipana mbuzi baada ya kutofautiana katika masuala kadhaa kulingana na mila na desturi za jamii yao.
Alisema baada ya siku sita, walikubaliana mbuzi huyo achinjwe na nyama hiyo igawanywe kwa majirani wengine katika kitongoji hicho.
“Hata hivyo siku chache baadaye kulizuka uvumi kijijini hapa kwamba nyama hiyo haikupaswa kuliwa na familia ya Mzee Mbao, jambo ambalo lilifuatiwa na vifo vya mfululizo kutoka familia hiyo,” alisema.

MWENYEKITI WA KITONGOJI
Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Ally Msambo, aliieleza Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Kiteto kuwa kabla ya vifo hivyo, wanafamilia hao walivimba mwili mzima.
Msambo aliwataja wana familia waliotangulia kufariki dunia kuwa ni watoto wawili, Juha Mbao (3) na Mwajuma Mbao (5).
Alisema siku moja baadaye babu yao, Chirangas Mbao naye alipatwa na ugonjwa huo huo wa ajabu na kufariki dunia akiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Kiteto.
Katika mfululizo huo wa vifo, mtoto mwingine, Agnes Mbao naye alipoteza maisha na kufuatiwa na baba yake Chilangas Chilangas aliyefia katika kitongoji hicho baada ya kutoroka hospitalini na kukamilisha idadi hiyo ya watu watano wa familia moja kupoteza maisha katika mazingira ya kutatanisha.
Mwenyekiti huyo wa kijiji aliiambia kamati hiyo kuwa baada ya wanakijiji kushtushwa na vifo hivyo, walikubaliana kutozika miili ya mtoto na baba yake hadi kwanza wapate ufumbuzi wa kiini cha vifo hivyo.

MKUU WA WILAYA
Akisimua tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Kiteto, Samuel Nzoka, alisema hali hiyo imesababisha wananchi kuingiza imani za kishirikina kwa kudai kuwa kuna kitu kimefanywa ili kiweze kuwadhuru wanafamilia hao.
Alisema tukio hilo lilitokea mwanzoni mwa wiki hii katika kijiji hicho.
Nzoka ambaye alikiri kuwapo kikao hicho cha upatanishi, alisema mama mmoja ambaye mumewe na watoto wake walifariki katika tukio hilo, alienda kukopa mbuzi kwa jirani yake ambaye ni Mmasai.
Baada ya kupata mbuzi huyo, alitakiwa amchinje ili wananchi waliojitokeza kwenye kikao kilichokuwa kinafanyika kijijini hapo wale ile nyama.
“Baada ya kula nyama hiyo, mtoto wa mama huyo alifariki, siku iliyofuata alifariki mtoto mwingine na siku ya tatu alifariki baba mdogo wa watoto hao,” alisema Nzoka.
Alisema wananchi walichukua maiti hizo na kwenda kuzika, lakini baadaye alifariki mtoto mwingine wa familia hiyo.
“Siku iliyofuata (juzi) alifariki baba mzazi wa watoto hao, hali iliyosababisha kujitokeza kwa hofu kwa wananchi wa kijiji hicho na kudai kuwa mbuzi huyo amefanyiwa mambo ya kishirikina ili watu wa familia hiyo waweze kufariki.
“Nilikwenda jana (juzi) mimi na timu yangu ya madaktari kutoka wilayani kwa ajili ya kusikiliza malalamiko ya wananchi hao na kuchukua hatua stahiki kwa ajili ya kuchunguza tukio hilo,” alisema Nzoka.
Alisema baada ya kuzifungua maiti, zilikuwa zimevimba sana hivyo madaktari walizifanyia upasuaji kwa kuchukua sampuli kwa ajili ya uchunguzi zaidi kwa Mkemia Mkuu wa Serikali jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa madaktari ambaye alihusika kufanyia uchunguzi maiti ya watoto wawili waliofia hospitalini, alisema mapafu yalikutwa yameharibika.

VIFO VINGINE FAMILIA MOJA
Kutoka mkoani Mara, watoto wanne wakiwamo watatu wa familia moja wamekufa maji katika matukio mawili tofauti yaliyotokea ndani ya wiki moja Manispaa ya Musoma na wilayani Butiama.
Watoto watatu wa familia moja walikufa maji katika Kijiji cha Mirwa wilayani Butiama baada ya kunasa kwenye tope wakiwa wanaogolea kwenye mto Mei 9, mwaka huu, saa 8 mchana.
Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Leonard Chacha, aliliambia MTANZANIA kuwa watoto hao waliokuwa wakiishi na mama yao, Mtabutwa Cherehani, waliondoka nyumbani kwa lengo la kwenda kuoga mtoni.
Aliwataja marehemu hao kuwa ni Wambura Kizengo (11) mwanafunzi wa darasa la tano, Dismas Kizengo (7) mwanafunzi wa darasa la kwanza, wote katika Shule ya Msingi Mirwa na Mkirya Kizengo (4) mwanafunzi wa chekechea.
Chacha alisema baada ya kupata taarifa za watoto kupotelea mtoni, ilipigwa ngoma kwa ajili ya kuwakusanya wananchi kwa lengo la kwenda kuwakoa, lakini walipofika mtoni walikuta tayari wamefariki dunia.
Diwani wa Kata ya Mirwa, Pitalis Odero, alisema wamesikitishwa na vifo vya watoto hao.
Katika tukio jingine lililotokea Manispaa ya Musoma, mvua iliyoambata na upepo mkali iliyonyesha juzi jioni, imesababisha kifo cha mwanafunzi Benaderta Aley (12) aliyekuwa anasoma darasa la pili Shule ya Msingi Kamnyonge.
Kaka wa mwanafunzi huyo, Delta Aley, alisema mdogo wake akiwa na wenzake walikwenda kusaga mashineni, wakati wanarudi mdogo wake alianguka kwenye mtaro uliokuwa unapitisha maji kwa kasi na kusombwa.
Alisema mwili wa marehemu ulipatikana baada ya siku mbili ukiwa umbali wa kilomita mbili.
Habari hii imeandaliwa na MOHAMED HAMAD, MANYARA NA PATRICIA, KIMELEMETA, DAR ES SALAAM, SHOMARI BINDA, MUSOMA

CHANZO   CHA   HABARI :  GAZETI  LA  MTANZANIA,  Ijumaa ,13  Mei , 2016.