Wednesday, May 4, 2016

MAKONDA AWASHA MOTO WATUMISHI HEWA DAR




MKOA wa Dar es Salaam umebainika kuwa na watumishi hewa 209 ambapo, hali hiyo imefanya wakuu wote wa idara mkoani humo kula viapo vya kuchukuliwa hatua kama watabainika wengine kutoka katika idara wanazoziongoza.

Mkuu wa mkoa huo, Paul Makonda aliyasema hayo jana katika kikao kilichoshirikisha wakuu wote wa wilaya, idara kutokana na taarifa za uongo kuwa mkoa huo una watumishi hewa 71 tu.

Makonda alisema inashangaza kuona mkoa huo kuwa na watumishi hewa 71 hivyo aliamua kufanya uchunguzi na kubaini watumishi hewa wengine 209 ambao wameisababishia serikali hasara zaidi ya sh. bilioni 2.9 kutokana na fedha walizolipwa.

"Ndio maana kila Mkuu wa Idara amekula kiapo cha kuandika na kusema ili tukiunda tume ya uchunguzi na kubaini watumishi hewa wengine wao wahusike moja kwa moja. Tulifanya uhakiki wa kwanza Temeke, walituambia watumishi hewa wapo 13 na mara ya pili wakasema wapo 51, mbaya zaidi tulipofanya uhakiki mara ya tatu tukabaini wapo 64," alisema.

Aliongeza kuwa, ongezeko la wafanyakazi hewa katika wilaya hiyo linamfanya ajiulize maswali mengi yasiyo na majibu hivyo, hayupo tayari kuona jambo hilo likifanywa kwa kimzaha.

Alisema kila Mkuu wa Idara aliomba kazi kwa hiari yake, wengine walitumia rushwa ili waweze kuipata; lakini kazi wanazofanya lazima wasimamiwe au kuandikiwa memo ndipo wawajibike wakati majukumu yao wanayajua.

"Mkataba utaanza kutumika Jumatatu ijayo, kuanzia leo hadi wiki ijayo kila Mkuu wa Idara ahakikishe katika idara yake hakuna watumishi hewa, baada ya hapo ikiundwa Tume ya uchunguzi na kubaini watumishi hewa hawa wakuu watakuwa wanahusika," alisema.

Makonda aliongeza kuwa, haiwezekani Rais Dkt. John Magufuli kila siku azungumzie uchafu na watumishi hewa kwa kuitaja Dar es Salaam wakati wahusika wapo jambo ambalo haliwezi kukubalika kwani kila mmoja anapaswa kuwahudumia wananchi katika nafasi yake.

Katibu Tawala wa Mkoa huo, Theresia Mmbando alisema mkoa una watumishi 26,324 ambao kati ya hao, 166 ni wa Sektetarieti ya Mkoa, 26,158 Mamlaka ya Serikali za Mitaa, jiji lina wafanyakazi 254 na Manispaa ya Kinondoni 9,009, Ilala 8,710, Temeke 8,185.

"Awali Kinondoni waligundulika watumishi hewa 34, tulipofanya uhakiki mara ya pili tuliwapata 55, hadi sasa wamefika 89, Ilala tuliwapata 21 lakini mara ya pili wamekuwa 35.

"Baadhi ya watumishi inadaiwa wapo masomoni bila ruhusa, likizo bila malipo, walioazimwa, waliofariki hivyo jumla ni 209," alisema.

Hata hivyo, baadhi ya wakuu wa idara walilamikia kitendo cha kusainishwa mikabata na kusema ni sawa na kuwatoa kafara kwani wengine wanasainiwa na wakubwa bila wao kujua chochote.

CHANZO  CHA  HABARI:  GAZETI  LA MAJIRA,03, MEI , 2016