Kwa kawaida mtu anaanza
biashara kwa vile ameona mtu fulani akifanya hivyo, na anahisi kuwa
huduma au bidhaa hiyo inahitajiwa katika eneo fulani, naye anamudu kwa
kiwango fulani kuingia katika biashara hivyo. Kwa maana hiyo biashara
hasa ni kujua bidhaa au huduma inayohitajiwa eneo hilo, na kuwa tayari
kutumika kwa jambo hilo, na mengineyo ni mazingira binafsi ya kuweza
kufanya hivyo, kwa mfano kupata mtaji, na katika mazingira kadhaa ya
jamii, hata kuruhusiwa kufanya hivyo. Hiyo inagusa biashara za kina
mama; akiolewa, siyo rahisi kujishughulisha.
Kuna tayari daraja la
kisaikolojia ambalo linavukwa kabla ya suala lenyewe la kuanzisha
biashara kuanza, nayo ni ule utayari wa kuingia katika hali hiyo, yaani
kutumika. Pale kwa mfano mwanamke anapokuwa mama wa nyumbani mwenye
mwenza anayehakikisha kila kitu kipo, staha kwa upande wake itakuwa ni
kuweka nyumba katika mazingira mazuri yanayopendeza kwa wageni wakifika,
ili mwenza ajisikie kuwa yuko mahali panapofaa. Mara nyingi suala la
biashara linaendana na hitaji halisi kimaisha, au kwa wale walioenda
shule, kwa vile hawawezi tu kukaa.
Tayari hapo kuna
tofauti ya mtazamo, kuwa mtu anayehitaji kufanya biashara kutokana na
hitaji halisi la maisha, kwa mfano hata fedha ya kulipa pango kila
wakati, atakuwa katika hali tofauti ya kisaikolojia na yule anayehitaji
tu kuongeza kipato. Suala la mafunzo katika biashara hasa linakuja kwa
hawa ambao nia yao ni kuongeza vipato, kwa maana kuwa watahitaji
biashara zenye mazingira bora zaidi kuliko ya 'wabangaizaji.' Hapo ni
rahisi zaidi kuharibu mtaji ambao ni mkubwa.'
Mafunzo, kama ilivyo
elimu ya darasani kwa jumla, si kitu ambacho kinatumika kwa upana wake,
kuwa hili amefundishwa analifahamu, na kadhalika, ila kwa ufinyu wake,
kuwa liko jambo ambalo anayefundishwa atakumbuka, hasa kama atakutana na
suala kama hilo baada ya masomo. Kwa maana hiyo lengo halisi la kuwepo
mafunzo ya biashara ni kutoa dokezo la maeneo mengi, na hata kujua
'visa' vilivyowahi kutokea kuhusu chembe moja au nyingine ya uendeshaji
wa biashara. Kwa mtu mpya katika eneo hilo anajifunza mengi; mzoefu
anathibitisha tu kile ambacho anakijua, au ashangae kuna suala alikuwa
halifahamu, alaitambue.
Mfikiriaji wa Ujerumani
wa karne ya 19, Karl Marx ni kama alitatua suala hilo kwa msemo
uliovuma katika nyanja za fikra ya sayansi, licha ya kuwa labda hakuwa
wa kwanza kugundua hilo lakini akalivumisha. Alisema "hitaji moja katika
viwanda linatoa msukumo mkubwa zaidi kwa sayansi kuliko vyuo vikuu
kumi," yaani, ambavyo vinafanya tu utafiti, wa kubuni na hata kutunga
matatizo. Pale mtu anapojaribu kutatua tatizo halisi katika biashara,
akafaulu, siyo tu kuwa anawezesha biashara yake kuendelea, lakini anatoa
mchango hata katika fikra ya kuendesha biashara kama hiyo, kwa mfano
pale akitokea mtu afuatilie alichofanya.
Hiyo ina maana kuwa
yapo maendeleo yanayopatikana kila siku katika uendeshaji wa biashara
bila kuwepo darasa lolote kwa wale wanaofanya shughuli hizo, yaani
kutatua matatizo halisi ya uendeshaji wa biashara kwa kukutana nayo, si
kusoma kuhusu matatizo hayo. Kuna msemo unaotumiwa na mwanzilishi wa
kampuni ya habari na vitabu ya Global Publishers ambao unafupishwa kama
Street University - chuo kikuu cha barabarani. Kujifunza mbinu za
biashara wakati wa kuifanya, kwa kutatua matatizo, ni moja ya vielelezo
vya Street University, kufaulu mtihani wa maisha kwani biashara ni
maisha. Inaweza kuharibu utulivu wa mtu anapokwama.
CHANZO CHA HABARI :GAZETI LA MAJIRA NA JOHN KIMBUTE, Jumatatu,Januari ,20, 2014.