Monday, April 25, 2016

KUANZISHA BIASHARA NI KUCHAGUA LA KUFANYA , SI KUKOMALIA PESA





UTANGULIZI
 Kabla ya yote, ni lazima tutafute maana ya dhana hii ya ujasiriamali, kwani kuna mitazamo tofauti.

Sasa hebu tuielekee taasisi maarufu ya kijamii ya HakiElimu, ambayo kwenye chapisho lake liitwalo “Elimu ya Ujasiriamali: Kuelekea kwenye Maendeleo Endelevu Tanzania”, lililoandikwa na Chiraka Muhura linasema:

“2.0. Maana ya Ujasiriamali
Dhana ya ujasiriamali imeelezwa kwa namna tofauti-tofauti. Baadhi ya watu hufikiri kuwa ujasiriamali ni kufanya biashara tu. Baadhi wanauangalia ujasiriamali katika muktadha mpana unaohusisha ujuzi na maarifa ya mtu katika kutumia fursa zilizopo. Tranchet na Rienstra, (2009), kwa mfano, wanaelezea dhana ya ujasiriamali kama uwezo binafsi wa mtu wa kubadilisha mawazo na kuwa vitendo. Ujasiriamali unajumuisha ubunifu, kutengeneza kitu kipya na kuwa tayari kukabiliana na ugumu; vilevile kuwa na uwezo wa kupanga na kuendeleza miradi ili kufikia malengo. Dhana hii humsaidia mtu katika maisha yake ya kila siku akiwa nyumbani na katika jamii. Huwafanya waajiriwa kuwa na uelewa kuhusu muktadha wa kazi zao na kuwa katika nafasi nzuri katika kutumia fursa. Pia ujasiriamali hutoa msingi kwa wajasiriamali kujenga shughuli za kijamii au kibiashara. Olomi, (2009) anakubalina na dhana kuwa ujasiriamali kwa ujumla unaweza kuelezewa kama namna ya kufikiri, kutafakari na kutenda inayosababisha utengenezaji, uimarishaji, utambuzi na ufanyaji mpya wa vitu kwa maslahi ya mtu mmoja mmoja, kikundi cha watu na jamii.

Mwandishi George Jobu anayeandika kwenye Blogu ya “‘ujasiriamali’ dhana chanya katika maendeleo”, yenye anuani yake http://gjobu.blogspot,com, anatamka ifuatavyo:

Zifuatazo ni tabia za ujasiriamali.

    Kuthubutu
Hii ni tabia muhimu kwa mjasiriamali, tukizingatia uwezo na utayairi wa kuamua kuingia katika biashara fulani au mradi fulani, ukiondoa nidhamu ya woga. Watu wanaogopa hasara, hawajui jinsi ya kuendesha mradi.
    Nidhamu
Hii ni kanuni muhimu kwa mjasiriamali. Mjasiriamali lazima awe na nidhamu katika biashara yake, nidhamu katika matumizi ya pesa na nidhamu ya kufanya kakazi, na nidhamu kwa wateja wake wasimkimbie.
    Umakini na Werevu
Wale waliofanikiwa walikuwa tayari kufanya kazi na waliweka umakini mkubwa katika kazi waliyokuwa wakiifanya. Mjasiriamali anatakiwa kuwa makini kwa kila jambo.
    Kuwa na uwezo wa Kuongoza
Mjasiriamali anapaswa kuwa na uwezo wa kuongoza na kuamua. Inadaiwa kwamba uongozi ni karama ombayo mtu anazaliwa nayo au anapewa na Mungu. Mtu anaweza kuzaliwa na kipaji cha kuongoza, lakini anaweza kujifunza na akawa kiongozi mzuri.
    Kupenda Kufanya Kazi
Ni lazima mjasiriamali aipende kazi anayoifanya. Kama unaipenda kazi unayoifanya, haitakuwa mgumu, utafanya kitu ambacho kwako ni “hobby”, na utaifanya kwa bidii na maarifa.
    Uaminifu na Ukweli
Hii ni tabia muhimu kwa mjasiriamali. Wateja wanapenda mtu mwaminifu na mkweli. Mjasiriamali uwe mwaminifu na mkweli upate wateja wengi. Uongo katika biashara ni sumu.
    Dhamira
Mtu yeyote naweza kujiita mjasiriamali lakini mafanikio yanahitaji uelewa, kufanya kazi huku ukiwa umeweka mbele lengo au dhamira. Dhamira ya inahitajika kabla hujaingia katika biashara au mradi.
    Kwenda na wakati
Mjasiriamali lazima aende na wakati aweze kutambua mabadirilo yanayotokea katika masoko. Mjasiriamali hataachwa nyuma kwa kwenda na wakati katika ushindani wa kibiashara katika soko huria Pia kunatoa fursa kwa mjasiriamali kujua njia mpya za uzalishaji, ambazo ni pamoja na kusoma magazeti, kufanya utafiti na kurambaza katika mitandao mbalimbali.

Tabia ambazo zimeorodheswa hapo juu ni tabia za ujumla ambazo mjasiriamali anatakiwa kuwa nazo,lakini kama huna baadhi ya tabia hizo usifadhaike kwani ujasiriamalia ni somo na sio kipaji.

Kwa mujibu wa Benki ya Azania, katika kipeperushi chake kinachoitwa “Usishindwe Kuanzisha Biashara kwa Kukosa Maarifa”, “ili ndoto yako itimie” mjasiriamali anatakiwa kuzingatia yafuatayo:

1.    Nyambulisha na uainishe mradi unaotaka kufanya kwa msingi wa wazo linalotekelezeka

2.    Fursa ya biashara hutokana na yafuatayo
a.    Tathmini ya wazo lako la biashara.
b.    Tathmini ya kina ya mahitaji ya soko ambalo biashara yako italenga.
c.    Tathmini ya kina ya bidhaa zako na huduma zako.
d.    Tathmini ya kina na jinsi bidhaa yako/huduma yako itakavyokidhi mahitaji ya soko ulilolenga
e.    Fikiria na ufafanue walengwa/watumiaji wa bidhaa au huduma zako.
f.    Tathimini taratibu za kisheria na kiutawala kuhusu biashara unayotaka kuanzisha.

3.    Angalia ushindani uliopo sokoni (husisha yafuatayo)
a.    Angalia na uorodheshe biashara nyingine zinazotoa huduma/bidhaa kama unazotaka kutoa wewe.
b.    Angalia na ujiulize kama wapo washindani wengine wapya wanaotaka kuingia kwenye biashara hiyo hiyo unayokusudia.
c.    Jiulize changamoto zilizopo na vikwazo vilivyopo (kisheria, kimtaji, au vinginevyo) vinavyoweza kuzuia biashara nyingine zinazofanana na biashara yako kuanzishwa.
d.    Jiulize na uorodheshe upekee wa bidhaa/huduma zako (jiulize sababu za kumfanya mtu ahitaji bidhaa/huduma yako badala ya bidhaa/huduma nyingine zilizopo sokoni)

4.    Angalia uwezekano wa biashara yako kuendelea na kukua (ujibu yafuatayo)
a.    Utawafikiaje walengwa wa biashara yako (Ni kwa vipi walengwa wako watajua kuhusu bidhaa na huduma zako)?
b.    Utasambazaje/fikishaje bidhaa/huduma zako (Bidhaa zako zitafikaje kwa wauzaji wa rejareja au huduma zako zitafikaje kwenye maeneo uliyokusudia na maeneo hayo ni yapi)?
c.    Nini makadirio yako ya wafanyakazi unaohitaji kwa miaka miwili ya kazi (wafanyakazi wangapi utahitaji mwaka wa kwanza, na wangapi utahitaji mwaka wa pili)?
d.    Unahitaji ufanye nini ili biashara yako ipate faida na itachukua muda gani kuwa na faida?
e.    Nini matarajio yako ya mapato na matumizi kwa miaka 4 ya kazi (ni mapato na matumizi kiasi gani katika mwaka wa kwanza, mwaka wa pili, wa tatu na wa nne)?
f.    Unahitaji mtaji wa kiasi gani (kiasi gani cha fedha unachohitaji kuwekeza) katika mwaka wa kwanza,wa pili, wa tatu na wa nne ili kuendesha biashara yako?
g.    Utawezaje kupata kiasi hicho cha mtaji? Je ni kwa kuanza kuweka akiba katika benki au kuomba mkopo na kwa gharama gani?. Je mchango wako katika mtaji ni kiasi gani?
h.    Je mradi wako unaweza ukabeba gharama zinazotakiwa kiundeshaji na bado ukazalisha faida?

5.    Uzoefu wako katika ujasiriamali na uwajibikaji.
a.    Tathmini kiwango chako cha elimu na uzoefu wako unaohusiana na wazo lako la biashara na mahusiano uliyo nayo na wadau muhimu kisekta wewe kama mjasiriamali.
b.    Tathmini kuhusu wataalam wa fani mbalimbali ambao utahitaji kuwatumia katika maeneo ambayo wewe si mtaalam wala mzoefu ili kufanikisha uanzishaji na uendeshaji wa biashara yako.
c.    Kwa ufupi tathmini nia/malengo yako ya kutimiliza kuanza na kukua kwa biashara ukizingatia muda utakaotumia kupanga, muda unaokusudia kutumia katika mradi, kiwango cha fedha za kwako mwenyewe unachoridhia kuweka katika mradi n.k.”

Huo ni mtazamo wa kibenki, kwa mujibu wa Benki ya Azania.

HITIMISHO
Msomaji wa makala haya, hiyo ni mitazamo kutoka vyanzo 4 tofauti. Je, mwandishi wa makala haya ana mtazamo gani? Maoni ya mwandishi kuhusu ujasiriamali ni kama ifuatavyo:

    Kasumba ya kuamini kwamba kila kitokacho nje ya nchi – Ulaya, Marekani au Asia – ni bora kuliko kitengenezwacho hapa nchini ifutwe. Hii ni dhana potofu sana. Wapo wataalam lukuki, wabunifu wa “kujaza”, hapa nchini; wanadharauliwa kutokana na kasumba hii. Sasa tuwathamini, tuwatumie ipasavyo, tutaona neema itakayokuja. Mdharau kwao ni mtumwa!
    Mwisho, lazima utambue – wewe mjasiriamali – kwamba wapo Watanzania wengi wenye KUOGOPA MAFANIKIO. Wao hawajiamini, wanaogopa mafanikio, kwa hiyo, kila wamjuaye mwenye dhamira ya kujituma na kuwa mjasiriamali, wanajaribu kila mbinu kumkatisha tamaa, kwani wanaona kwamba kwa kuwa wao hawawezi kufanikiwa, basi, hakuna mwingine atakayefanikiwa. Achana kabisa na watu hawa. Usiwasikilize. Usiwaendekeze. Ujasiriamali unahitaji uwe “mbishi” katika maamuzi yako. Mtu akikuambia “huwezi”, wewe mwambie “Asante kwa kunipa moyo! Sasa naamini nitaweza!” Songa mbele, usirudi nyuma!

[Makala haya yamehaririwa na mwandishi kwa kurekebisha makosa ya lugha na kuyafupisha.]

Asanteni kwa kunisoma. Ni mimi mjasiriamali wenu, Paul Francis Mongi,Gazeti   la  Majira, Jumatatu ,January,20,2014.