Saturday, April 23, 2016

MIEZI MITATU KABLA SIMU BANDIA KUZIMWA , WATEJA WAHAHA KUZIBADILI




DESEMBA 18, mwaka jana Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) ilitangaza kuzifunga simu zote zitakazobainika kuwa bandia baada ya miezi sita ya mwanzo ya mwaka huu, yaani Januari Hadi Juni.
Kwa maana hiyo imebaki takribani miezi mitatu kutoka hivi sasa ili kuifikia Juni ambapo Mamlaka hiyo itazizima simu zote bandia na wamiliki wake hawataweza kupata mawasiliano.
Ukweli ni kwamba dunia ya sasa ni ya mawasiliano na kila mmoja  anapenda kuwa ‘hewani’ akiwasiliana na ndugu, jamaa na marafiki zake kila wakati.
Ndio maana matumizi ya simu za mkononi yamekua kwa kasi katika miaka ya karibuni duniani.
Mussa Mwaikyusa, mkazi wa Dar es Salaam, anasema alilazimika kununua simu ya mkononi  ili imsaidie kurahisisha mipango yake ya kibiashara.
“Mimi naishi hapa Dar es Salaam lakini natokea mkoani Mbeya huku nimekuja kwa lengo la kufanya biashara na familia yangu ipo mkoani Mbeya, huwa nachukua mizigo kule na kuja kuiuza huku hasa ndizi na viazi.
“Mara nyingi huwa natumia simu yangu ya mkononi kuwasiliana na familia yangu pamoja na kuwajulisha waniandalie mzigo mwingine pale ninapokaribia kumaliza ule nilionao,” anasema.
Mwaikyusa anasema alinunua simu yake hiyo aina ya Samsung katika duka moja hapa jijini Dar es Salaam kwa Sh 80,000.
“Ina mawasiliano vizuri lakini nimesikia habari kwamba TCRA itazizima itakapofika Juni na nimejaribu kuuliza kama walivyosema kujua kama ni halisi au bandia nikagundua kwamba ni bandia,” anasema kwa masikitiko Mwaikyusa.
Mwaikyusa hivi sasa yupo katika harakati za kununua simu nyingine mpya na anasisitiza kwamba kabla hata hajaondoka katika duka atakalonunulia ataingiza namba zilizotolewa na TCRA ili ajue kama na yenyewe ni halisi au la.
Mary Kazaula anasema aliwahi kununua simu kwa Sh 20,000 katika duka moja huko Kariakoo ambapo alipatiwa muda wa kuichunguza wa wiki mbili.
“Miaka mitatu iliyopita niliinunua na kwenda zangu nyumbani kabla hata wiki mbili hazijaisha nilishangaa imezima ghafla ikabidi niirudishe lakini hawakukubali kuipokea, nilisikitika kwamba nimepoteza Sh 20,000 yangu nikalazimika kwenda kununua nyingine ambayo nimedumu nayo hadi sasa na nimeingiza hizo namba za TCRA imeniambia kuwa ni halisi,” anasema.
Ukweli ni kwamba soko la Kariakoo ndilo eneo maarufu ambako wafanyabiashara wengi wanauza simu za kila aina kwa bei mbalimbali.
Na kwa miaka mingi wafanyabiashara hao wamekuwa wakiuza simu hizo ambazo  zinafanana na simu halisi na za aina tofauti bila kujali suala la ubora wa vifaa hivyo.
Kutokana na bidhaa feki kuwa zinakwepa kodi Tanzania imekuwa inapoteza kiasi kikubwa cha mapato kutoka kwenye mauzo na hata kodi ya ongezeko la thamani (VAT) na halikadhalika ushuru mwingine pamoja na tozo nyingine za serikali.
Kwa mujibu wa baadhi ya ripoti, simu  feki zilizojaa kwenye soko lisilo rasmi zinaunda takribani asilimia kumi ya mauzo duniani kote na kiwango hicho kinaweza kuongezeka. Simu feki zina madhara kwa watumiaji  na hata wapendwa wao.
Halikadhalika madhara mengine ni pamoja na uharibifu wa mtandao pamoja na kumiliki bidhaa zilizo duni.

 Tigo yapewa jukumu la kuhamasisha
Ili kuhakikisha kwamba elimu hiyo inafika vyema kwa jamii  TCRA  imeamua kuipa jukumu hilo kampuni ya simu za mkononi ya mtandao wa maisha ya kidigitali Tigo.
Akizungumzia hatua ya Tigo kutoa tahadhari kwa wateja wake Mkuu wa Idara ya Vifaa vya simu  wa kampuni hiyo, David Zakaria anawatahadharisha wateja kuhusu muundo na alama za biashara za bidhaa halisi zinazotumika  kulaghai wateja kabla ya kununua.
“Ili mteja aweze kuelewa iwapo simu zao ni feki  au ni halisi anatakiwa kupiga namba *#06# ambapo  atapokea  namba ya Utambulisho wa Kimataifa wa Vifaa vya Simu  (IMEI) ambapo pia inaweza kupelekwa kama ujumbe mfupi wa maneno (meseji) kwa namba 15090 ilikupata jibu kama  simu hiyo ya mkononi ni halisi au nifeki,” anasema Zakaria.
Kwa mujibu wa Ofisa Uhusiano wa Umma wa TCRA, Innocent Mungy kuchukuliwa kwa hatua hiyo ni kwa mujibu wa Sheria ya Mawasiliano na Posta  ambayo inaiwezesha Mamlaka kusimamia mawasiliano ya simu nchini na shughuli zinazohusiana ili kudhibiti uhalifu wakupangwa ambapo simu za mkononi zimekuwa zinaibwa na kuingizwa nchini.
“Kwa miaka minne sisi wenyewe tumekuwa tunajipanga pamoja na kampuni za simu zilizopo nchini ili kutekeleza jambo hili. Hitaji la kuzifunga simu feki linakwenda mbali zaidi ya  hitaji la nchi la kuondokana na bidhaa feki na kutokomeza  uhalifu wa kupangwa. Badala yake  unalenga kwenye afya na ubora na kutapakaa kwa bidhaa hizo,” anasema.
Anasema utambulisho IMEI una maanisha kuwa kila simu ya mkononi ina namba ya kipeke ya kuitambulisha hivyo kwamba endapo simu inaelezwa kuwa ni feki au imeibwa, namba hiyo IMEI itapelekwa kwenye Rajisi Kuu ya Utambulisho wa Vifaa (CEIR) ambayo ina wajibika kuifanya kifaa husika kisitumike kwenye  mtandao wowote duniani.
“Baadhi ya simu hizi za mkononi ambazo ni bandia hazijakidhi viwango vya mionzi vilivyowekwa na Shirika la Afya Duniani (WHO). Halikadhalika kuwepo kwa namba ya kipekee ya IMEI kuna mwezesha mteja  kuizuia simu yake iliyopotea kitendo ambacho kinazuia matumizi yake sehemu yoyote duniani,” anasema.
Anasema TCRA imefunga CIER ambayo itahakikisha, mbali na  kudhibiti  kupenyezwa kwa simu bandia, simu zilizoibwa zinaweza kufungwa na hazitaweza kutumiwa  tena.
Mungy anafafanua CEIR ni Rajisi Kuu ya Utambulisho wa vifaa ambayo  huhifadhiwa kwa ajili ya Utambulisho wa Kimataifa wa Vifaa vya simu (IMEI) na namba za simu zote zilizofungiwa ndani ya nchi.
“Pindi simu  ya mkononi inapoelezwa kuwa ni bandia au imeibwa namba ya rajisi yaani IMEI inaenda moja kwa moja CEIR na mara moja  simu hufungwa au kifaa hicho kuzuiwa kutumika tena duniani kote. Hivyo basi kifaa  kinapotambulika kama ni bandia au kimeibwa namba inayotambuliwa kimataifa hukizima,” anasema Mungy.
Anasema mwaka  2012 takribani wananchi wa Kenya  milioni 1.5 waliathirika kutokana na zoezi la  kuzifungia simu bandia  lililoendeshwa na Tume ya Mawasiliano ya Kenya (CCK) katika kuzitokomeza.
“Kwa maana hiyo Watanzania wanatakiwa kuchukua hatua za haraka ili kuachana na simu zao feki kabla ya siku hiyo haijafika,” anatoa wito.

CHANZO  CHA  HABARI :  GAZETI   LA   MTANZANIA.Na  VERONICA  ROMWALD , DAR   ES  SALAAM.  Jumanne , machi  15 ,2016.

MBARALI ILIVYOKWEPA WAZABUNI KUOKOA MILIONI 800 KUTENGENEZA MADAWATI


Wanafunzi wakiwa darasani.
CHANGAMOTO ya uhaba wa madawati katika shule nyingi za msingi nchini imeongezeka mara dufu mwaka huu kutokana na serikali kuanza utekelezaji wa mpango wa elimu bila malipo.
Shule nyingi zimejikuta zikiandikisha wanafunzi wengi waliojiunga na madarasa ya awali pamoja na darasa la kwanza.
Ukubwa wa changamoto hii umezilazimu halmashauri mbalimbali nchini kuibuka na mikakati ya kuweza kukabiliana nalo, miongoni mwa halmashauri hizo ikiwa ya Mbarali mkoani Mbeya.
Hii ni moja ya halmashauri sita zinazounda Mkoa wa Mbeya, ina shule za msingi 112, kati ya hizo 109 ni za serikali zenye wanafunzi 49,724, wavulana 24,079 na wasichana 25,645.
Mwanzoni mwa mwaka huu wilaya hiyo ilisajili wanafunzi 19,046 kwa madarasa ya awali na la kwanza, idadi ambayo ilikuwa takriban mara mbili ya kiwango kilichokuwa kikitarajiwa awali.
Fanikio hili likaja na changamoto ya ongezeko la uhaba wa madawati, ambalo tangu awali lilikuwa likiikabili halmashauri hii.
Tathmini iliyofanywa na wataalamu wa halmashauri ikabainisha kuwa shule za wilayani humo zina madawati 12,889 tu huku mahitaji yakiwa ni madawati 18,860.
Hii ikimaanisha kuna upungufu wa madawati 5,971.
Aidha, wataalamu hao wakapiga hesabu za wastani wa kila dawati kwa bei za kawaida za mitaani na kubaini kuwa halmashauri ingeweza kutumia zaidi ya Sh milioni 800 kuweza kuondosha tatizo hilo, kwa wastani wa kila dawati ni Sh 140,000.
Kiasi hiki ni kingi kwa halmashauri hii ambayo kwa kiasi kikubwa inategemea kilimo, huku miundombinu ya umwagiliaji ikiwa haijatosheleza, hivyo inakabiliwa na changamoto nyingi zaidi ya hiyo ya madawati.
Ndipo likaja wazo la halmashauri kuwa na karakana yake ili kutengeneza madawati hayo hali ambayo si tu kuwa itapunguza gharama za kutengeneza madawati hayo bali pia kutengeneza nafasi za ajira kwa vijana wenye ujuzi wa useremala wilayani hapo.
Mkakati huo utaiwezesha halmashauri hiyo kupunguza matumizi ya fedha za madawati hadi kufikia Sh milioni 235 kutoka milioni 800 ambazo ingetumia kama ingechukua wazabuni.
Upungufu huo wa gharama umetokana pia na ushirikishwaji wa wananchi katika kata zote 20 zinazounda wilaya hiyo, ambapo kila kata itachangia magogo yatakayochanwa na kupatikana mbao kwa ajili ya kufanikisha utengenezaji huo wa madawati.
Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Yeremiah Mahinya, anasema wana uhakika wa zoezi hilo kufanikiwa haraka iwezekanavyo, hasa kwa kuwa kumekuwa na mwitikio mkubwa wa wananchi katika kushirikiana nao ili kuondokana na tatizo la watoto kusoma wakiwa wamekaa chini.
“Ukiachilia mbali vijiji viwili tu ambavyo hadi sasa vimesuasua kuchangia magogo kwa ajili ya kuchana mbao, vijiji vingine vilivyosalia vilishatoa magogo ili kutatua tatizo la watoto kusoma katika mazingira magumu,” anasema mkurugenzi huyo.
Utekelezaji wa mkakati huu ambao uko katika awamu mbili, umeshashuhudia awamu ya kwanza ambayo ilipangwa kukamilika mwishoni mwa Februari mwaka huu, ikikamilika kwa utengenezaji wa madawati 4,281 huku sehemu ya pili ikitarajiwa kukamilika kwa kumalizia madawati 1,690 yaliyosalia.
Kwa mujibu wa mkurugenzi huyo, utekelezaji wa mpango huo ambao ulianza tangu mwaka 2014, ulianza kwa harambee ya uchangiaji madawati iliyokuwa imeitishwa na Mkuu wa Wilaya hiyo, Hussein Kiffu, ambapoSh 112,261,000zilipatikana.
Aidha, wananchi walishirikishwa ambapo waliombwa kuchangia Sh milioni 104, ingawa kiasi kilichokusanywa kilikuwa milioni 98 tu.
Wadau wengine kadhaa pia walijitokeza kusaidia kufanikishwa kwa mkakati huu ikiwemo Hifadhi ya Taifa ya Ruaha, ambao walichangia Sh milioni 7.
“Kwa ujumla tuliweza kukusanya Sh milioni 218 na hadi sasa tumeshatumia Sh milioni 216, ili kufanikisha awamu hii ya kwanza ya utengenezaji wa madawati,” anasema.
Hatua hii ya halmashauri ya Mbarali, ilimvutia naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jaffo, ambaye hivi karibuni alitembelea halmashauri hiyo kukagua shughuli za maendeleo pamoja na kukutana na watendaji wa halmashauri hiyo.
Mara baada ya kupokea taarifa ya utekekezwaji wa mpango huo, Jafo akazitaka pia halmashauri zingine nchini kuiga mfano huo wa kupunguza gharama za mahitaji mbalimbali ya kimsingi kama hilo la madawati kwa kuwa na karakana zao.
“Kwa kuangalia mchanganuo huu utaona ni kiasi gani halmashauri imeweza kuokoa kiasi kikubwa cha fedha ambazo zitatumika kwenye shughuli zingine za kuwaletea maendeleo wananchi na hili linawezekana kufanyika kwenye halmashauri zingine pia,” anasema Jafo.
Anasema ni lazima watendaji wawe wabunifu kwa sababu mahitaji ya wananchi ni mengi na yote ni ya msingi.
“Fedha zilizopo haziwezi kutosheleza kila kitu, kwahiyo kama kuna uwezekano wa kuwa na mikakati ya halmashauri kubeba baadhi ya kazi kwa kiwango hiki, mtakuwa mnaisaidia serikali kufikia malengo ya kuwaletea wananchi maisha bora kwa haraka zaidi,” anasema.
Aidha Naibu waziri huyo akatumia fursa hiyo kuagiza vijiji kadhaa ambavyo vilikuwa havijachangia magogo, kutekeleza agizo hilo haraka iwezekanavyo, la sivyo wachukuliwe hatua za kisheria kwani watakuwa wanahujumu harakati za kuwapatia wanafunzi mazingira mazuri ya kujifunzia.
“Misitu ni ya serikali, watoto wanaosoma ni wao na ni wetu sote, haiwezekani baadhi waone kuna umuhimu na kujitolea rasilimali walizonazo, kisha wengine wakaidi kufanya hivyo, hii ni kukwamisha harakati za halmashauri na za wananchi wenzao katika kuweka mazingira bora kwa wanafunzi kupata elimu,” anasema Jafo.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Amosi Makala, anasema kila halmashauri inatakiwa kuwa na takwimu sahihi juu ya uhaba wa madawati.
“Pamoja na juhudi kubwa ambazo zimefanywa na halmashauri mbalimbali zamkoa huu upande wa elimu, naomba wakurugenzi katika halmashauri husika wahakikishe wana takwimu sahihi hasa za uhaba wa madawati ili kuwezesha mkoa kuwa na mikakati ya uhakika ya kulishughulikia,” anaagiza mkuu huyo wa mkoa.

 CHANZO  CHA    HABARI :  GAZETI  LA  MTANZANIA,  Na   PENDO   FUNDISHA,  MBEYA. Ijumaa, Aprili    01 , 2106.

SERA YA ELIMU BURE INAVYOWATESA WAKENYA


CLASS TWO STUDENTS1284889194
KENYA imekuwa ikitajwa kuwa miongoni mwa nchi za Afrika zinazotoa elimu bora, japo wapo wanaopinga hilo, wakiwamo baadhi ya Watanzania.
Wanaoisifia Kenya kielimu, wanadai kuwa Wakenya wamekuwa na uelewa wa hali ya juu katika mambo mbalimbali kutokana na msingi uliojengwa katika elimu yao kuanzia ya awali hadi vyuoni.
Kwa wale wanaopinga hilo, wamekuwa wakidai kuwa kinachowabeba Wakenya dhidi ya raia wa nchi nyingine za Afrika Mashariki, ni uwezo wao mkubwa wa kuzungumza Kiingereza na si uelewa wa mambo kulingana na elimu yao.
Uwezo mkubwa wa Wakenya katika kuzungumza Kingereza, umetokana na mfumo wao wa elimu ambapo kuanzia ngazi ya awali, masomo hufundishwa kwa lugha hiyo, hali inayomfanya mtoto anapofikia umri wa kuanza shule ya msingi, kuwa fundi wa kuzungumza Kingereza.
Lakini pia, wapo wanaodai kuwa Wakenya si kwamba ni watu walioelimika zaidi ya wengine ndani ya ukanda huu, bali kinachowabeba ni ujanja wao wa kuchangamkia fursa mbalimbali, lakini pia ‘ushapu’ wao unaobebwa na uchapakazi wawapo sehemu ya kazi.
Hali hiyo imeelezwa kuwa tofauti na ilivyo kwa Watanzania ambao wengi wamedaiwa kuwa wavivu, wakitumia muda mwingi kupiga domo sehemu za kazi na kuendekeza zaidi starehe bila sababu zozote za msingi.
Hebu tuone mfumo mzima wa elimu nchini humo unaoelezewa kuwabeba Wakenya na kuonekana kuwa wataalam zaidi ya wakaazi wengi wa nchi nyingine za Afrika Mashariki na Kati kwa ujumla.
Kwa ujumla, elimu nchini Kenya imekuwa ikizingatia mfumo wa 8-4-4 tangu mwishoni mwa miaka wa 1980, ikiwa ni miaka minane ya elimu ya msingi, ikifuatiwa na miaka minne ya shule ya upili, kisha miaka minne ya taasisi au chuo kikuu.
Mbali na hayo, pia kuna sekta kubwa ya shule za kibinafsi ambazo hushughulikia watu wa viwango vya maisha ya kati na ya juu, ambao kwa ujumla hufuata mfumo wa elimu ya Uingereza wa elimu ya sekondari na msingi.
Kati ya watoto wote nchini Kenya, asilimia 85 huhudhuria shule za msingi, asilimia 24 huhudhuria shule za upili na asilimia mbili hujiunga na taasisi za elimu ya juu.

Elimu ya Msingi

Kuna aina tatu ya shule za msingi: Shule za kutwa ambazo zinajumuisha shule nyingi za msingi; shule za bweni ambazo zimegawanywa katika vitengo vitatu, vile vya gharama ya chini, wastani na za gharama ya juu; na shule za maeneo kame.
Elimu ya msingi katika shule za msingi za serikali ilifanywa kuwa ya bure na ya kila mmoja (si ya lazima) Januari mwaka 2003.
Mfumo wa Harambee (yaani kuungana pamoja) huchangia pakubwa katika utoaji wa elimu ya shule za msingi nchini humo. Mfumo wa Harambee hugharamia takriban asilimia 75 ya shule za msingi nchini Kenya. Mtihani wa kitaifa wa shule za msingi nchini Kenya hufanywa mwishoni mwa masomo ya msingi.
Kimani Maruge, ambaye ni Mkenya, ndiye aliyekuwa mtu mkongwe zaidi ulimwanguni kujiunga na shule ya msingi. Ni mkulima ambaye hakuwa amesoma, alijisajili akiwa na miaka 84 baada ya kufahamu kuwa masomo ya msingi yalikuwa ya bure ambapo alifariki mwaka wa 2009 akiwa na umri wa miaka 89

Elimu ya Shule za Upili

Wanafunzi nchini Kenya katika shule za sekondari huchukua miaka minne kujiandaa kwa masomo ya taasisi. Wanafunzi wengi huanza kuyajenga maisha yao ya usoni kwa kujiendeleza katika masomo yatakayowapa kazi.
Mtihani wa kitaifa wa kadato cha nne hufanywa mwishoni mwa masomo ya shule ya upili. Mwaka 2008, serikali ilianzisha mpango wa kutoa elimu bure kwa shule za upili.
Kuna vitengo vitatu vya shule za sekondari: Shule za kibinafsi, shule zinazofadhiliwa na serikali na shule za harambee. Shule zinazofadhiliwa na serikali zina ushindani mkali unaosababisha mmoja kati ya watoto wanne kukubaliwa kujiunga nazo.
Kujiunga na shule ya upili hutegemea alama za mwanafunzi katika mtihani wake wa darasa la nane (K.C.P.E) na kwamba shule nyingi zinazofadhiliwa na serikali ni za bweni.
Shule za Harambee hazina ushindani mkali na zinajumuisha asilimia 75 ya shule zote za upili nchini ambapo wanafunzi wanaopata alama za chini katika mtihani wao wa darasa la nane hujiunga na shule za harambee, shule za kibiashara au kuacha shule.
Vifaa katika shule hizo si vizuri kama vile vya shule zinazo fadhiliwa na serikali na mara nyingi hukosa vitabu, walimu waliohitimu, madawati na mengineyo.
Shule nyingi za kibinafsi huwa na mfumo wa elimu ya Uingereza , ukifuatiwa na elimu ya sekondari ya juu (A-level) ya kimataifa licha tu ya chache zinazofuata mfumo wa Marekani. Shule chache za kibinafsi hufuata mfumo wa KCSE kando na mifumo ya kigeni wakiwapa wanafunzi kuchagua ni upi wa kufuatwa.

Taasisi za elimu
Hizi ni taasisi zinazotoa elimu ya juu kwa miaka miwili au mitatu katika viwango vya cheti, diploma na diploma ya juu ya kitaifa ambapo taasisi hizo hutoa mafunzo ya kiufundi kwa kutumia ujuzi wa mikono katika nyanja mbalimbali kama vile uhandisi sayansi ya madawa, elimu, sayansi ya kompyuta na mengineyo.
Zinajumuisha vyuo vya mafunzo ya ualimu (TTCs), taasisi za mafunzo ya udaktari nchini Kenya (KMTC), Kenya Polytechnic, Mombasa Polytechnic, Eldoret Polytechnic, Tasisi ya mafunzo ya utangazaji na nyingine nyingi ambapo taasisi hizo zote huanzishwa na miswada mbalimbali ya Bunge.

Vyuo vya umma

Vyuo vikongwe zaidi nchini Kenya ni pamoja na Chuo kikuu cha Jomo Kenyatta cha Kilimo na Teknolojia, Chuo kikuu cha Egerton, Moi, Chuo kikuu cha Mseno na Chuo Kikuu cha Masinde Muliro cha Sayansi na Teknolojia (zamani Chuo cha Mgharibi).

CHANZO  CHA  HABARI:  GAZETI  LA  MTANZANIA,
Ijumaa,Aprili  01, 2016.