Friday, September 3, 2021

MITIHANI YA MAISHA HAINA MWISHO , UKISHINDA MTIHANI HUU UNAKUJA ULE.

Bila maandalizi maishani ni kukubali kushindwa au kufeli. Maandalizi hutusaidia kupunguza mawezekano ya kushindwa, kushangazwa au hata kuumia. Wanasema wakati wa vita sio wakati sahihi wa kufanya maandalizi isipokuwa kabla ya vita ndo ulikuwa wakati sahihi wa kujiandaa. Si hilo tu hata maisha ya kila siku bila maandalizi ya mapema ni mtu kujiandaa kushindwa au kuumia zaidi.

Imekuwa ni kawaida yetu sisi binadamu kutoweka uzito katika maandalizi ya mambo mengi maishani na hili linajitokeza kutokea kwa mambo yakitukuta hatukuwa na maandalizi yoyote yale. Inawezekana ni suala la kiuchumi, mahusiano au hata masuala ya kiafya huwa hatujiandai mpaka pale mambo yamejitokeza na kutuzindua kuwa tulipaswa kujiandaa mapema kabisa.

Maisha yamejaa mitihani na majaribu katika kila kona ya kuishi kwetu ikiwa ni kutufungua na kutukumbusha ilivyo haja kubwa ya kuwa na maandalizi mapema ya mambo hayo. Mambo mengi yanayojitokeza na tukayaona ni kama yametokea ghafla kama ajali ni kuwa hatukuwa na maandalizi nayo. Kila mtego ambao mtu anaweza kukutwa amenaswa ni kuwa hakugundua mapema kuwa ilibidi kujua ishara za awali na kujiandaa ili asijekushindwa katika mtihani huo. Wengi tumejikuta tunaanguka katika mambo mengi maishani sababu ya kuondoa nafasi ya maandalizi ambayo ilipaswa kuwepo kila siku.

Maisha hayaachi kutufundisha uhalisia wake kuwa kuna nyakati ngumu na nyepesi, furaha na huzuni, giza na nuru, kushuka na kupanda, kufaulu na kufeli na kuishi na kufa. Safari zote hizi hujitokeza na zinakuja wakati wowote ule ambao mtu anaweza asitegemee ingekuwa hivyo. Bila maandalizi ya kujua hilo ndo kunakozalisha kuyaona maisha yana sura moja tu ya kuwa ni magumu na yasoruhusu watu kuwa na furaha. Yote hujitokeza sababu ya mtu kukosa kujiandaa na kujua ukweli huu wa maisha kuwa wakati wowote ni safari ya maandalizi kwa kuwa mitihani haikosi kuwepo maishani.

Tunapaswa kujiandaa kukutana na kila aina ya watu ambao wanaweza kutufundisha vitu au kutuachia maumivu, wanaweza kutusaidia kukua au kutudumaza kabisa, watu wanaoweza kutuunga mkono au kutukatisha kabisa tamaa, watu ambao watafurahia hatua zetu au kutozifurahia. Aina ya watu hawa tunaweza kukutana nao katika safari ya maisha yetu ya kila siku. Tunapokosa kuwa tayari kujiandaa kwa hilo tunakubali kuumia na kushangazwa na mambo yatakapojitokeza.

Jiandae kwa kila hatua yako hasa pale ambapo upo karibu na watu wanaokuzunguka. Watu wanaotuzunguka wana uwezo mkubwa wa kutufanya tujikute tunaumizwa nao kwa vitu ambavyo wanaweza kuvifanya na tukabaki kushangaa kwa sababu huwa hatujiandai kuwa hata wanaotuzunguka ni watu wenye madhaifu na wanaweza kutuumiza pia. Mitihani ya maisha inaweza kuja kutoka eneo lolote na mtu anapokosa kujua hili tu ni kujiandaa kuumia na kushangazwa na mambo hayo.

Jiandae kwa kuyaweka mambo katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni lile lile la kuangalia mambo yaliyo katika uwezo wako ushughulike nayo na kundi la pili ni yale mambo yaso katika uwezo wako uyaache kama yalivyo au kuwa tayari kuishi nayo. Ni falsafa ngumu kuifuatilia ila inampa nguvu mtu katika kujiandaa na kukabiliana na mitihani maishani na majaribu mengi ambayo hujitokeza kutupima na kufungua uhitaji wa kujiandaa zaidi kila siku. 

JIUNGE  DARASA--ONLINE  "  UJIFUNZE   MENGI USIYOYAJUA  TUWASILIANE  SASA  NIKUUNGE KWA   DARASA. "

NA KOCHA   MWL. JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA

WhatsApp + 255 716924136  /    + 255  755 400128