Sunday, February 28, 2021

VITABU 31 VYA KUSOMA MWAKA 2021 ILI MAISHA YAKO YAWE BORA ZAIDI.

Inapokuja kwenye mafanikio, kila mtu ana maana yake.

Lakini kwa ujumla, mafanikio ni pale mtu anapokuwa bora zaidi ya alivyokuwa huko nyuma.

Kifedha kama ulikuwa na kipato kidogo na kikaongezeka, umefanikiwa.

Kimahusiano kama ulikuwa na hali ya kutokuelewana na wale wa karibu na ukaitatua, umefanikiwa.

Mwaka 2020 ulikuwa mwaka wa mengi, wengi walikuwa wanaomba uishe na kuanza mwaka 2021.

Lakini wale wote waliokuwa wanausubiri mwaka 2021 kwa hamu, wakiamini utakuwa tofauti na 2020, wamepigwa na butwaa, kwani mwaka 2021 unaonekana kuwa na changamoto zaidi ya 2020 na zimeanza mapema kabisa.

Kitakachobadili maisha yako siyo mabadiliko ya kalenda, bali mabadiliko yako binafsi.

Na mabadiliko yako binafsi hayatakuja kwa kuendelea vile ulivyo sasa, lazima ubadilike, swali ni unabadilikaje?

Ipo kauli inasema; unavyofikiri ndivyo unavyotenda, unavyotenda ndivyo unavyokuwa na unavyokuwa ndiyo hatima ya maisha yako.

Kumbe kama unataka kubadili maisha yako, basi sehemu ya kuanzia ni kwenye fikra.

Na njia rahisi ya kubadili fikra zako, ni kujifunza vitu tofauti, vitu vyenye manufaa, vitakavyokupa maarifa na hamasa ya kufanya makubwa zaidi.

Mwaka 2020, kupitia channel ya SOMA VITABU TANZANIA tulipata chambuzi za vitabu mbalimbali vya maendeleo binafsi.

Hapa nimekuchagulia vitabu 31 muhimu kwako kuvisoma (kwa kuanza na chambuzi zake) ili uweze kubadilika na kufanya makubwa 2021.

Karibu ujue vitabu hivyo na kwa kifupi unachokwenda kupata, kisha kama itakupendeza nikukaribishe kujiunga na channel ya SOMA VITABU TANZANIA, ili upate chambuzi zake kwa lugha rahisi kabisa ya Kiswahili.

Twende kwenye orodha.

1. Man’s Search For Meaning - Viktor E Frankl

Hitaji la kwanza na muhimu kabisa kwenye maisha yako ni kujua kusudi la wewe kuwa hapa duniani. Hapo ndipo wengi wanakwama na kujikuta wakiendesha maisha ambayo hawayaelewi.

Kupitia kitabu hiki, Viktor Frankl anashirikisha yale aliyopitia kwenye makambi ya mateso kwenye utawala wa NAZI wakati wa vita ya pili ya dunia. Kupitia uzoefu wake na wengine, Frankl aliweza kugundua njia tatu za mtu kujua kusudi la maisha.

Soma kitabu hiki, ujue kusudi la maisha yako na uanze kuliishi mara moja bila ya kuchelewa.

2. The 4-Hour Workweek - Timothy Ferriss

Unaweza kuwa unafanya kazi sana, uko bize kweli kweli, kila siku unachoka lakini mwisho wa siku hakuna matokeo makubwa unayozalisha. Na hata kipato unachoingiza bado hakikidhi mahitaji yako.

Tim Ferris kupitia kitabu hiki, anatuonesha jinsi ya kuweka vipaumbele vyetu vizuri, kuchagua kufanyia kazi yale yenye matokeo makubwa na kunufaika pia.

Fikiria kama ungeweza kupunguza muda wako wa kufanya kazi huku kipato chako kikiongezeka! Soma kitabu hiki na ujue jinsi ya kufanikisha hilo.

3. The Almanack of Naval Ravikant by Eric-Jorgenson

Kuna kauli maarufu kwamba fedha haiwezi kununua furaha, huku matajiri wakionekana kuwa na kila wanachokitaka lakini hawana furaha.

Hali ilikuwa hivyo kipindi cha nyuma kwa sababu wengi walipata utajiri wao kwa mchezo wa kupata na kukosa (zero sum), yaani ili mtu atajirike, ilibidi achukue kwa wengine, kupitia kuiba au kuwanyonya.

Lakini zama zimebadilika, sasa unaweza kuwa tajiri bila kuwaibia au kuwanyonya wengine. Teknolojia imekua sana kiasi kwamba unaweza kutajirika kwa kuwatajirisha wengine, kitu kitakachokupa utajiri na furaha.

Naval Ravikant anatushirikisha falsafa hiyo ya utajiri na furaha kupitia kitabu hicho, kisome kitakufanya uwe wa tofauti kabisa.

4. Principles - Life and Work - Ray Dalio

Huwa tunahangaika sana kwenye maisha na kazi kwa sababu hatuna misingi tuliyojiwekea na kuiishi, hasa wakati wa kufanya maamuzi.

Ray Dalio, kupitia uzoefu wake kwenye uwekezaji, anatushirikisha jinsi kuwa na misingi unayoifuata kunavyorahisisha kazi na maisha kwa ujumla.

Kitabu muhimu mno kusoma kwa kila anayetaka kujenga kampuni au biashara inayoweza kujiendesha bila hata ya uwepo wako huku ukiacha alama kubwa duniani.

5. The Alchemist - Paulo Coelho

Huwa tunahangaika kwenda mbali kutafuta hazina ya maisha yetu, wakati hazina hiyo ipo pale tulipo sasa.

Coelho kupitia riwaya hii anatuonesha maisha ya kijana aliyesafiri masafa marefu kutafuta hazina yake, mwisho wa siku akaikuta pale alipoanzia. Lakini kwenye safari nzima, alijifunza mengi kuhusu maisha.

Kila unalopitia kwenye maisha ni funzo na kabla hujaenda mbali kutafuta unachotaka, hebu anzia hapo ulipo sasa. Soma kitabu hiki, ni mwongozo wa kiroho na maisha kwa ujumla.

6. Atlas Shrugged - Ayn Rand

Kuna wimbi la mataifa mengi duniani kuona mfumo wa ubepari siyo mzuri na kujaribu kurudi kwenye mfumo wa ujamaa. Wimbi hili siyo jipya, limewahi kujaribiwa huko nyuma na matokeo yake hayakuwa mazuri, kwani watu wengi mno walikufa.

Ayn Rand, kupitia riwaya ya Atlas Shrugged anaonesha jinsi taifa linavyoanguka kama litapinga mfumo wa ubepari na soko huru na kukumbatia mfumo wa taifa kudhibiti kila kitu.

Ameonesha kitu anakiita mgomo wa kiakili, ambao wale wenye uwezo mkubwa na wanaozalisha wanakataa kukandamizwa na serikali huku wasio na uwezo wala kuzalisha wakibebwa.

Riwaya hii inatupa tahadhari kubwa ya jinsi mambo yanavyoanza kuharibika kidogo kidogo. Ni muhimu sana kwa zama tunazoishi sasa.

7. High Output Management - Andrew S. Grove

Kama umejiajiri au umeajiriwa, matokeo unayozalisha yanaathiriwa sana na aina ya usimamizi uliopo. Usimamizi unaweza kuchochea matokeo au ukayadidimiza.

Andrew kwa kutumia uzoefu wake anatuonesha jinsi tunavyoweza kupata matokeo makubwa kwenye kazi tunazofanya kwa kutengeneza usimamizi mzuri. Soma kitabu hiki, kuna mengi ya kujifunza kuhusu mahusiano ya kikazi.

8. The Innovator's Dilemma - Clayton M. Christensen

Ugunduzi wa teknolojia mpya umekuwa unayaweka makampuni makubwa njia panda. Na yanaposhindwa kuchukua hatua sahihi, yanakuja kuangushwa na vikampuni vidogo.

Kama upo kwenye kampuni au taasisi yoyote kubwa, unahitaji kujua jinsi ya kutumia teknolojia mpya kupiga hatua. Na hata kama uko kwenye taasisi ndogo au unaanzisha biashara yako, unapaswa kuwa na mkakati wa kutumia vizuri teknolojia kwa ukuaji, kitabu hiki ni muhimu kusoma.

9. Tao Te Ching - Lao Tzu

Wanaoongea sana hawajui, na wanaojua hawaongei sana, ni moja ya fundisho kubwa linalopatikana kwenye kitabu hiki.

Kitabu kinafundisha falsafa ya kiroho ya China ya kale, falsafa ya Tao ambayo inatufundisha kuishi kulingana na sheria za asili.

Kitabu ni kifupi na mafunzo yake yanagusa kila eneo la maisha, kisome.

10. The Fountainhead - Ayn Rand

Ayn Rand tena, hapa anaonesha vita iliyopo kwenye jamii kati ya kuwa tofauti na kufuata kundi.

Jamii inakupenda pale unapofanya kile ambacho wengine wanafanya na kimezoeleka, lakini hapo utalazimika kujipendekeza ili upate upendeleo, kitu kinachokuja kukuangusha baadaye.

Lakini ukichagua kuwa tofauti, ukichagua kufanya yale ambayo hayajazoeleka, jamii itakupiga vita, utakutana na vikwazo vingi, lakini kama utasimama imara, mwisho utapata ushindi mkubwa.

Niseme kama mtu umejiajiri au uko kwenye biashara au ndiyo unapanga kufanya hivyo, basi soma riwaya hii, misingi na misimamo ya Howard Roark itakusaidia sana, hasa kwa zama tunazoishi sasa.

11. Poor Charlie’s Almanack - The Wit and Wisdom of Charles T. Munger - Charles T. Munger

Charlie Munger ni mshirika wa Warren Buffet katika uwekezaji, wamekuwa pamoja kwa miaka 50 na wamekuwa wawekezaji wenye mafanikio makubwa.

Mafanikio yao yako kwenye kitu kimoja, kusoma vitabu. Munger ambaye ana miaka 90 anatumia asilimia 80 ya muda wake kusoma vitabu.

Kwenye kitabu hiki anatushirikisha hekima alizojifunza na kuzitumia kufanikiwa kwenye uwekezaji, anatuonesha makosa ya kuepuka wakati wa kufanya maamuzi ya kifedha.

Kama unafanya biashara au uwekezaji, Munger ni mtu unayepaswa kumsoma, maana anatufundisha jinsi ya kutengeneza mfumo wa kiakili wa kufanya maamuzi (Mental Modal).

12. The Black Swan - The Impact of the Highly Improbable by Nassim Nicholas Taleb

Kwa sababu tukio halijawahi kutokea, haimaanishi kwamba haliwezi kutokea. Hilo ndiyo kosa kubwa ambalo binadamu huwa tunafanya, tunaishi kwa mazoea na linatokea jambo ambalo hatujajiandaa nalo na linatusumbua.

Taleb kupitia kitabu hiki anatufundisha jinsi ya kuwa tayari kwa yale ambayo hayajawahi kutokea. Kila mtu anapaswa kusoma kitabu hiki.

13. Dune by Herbert Frank

Maisha, siasa, uongozi, dini na sayansi ni vitu vinavyojenga jamii yetu, vitu ambavyo vina mwingiliano mkubwa.

Kupitia riwaya ya Dune, Herbert ametuonesha jinsi mambo hayo yanavyoingiliana na madhara yake iwapo hayatafanyika vizuri. Herbert ameonesha hatari ya jamii pale inapokuwa chini ya kiongozi shujaa, kwani huwa hayaoni madhaifu yake na yanakuwa angamizo.

Kikubwa kabia kwenye riwaya hii, ni sala ya kuishinda hofu, sala inayokupa nguvu ya kukabiliana na chochote kile. Soma kitabu hiki, kinaendana sana na zama tunazopitia sasa.

14. The War of Art_ Winning the Inner Creative Battle by Steven Pressfield

Kama unafanya kazi yoyote ya kibunifu, iwe ni kuandika, kuchora, kutunga, kuandaa programu mbalimbali na mengine, unajua vita kubwa ambayo huwa inaendelea ndani yako.

Kila unapopanga ukae chini kwa ajili ya kazi ya ubunifu, kunatokea kitu cha kukushawishi uahirishe. Kupitia kitabu hiki, Pressfield anatupa mbinu za kushinda vita ya ndani yetu na kuweza kuzalisha kazi bora kabisa za kibunifu.

15. A Journal of the Plague Year by Defoe Daniel

Mwaka 2020 dunia ilijikuta ikisimama kwa sababu ya mlipuko wa Covid 19. Mwanzoni watu walikuwa na matumaini kwamba ni kitu kitakachopita na mambo yatarudi sawa tu. Lakini sasa tupo 2021 na hakuna dalili za mambo kurudi sawa.

Unaweza kufikiri hili ni jipya, kwamba ndiyo mara ya kwanza dunia inapitia hali kama hii. Lakini siyo kweli, kwani kwenye karne ya 16, mji wa London ulipatwa na mlipuko kama huu na cha kushangaza, makosa yaliyofanyika kipindi hicho, ndiyo tunayarudia sasa.

Dunia inapitia kipindi kigumu kutokana na mlipuko huu, ambapo matumaini yaliyokuwa yamepatikana kutokana na kugunduliwa kwa chanjo haraka, yamezimika ghafla kwa kuja kwa aina mpya ya kirusi cha ugonjwa huo ambacho hakizuiliki kwa chanjo zilizopo sasa.

Kwa kusoma kitabu hiki, tunajifunza makosa ya kuepuka ili kuweza kuvuka janga hili salama.

16. Zero to One - Notes on Startups, or How to Build the Future by Peter Thiel, Blake Masters

Kuna njia mbili za kuiboresha dunia, Ugunduzi na Utandawazi. Ugunduzi ni pale unapoanzia sifuri na kuja na kitu ambacho ni kipya kabisa. Utandawazi ni kuhamisha kile ambacho kimefanya kazi eneo moja na kufanya eneo jingine.

Kama unataka mafanikio makubwa, basi unapaswa kuwa mgunduzi, kwa kuanzia sifuri kwenda moja.

Peter Thiel, bilionea mwekezaji ambaye alianzia sifuri kwenye mengi, anatushirikisha jinsi ya kuweza kuja na ugunduzi utakaoibadili dunia na kutupa mafanikio makubwa.

17. The Hard Thing About Hard Things - Building a Business When There Are No Easy Answers by Ben Horowitz

Sheria ya kwanza kwenye mafanikio kupitia biashara na ujasiriamali ni kwamba hakuna sheria moja inayowafaa watu wote.

Hivyo pamoja na kujifunza kutoka kwa wengine, bado unapaswa kufanya maamuzi magumu wewe mwenyewe.

Horowitz, kupitia uzoefu wake kwenye kuanzisha na kukuza biashara mbalimbali, anatuonesha jinsi maamuzi yalivyo magumu na jinsi ya kufanya maamuzi sahihi. Kama upo au unapanga kuingia kwenye biashara, hiki ni kitabu ambacho unapaswa kusoma, kitakuandaa vizuri sana kukabiliana na ugumu wa safari.

18. The plague by Albert Camus

Kitabu namba 15 hapo juu kimeonesha maisha wakati wa mlipuko, hasa kwa wananchi wa kawaida, namna walivyokuwa wanapambana na hali ya mlipuko. Kitabu hicho kina matukio mengi ambayo yalikuwa ya kweli kabisa.

Albert Camus yeye aliandika riwaya iliyoelezea maisha wakati wa mlipuko, hasa kwa upande wa wapambanaji. Ni riwaya inayotuonesha wakati mgumu wanaokuwa nao wale walio mstari wa mbele katika kupambana na mlipuko. Kuanzia viongozi wa kisiasa, vingozi wa dini na wahudumu wa afya.

Wapo ambao wanaamua kusimamia ukweli na wapo wanaoukataa ukweli. Riwaya hii inatuonesha madhara ya yote hayo, inatuonesha jinsi mlipuko wa majanga unavyogusa kila eneo la maisha, hasa eneo la kiroho.

Kama unapata wakati mgumu wa kufanya maamuzi mbalimbali kipindi hiki cha mlipuko wa Covid 19, soma kitabu hiki, kitakupa msingi wa kufanya maamuzi sahihi.

19. How to Win Friends and Influence People by Dale Carnegie

Chochote unachotafuta kwenye maisha, kipo kwenye mikono ya wengine. Ukiwanyang’anya kwa nguvu hutakifurahia, lakini ipo njia ya kuwashawishi wao wenyewe wakupe unachotaka tena wakiwa wanafurahia.

Carnegie ametupa ufungu wa kuingia kwenye mioyo ya watu na kukubalika. Ametupa siri nyingi, moja wapo ni kutumia jina la mtu kwa usahihi.

Kitabu hiki ni cha kusomwa na kila mtu, kwa sababu kila mmoja wetu kuna kitu anataka kwa mwingine, ukiwa na ushawishi mzuri, utapata kila unachotaka.

20. Thinking, Fast and Slow-Farrar - Daniel Kahneman

Ubongo wetu una mifumo miwili ya kufikiri, wa kwanza ni wa haraka na unaotumia hisia, wa pili ni wa taratibu na unaotumia mantiki.

Makosa mengi tunayofanya kwenye maisha ni kwa sababu tunatumia zaidi mfumo wa kwanza kuliko wa pili.

Kahneman ameichambua vizuri mifumo hiyo miwili na kutuonesha jinsi ya kuitumia kufanya maamuzi ambayo ni bora. Kama umekuwa unafanya maamuzi kwa mhemko na yanakugharimu, soma kitabu hiki.

21. Bird by Bird - Some Instructions on Writing and Life - Anne Lamott

Kwa waandishi, unapokuwa na kazi kubwa ya kuandika ni rahisi kuahirisha kuliko kukaa chini na kuandika.

Mfano makala hii yenye vitabu 31 vya kusoma, kila mara nimekuwa najiambia nitaiandika, lakini naona mpaka nimalize vitabu vyote 31 itachukua muda.

Lakini nikakumbuka ushauri wa Lamott, kwamba kama una kazi kubwa ya kuandika, nenda kipande kwa kipande.

Kitabu hiki ni kozi fupi ya uandishi, tangu kupata wazo, kuandika, kuhariri mpaka kuchapa. Kama ni mwandishi au unataka kuandika, kitabu hiki ni muhimu kukisoma.

22. Fahrenheit 451 by Bradbury Ray

Riwaya nyingine inayoendana na zama tunazoishi, unaweza kuona orodha hii ya vitabu ina riwaya (novel) saba, na zote zinaendana mno na zama tunazoishi sasa.

Msingi wa riwaya ya Fahrenheit 451 ni jamii inayoangamia kwa sababu imeacha kusoma vitabu. Watawala wanafurahia hilo, kwa sababu watu hawafikiri tena, muda wote wanaangalia tv huku wakijazwa propaganda. Kikosi cha zimamoto kimepewa kazi ya kusaka na kuchoma vitabu vyote vilivyosalia.

Umeshaona jinsi inaendana na zama hizi? Iko wazi, watu kwa sasa hawasomi tena vitabu, ila muda wote wapo kwenye mitandao ya kijamii, wanajazwa propaganda nyingi na hawawezi tena kufikiri kwa usahihi.

Tushukuru bado vitabu havijapigwa marufuku, lakini hatujui siku zijazo, huenda sisi wasomaji tukaonekana ndiyo kikwazo na vitabu vikaanza kupigwa marufuku. Hivyo tusome vitabu, tufikiri kwa akili zetu na kuyaishi maisha yenye maana kwetu na siyo kufuata tu mkumbo.

Soma kitabu hiki kama unataka kuwa na maisha huru, kufikiri kwa akili yako na kufanya maamuzi yako mwenyewe.

23. Surely Youre Joking, Mr. Feynman (Adventures of a Curious Character) by Richard P. Feynman, Ralph Leighton

Kuna watu huwa wanachagua kuyaishi maisha yao na kwa namna wanavyoyaishi, wengine wanahamasika kuchagua kuishi maisha yao pia.

Mmoja wa watu hao ni aliyekuwa mwanafizikia Richard Feynman, huyu alifanya kazi ana kwa ana na akina Albert Einstein, Niel Bohr na wanasayansi wengine wakubwa ambao tumesoma nadharia zao kwenye vitabu.

Feynman alikuwa ni mtu mwenye udadisi mkubwa, ambaye hakuwa anakubaliana na kitu kwa sababu wengi wanakubaliana nacho, badala yake alikuwa anajaribu kila kitu yeye mwenyewe.

Kuna mifano mingi mno ya jinsi alivyojaribu mambo na kugundua watu walikuwa hawapo sahihi, soma kitabu hiki, kitakuhamasisha kuchagua kuyaishi maisha yako na kuwa na msimamo sahihi.

24. High Growth Handbook - Elad Gil

Kuna aina mbili za ukuaji wa biashara, ukuaji wa awali, pale kampuni inapotoka wafanyakazi chini ya kumi mpaka kufika wafanyakazi makumi. Halafu kuna ukuaji wa kasi wa baadaye, kutoka wafanyakazi makumi kwenda maelfu.

Mikakati ya ukuaji haifanani katika vipindi hivyo. Vitabu vingi vya biashara vinaelezea ukuaji wa awali, lakini ukuaji wa kasi wa baadaye huwa hauelezewi kwa kina na hapo ndipo wengi hufanya makosa yanayoangusha kabisa biashara.

Kama upo kwenye biashara, hiki ni kitabu muhimu kusoma, pia kama upo kwenye taasisi yenye malengo ya kukua zaidi, soma kitabu hiki, utapata madini ya kuisaidia taasisi kitu kitakachofanya uthaminiwe zaidi.

25. Give and Take; A Revolutionary Approach to Success - Adam M. Grant Ph.D.

Watu wamegawanyika katika makundi matatu, watoaji, wachukuaji na wabadilishanaji.

Watoaji ni wale wanaotoa kwa wengine bila kuangalia wanapata nini. Wachukuaji hawa huangalia wanapata nini bila kujali wengine wanapata nini. Wabadilishanaji ni wale wa nipe nikupe, nikune nikukune.

Katika makundi hayo matatu, wanaopata mafanikio makubwa sana ni watoaji. Unaweza usielewe, lakini mwandishi ameeleza vizuri nguvu ya utoaji kwenye mafanikio. Soma kitabu hiki, kitakusaidia mno katika kujenga msingi utakaokufikisha kwenye mafanikio makubwa hata kama unaanzia chini kabisa.

26. Siddhartha - Hermann Hesse

Riwaya ya kiroho, inayoelezea maisha ya kijana aliyechoshwa na imani ya mazoea kwenye jamii yake na kwenda kutafuta imani mpya na yenye maana. Katika safari hiyo anapotea, anaanguka kwenye maisha ya anasa za dunia, lakini baadaye anapata uamsho na kurudi kwenye njia sahihi.

Maisha yana njia mbalimbali za kututega na kutuangusha, kibaya siyo kuanguka, bali kuanguka na kutokuinuka tena. Maisha ya Siddhartha yanatufundisha mengi, kuanzia kukataa kuishi kwa mazoea, kuwa na kitu chenye thamani ndani yako na kutokusahau kile kilicho ndani yako.

Soma riwaya hii, itakupa nguvu ya kukabiliana na magumu ya maisha.

27. Mindset - Changing The Way You think To Fulfil Your Potential by Carol S. Dweck

Kuna mitazamo miwili ya kiakili, mgando (fixed) na ukuaji (growth).

Wale wanaofanikiwa kwenye maisha ni wenye mtazamo wa ukuaji na siyo mtazamo wa mgando.

Kupitia tafiti mbalimbali, Dweck anatuonesha kwa nini inakuwa hivyo.

Kikubwa sana ambacho utajifunza kwenye kitabu hiki, ni kulea watoto wenye mtazamo wa ukuaji na siyo mgando.

Kuna kauli ambazo ukizitumia kama mzazi zinamjengea mtoto mtazamo mgando na kuwa kikwazo kwake. Mfano mtoto akifaulu ukamwambia ana akili au akifeli na kumwambia hana akili, hapo unamfanya awe na mtazamo mgando, aamini ana akili au hana. Lakini ukimwambia mtoto amepata matokeo aliyopata kutokana na juhudi alizoweka, anakuwa na mtazamo wa ukuaji, ambao utamsukuma aweke juhudi zaidi na afaulu zaidi.

Kama ni mzazi, mwalimu, kocha au kiongozi wa aina yoyote ile, kitabu hiki ni muhimu mno kusoma.

28. Influence - the psychology of persuasion by Cialdini, Robert B

Kitabu namba 19 hapo juu ni cha kukusaidia uwe na ushawishi mkubwa kwa wengine kwenye mahusiano binafsi. Kitabu hiki cha namba 28 kinakusaidia kuwa na ushawishi mkubwa kwa wengine kwenye biashara au uongozi.

Mwandishi ametumia tafiti mbalimbali kuelezea silaha kuu sita za ushawishi, silaha ambazo zina nguvu ya kumshawishi mtu kuchukua hatua fulani.

Matangazo yoyote ya biashara unayokutana nayo kila siku, yanatumia sana misingi ya kitabu hiki.

Kama unataka kuwa na ushawishi kwa watu, hata ambao hawakujui, basi soma kitabu hiki. Kama upo kwenye biashara au kazi yako inahusisha masoko na mauzo, hii inapaswa kuwa biblia yako, zijue silaha sita za ushawishi na jinsi ya kuzitumia kupata matokeo mazuri.

29. Can't Even - How Millennials Became the Burnout Generation by Anne Helen Petersen

Kuna kitu kimoja nimekuwa nakiona kwenye kazi yangu ya utabibu, sehemu kubwa ya watu wenye miaka kati ya 25 mpaka 45 wanaokuja hospitali hawaumwi chochote, ni uchovu tu.

Mtu atakuja akionekana yuko hoi, kila kiungo cha mwili kinamuuma, vinafanyika vipimo mbalimbali na vyote vinaonesha hakuna tatizo. Watu wengi walio kwenye hilo kundi (ukiondoa wajawazito na wenye magonjwa sugu) huwa wako kwenye afya njema kabisa, ila uchovu ndiyo unawasumbua.

Kwa kuwa siku hizi kazi nyingi tunazofanya ni za kutumia akili kuliko mwili, mtu anakikuta anafanya kazi muda mrefu na hapati muda wa kutosha wa kupumzisha akili, kinachotokea ni akili kuulazimisha mwili upumzike, hilo ndiyo linafanya mtu aone anaumwa wakati hana ugonjwa wowote.

Petersen kupitia kitabu hiki anaonesha kwa nini kizazi cha milenia (watu waliozaliwa kati ya mwaka 1981 mpaka 1996) kimekuwa kizazi cha watu wenye uchovu sana.

Anaonesha jinsi uchovu umeanzia shuleni ambapo tulikazaniwa kusoma sana ili tufaulu, ukaenda kwenye kazi ambapo kwanza hazipatikani na zikipatikana siyo zenye kipato kizuri. Na mbaya zaidi ni hii mitandao ya kijamii ambayo inafanya mtu kuwa bize muda wote.

Sina haja ya kukueleza zaidi kuhusu uchovu unaopitia, unaujua, soma kitabu hiki ili ujue hatua sahihi za kuondokana na uchovu ulionao sasa na kuwa na maisha tulivu.

30. The Four Agreements by Don Miguel Ruiz

Kuna maagano mengi ambayo unayaishi sasa, maagano ambayo yamekuweka kwenye kifungo na kujikuta ukiishi kama uko jehanamu. Maagano hayo yana nguvu kubwa ila huijui, kwa sababu jamii haitaki ujue, inataka uendelee kukaa kwenye maagano hayo ili ikutumie utakavyo.

Miguel kupitia kitabu chake anatushirikisha maagano mapya manne ya kuyaishi kwenye maisha yako, ambayo yatakufanya uwe huru na uishi mbingu ukiwa hapa duniani. Kwa kuyajua na kuyaishi maagano haya, hutakuwa tena kwenye utumwa wa kijamii, badala yake utakuwa huru kuyaishi maisha yako.

Huwezi kujua gereza ulilopo kama hujasoma kitabu hiki, hivyo kisome, maagano ni rahisi kabisa na hayakutaki ubadili chochote kwenye maisha yako isipokuwa fikra zako na namna unavyoyachukulia maisha.

31. The Psychology of Money - Timeless Lessons on Wealth, Greed, and Happiness by Morgan Housel

Inapokuja kwenye pesa, kila mtu anafanya maamuzi ambayo kwake anaona ni sahihi, japo kwa wengine yanaweza kuonekana ni ya ajabu. Haijalishi utawashauri nini watu kuhusu pesa, bado mwisho wa siku watafanya maamuzi ambayo huwezi kuyaelewa.

Hiyo ni kwa sababu maamuzi yetu ya kifedha huwa tunayafanya kwa hisia na siyo mantiki. Hivyo kilicho muhimu sana kwenye fedha ni saikolojia yetu. Tunashindwa kubadilika inapokuja kwenye fedha, kwa sababu hatujui jinsi ya kubadili saikolojia yetu kifedha.

Kwenye kitabu hiki, Morgan Housel anatupa masomo 20 kuhusu saikolojia ya fedha, jinsi tunavyosukumwa kufanya maamuzi ya kifedha na namna ya kufanya maamuzi bora.

Fedha ni eneo muhimu kwenye maisha ya kila mtu, hivyo hiki ni kitabu ambacho kila mtu anapaswa kukisoma ili aweze kufanya maamuzi sahihi kifedha.

Rafiki, hivyo ndiyo vitabu 31 vya kusoma ili mwaka 2021 uwe bora kabisa kwako.
 
Ndimi  KOCHA  MWL.  JAPHET    MASATU
 
WhatsApp + 255 716924136 

 

Saturday, February 27, 2021

HASIRA HASARA , UNAPOKUWA NA HASIRA , JIFUNZE KUTULIA , TUMIA NAFASI VIZURI.

Tumeona namna matokeo ya hasira katika jamii zetu yalivyo makubwa. Tumeona namna watu hupigana, kutengana, kuuana sababu tu walikosa kujidhibiti hasira zao wakaamua kuchukua hatua za hatari ambazo zilihatarisha maisha ya watu wengine au kukatisha kabisa maisha ya watu wengine. Matokeo ya hasira ni mabaya mno na yameleta maumivu makali kwa maisha ya watu

Nakumbuka moja ya tukio maarufu lilitangazwa hata katika magazeti nilowahi kulisikia katika udogo wangu ni tukio la watu walokuwa wanapiga debe kupishana kidogo katika kauli na kuanzisha ugomvi maeneo ya Sokomatola mkoani Mbeya kipindi hicho kabla ya kuwa Jiji. Ugomvi huu ulipelekea mmoja kumchoma mwenzake kisu kifuani. Matokeo ya kuchomwa kwa huyu mtu aliyekuwa ni rasta yalipelekea kuvuja damu nyingi kiasi cha kufika hospitali “Mbeya Rufaa” akiwa katika hali mbaya ilopelekea kukatisha maisha yake. Mgomvi mwenzake hakujua tukio la kudhibiti hasira zake kungaliepusha kifo cha kuzuilika kabisa. Je ni wangapi wanakufa au kujeruhiana sababu ya kukosa udhibiti wa hasira ?

Mtu unapokuwa na hasira ni sawa na mtu aliyepoteza utimamu kwa muda. Akili unayokuwa nayo wakati ukiwa na hasira huwa inakuwa na maamuzi ya haraka bila kufikiri ambayo mtu hujutia baadaye baada ya kufanya kitu. Unapokuwa na hasira uwezo wa kufikiri hushuka na hisia hupanda na kuzalisha kujihami. Kujihami huku kiasili kunaweza mtu kutaka kupigana, kutukana au kujeruhi kabisa. Wengine wakiwa na hasira huvunja hadi vitu, hupiga mtu na wengine kuharibu mali zao. Matokeo ya hasara huleta maharibifu mengi maana anayefanya ni sawa na mtu aliyerukwa akili.

Mtu anaingia na hasira pale ambapo anaruhusu kujenga picha akilini juu ya kile kilichomtokea. Mfano mtu anapotukanwa lile tusi analitafsiri na kuona huenda anadhauriwa na hilo linaanzisha ugomvi na hatimaye kuzalisha matokeo mabaya. Mbona mtu huwa hajisumbui endapo mtu aliyemtusi mtu asiye mtimamu. Mtu asiye na utimamu huachwa kwa sababu mtu hutambua kuwa huenda huyo mtu ana matatizo tu ya akili basi asihangaike kushughulika naye. Vile vile tafsiri unayoitoa unapotukanwa au kukutana na tukio ndio inayoathiri kufanya maamuzi na udhibiti wa hasira ndani ya watu.

Jifunze kutulia unapokutana na hali ukakasirishwa ili uepuke madhara yatakayojitokeza endapo utaanzisha ugomvi au kutukana mtu. Vuta pumzi yako pindi unapokuta hasira imekupanda na jicheleweshe kuchukua hatua yoyote ile dhidi ya tukio au mtu aliyechochea upandwe na hasira. Hali ya mihemko ya hasira hupita kama vile upitavyo upepo. Ukingoja basi baada ya muda hasira inakuwa imeisha na unarudi hali ya kawaida ya kufikiri na kuamua mambo. Jifunze kutulia na si lazima kila unalokasirishwa useme au uchukue hatua fulani. Hili litakuepusha na mengi katika maisha.

Kwa wale ambao wanapenda zaidi kujifunza falsafa na kuishi hatua hadi hatua za kifalsafa. Nimeshirikisha hapa hiki kiungo pia cha mwandishi mstoa Ryan Holiday akigusia misemo mifupi mifupi ya Kistoa kwa ajili ya kuishi maisha bora na imara. Ipitie na kuisoma kwa kina utapata mengi zaidi ya kujifunza 


KOCHA MWL.  JAPHET    MASATU

WhatsApp  +255 716924136  / + 255  755  400  128 




 

VYOTE TUNAVYOFIKIRI TUNAMILIKI , HATUVIMILIKI.

Maisha tunayoishi na vyote tunavyopata maishani hudumu nasi kwa muda tu na mwisho huwa tunavipoteza, vinaharibika, vinapoteza thamani na wakati mwingine hufa. Hakuna kitu ambacho kitadumu nasi maisha yote. Hili ni suala la uhalisia na huwa tunaliona ni kweli pale ambapo tunapopoteza zaidi watu wetu wa karibu kwa njia ya kifo. Si kifo pekee kinatufundisha hili kuwa hatutaishi na wanaotuzunguka milele ipo siku watakuwa mbali nasi siku moja ikiwa bado haijatokea.

Umiliki wetu wa watu au vitu ndio chanzo kikubwa cha maumivu ambayo hutokea pindi tunapokuwa tumepoteza hivyo vitu. Utaumia zaidi pale utakapopoteza mtu au vitu ulivyokuwa navyo karibu au kuvitegemea au kufikiri ulikuwa unamiliki maisha yote kumbe si kweli huwa vina ukomo wake kwako na huondoka mbali na wewe. Chochote ulichonacho sasa kitapotea au utakikosa kwa baadaye. Kuanzia uhai wako utafika ukomo, mwili wako utazeeka, wanaokuzunguka watakufa, ajira ulonayo utafika utastaafu, ujana wako utaisha na kupotea. Wakati wa kukoma kwa kila kitu husogea taratibu kama ilivyo muda unapovyoondoka kwa kuanza na dakika, saa, masaa, wiki, mwezi, miezi, mwaka, miaka hadi karne.

Jiondoe katika kuamini kuwa ulichonacho utaweza kukimiliki milele maana kadri muda uendavyo ndivyo nafasi ya kuvipoteza inapokaribia. Una mke, mume au watoto au wazazi unaweza kuishi kama umewamiliki ni wa kwako ila hufika ukomo usimiliki chochote toka kwao. Wanaweza kukimbia, wanaweza kufa wakati wowote ule na wasiwe wako tena. Wewe ni mzazi unaweza fikiria kuwa unamiliki mtoto wako ila kadri muda unavyoenda umiliki wako unapungua kwake. Mtoto anaweza kuwa mbali na wewe akaanzisha familia yake, anaweza kuondoka na kuishi ng’ambo asikumbuke nyumbani tena au akapoteza maisha kabisa. Umiliki wa chochote unaweza kutengeneza manung’uniko au maumivu pale ambapo vitakapopotea na hukuwa unajua kuwa vitapotea.

Kama falsafa ya Ustoa inavyotufundisha kuwa imara na kuwa tayari kwa chochote kitakachojitokeza tusishangazwe nacho maana tayari tunajua hakuna kitakachodumu milele, chochote kinaweza kukutwa na mabadiliko na hakuna namna au uwezo wa kuzuia mambo yaliyo nje ya uwezo wetu. Tunajua kuwa kila ambacho tunacho sasa kina nafasi kubwa ya kupotea na hili linatukumbusha kuvipa uzito vitu hivyo vinapokuwepo nasi. Hili linatuamsha namna ya kuthamini muda wa kuwa navyo hivyo vitu ili vinapopotea tusiumizwe na mabadiliko hayo.

Unapofanya chochote jikumbushe kuwa huenda kitu hicho unakifanya mara ya mwisho sasa na hutakipata nafasi ya kukiona au kukitumia tena. Ondoa yale mazoea kuwa vitu vitaendelea kuwepo namna unavyovichukulia kila siku. Mabadiliko hutokea na vile vyote ulivyokuwa unafikiria vitaendelea kuwepo vinaweza kusitishwa, kuharibika, kufungwa, kuanguka au kufa kabisa. Vitu vingi vilikuwepo miaka 100 ilopita ila sasa havipo, vimeanguka, vimesahaulika na vimekufa. Hili pia lina nafasi ya kuleta mabadiliko miaka 100 ijayo kuwa chochote ambacho kipo sasa hakitakuwepo au kitakuwa kimeharibika au kubadilika. Tumia nafasi ulizonazo sasa kwa chochote kile ulichopewa au kukiona kama ni nafasi adhimu mno ya kutochukulia kirahisi ukijua kuna siku hutapata hiyo nafasi.

KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU

WhatsApp + 255 716   924  136 ) /  + 255 755  400   128

 

KAMA HUNA HABARI ZA KUTOSHA KUHUSU WATU EPUKA KUWAZUNGUMZIA.

Kwa asili yetu sisi binadamu huwa tunapenda kuzijua habari za watu wengine. Inaweza kuwa hujioneshi ila kwa namna fulani unavutiwa kusikia maisha ya watu wengine yalivyo. Mtu asipoweza kujidhibiti basi ataangukia katika kufuatilia maisha ya watu. Tena kwa siku hizi ilivyo watu wanaonesha maisha yao kupitia mitandao basi mitandao yenye habari za maisha ya watu “udaku” hupata wafuasi wengi wakijua ni asili ya watu kupenda kujua maisha ya watu wengine.

Wengi tunaangukia katika mtego wa kutamani sana kuzungumzia watu wengine na pengine mazungumzo hayo yanajaa kuwazungumzia ubaya au mambo ambayo hatujaona kwa macho bali tumepokezana tu kusikia sikia kuhusu wao. Tumeishia kuhukumu watu na kuwaona kwa ubaya kumbe tungejua ukweli kuhusu wao baadaye tunakuja kujilaumu kuwa tumesambaza habari zao ambazo si kweli kuhusu wao. Mtego huu unapokosa kuuvuka unawaletea watu wengi matatizo na wanajishushia heshima walowekewa na wengine. Maisha ya watu wengine huenda si jambo unalopaswa kuliweka kipaumbele ikiwa unataka kuimarisha maisha yako ya kila siku.

Kufuatilia watu wengine na kuanza kuchambua maisha yao ni chanzo cha watu wengi kupatwa na wivu, chuki, hasira na kujichelewesha kufanikiwa kwa mambo yao. Si kwa ubaya kujifunza kupitia maisha ya watu wengine ila jambo la kuzungumza mambo usio na uhakika nayo ni kukosa kufikiri na kuhoji kama mwanafalsafa. Vipi ulichosambaza si kweli kumhusu mtu na ukajulikana ni wewe uliyezungumza. Utajisikiaje na watu watakupa tafsiri gani ?, je ni lazima kuzungumzia maisha ya watu unapokuwa huna ufafanuzi wa kutosha?. Ni muhimu sana kujiuliza mara kwa mara pale unapotaka kuzungumza maisha ya watu wengine.

Usinase katika mtego wa kubeba uliyoyasikia na kuwaambia wengine kama ni jambo toshelevu kuhusu habari au taarifa za mtu. Isitoshe sisi ni binadamu na tu watu wa viungo katika mwili mmoja. Kutamani maisha ya watu wengine yasambazwe kwa habari za uongo ni kukosa kukomaa kifalsafa. Mtu aliye na njia ya maisha hafanyi kitu bila kufikiri au kuongozwa na mihemko ya mkumbo. Hujiuliza na kupima ulazima wa jambo kufanya. Muda ambao tunaishi ni mfupi usotosha kupoteza maisha yetu kuwa watumwa wa maisha ya watu wengine kuchambua maisha yao na yale yote wanayoyapitia.

Wavumilie wengine na jiepushe na mazungumzo ya kuwafuatilia watu ukiwa huna ufafanuzi wa kutosha wa maisha yao. Hata ikitokea upo katika mazungumzo jaribu kuwa msikilizaji na kujifunza namna watu wasivyoweza kujidhibiti na kufikiri katika kuyaangalia mambo. Kuwa kimya ni bora kuliko kuongea kitu kisicho na uthibitisho. Usisukumwe kusambaza chochote au tetesi tu bila kushuhudia au kitu hicho kuthibitishwa. Ila ongozwa na fikara za kujiuliza hivi je hiki nachotaka kuzungumza au kusambaza ni lazima ?

KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU

 ( WhatsApp +255 716 924136 ) /  + 255  755 400128


 

USITOE MAJIBU MEPESI KAMA HUJAWAHI KUPITIA HALI WALIZOPITIA WENGINE.

Chochote kile ambacho hujawahi kukipitia unaweza kutoa maoni mepesi au kuwaona wanaofanya kuna sehemu wanakosea usijue kuwa ingekuwa zamu yako kupitia hiyo hali huenda ungeharibu zaidi. Kitu chepesi ambacho huwa tunawaambia watu wanapopitia magumu ni kusema hilo litapita tu usijali. Au mtu kafiwa ni rahisi kusema pole sana na Mungu akuvushe unalopitia na pengine ukasahau kabisa kufikiri ni kwa vipi huyo mtu hali anayopitia. Ila hiyo hali inapokuja kugusa maisha yako unaweza kuona namna huenda ulichokuwa ukikifikiri ni tofauti kabisa.

Unapokuwa nje ya uwanja na kuangalia wachezaji wanavyocheza unaweza kuona namna wanavyokosea na walivyo wazembe katika mchezo huo wa mpira. Huenda ukiingia katika mchezo isitoshe ukafanya kama wao au kukosea kabisa zaidi. Ndivyo maisha yetu ya kila siku tunavyoyafanya kwa kuwa watazamaji na watoa maoni kuhusu maisha ya watu wengine wanapopitia hali mbalimbali katika maisha. Huenda watu wanapopitia mambo tunawachukulia kuwa ni watu wasio imara, wazembe, wavivu na wasiojitambua kwa sababu sio sisi tunaopitia hizo hali na kuchukulia kiwepesi tu kusema.

Wakati naanza safari ya kujifunza kuchambua vitabu mwaka 2017 mwishoni mwishoni nilikuwa naona wanaofanya kazi ya uchambuzi wa kitabu ni kazi nyepesi mpaka nilipokuja kuanza mwenyewe kuchambua na kujua ukweli kuwa si vile nilivyokuwa nafikiria. Si hilo tu bali kuna wale watu ambao nimewahi kukutana nao wanaosubiri mtu achambue kitabu au afanye kazi fulani ya uandishi na yeye abadili jina na kujimilikisha kuwa ni jasho la kazi alofanya. Ila unapokutana naye na kujua kazi imeibiwa na kumsaidia kama kapenda hizo kazi ajifunze hachukui siku nyingi anakimbia katika mafunzo hayo. Sababu ya kukimbia mafunzo hayo ni kuujua ukweli kuwa kazi hiyo sio rahisi kama alivyokuwa akidhani na kuanzia hapo hutambua kuwa kuandika au kuchambua kitabu si kazi ya kubeza wanaofanya hilo.

Tunaishi katika jamii ambayo inarahisisha mambo na kuchukulia vitu rahisi rahisi tu. Watu wengi hawathamini yale wanayofanya wengine kwa sababu hawajui namna hao watu wanavyopitia. Ni rahisi siku hizi kuona watu wanaomba bidhaa za vitabu zilizo katika nakala laini “softcopy” hata kwa kazi za wazawa wakiona ni jambo la waandishi hao kuwajibika kutoa bidhaa hizo kwa kila mtu. Si vibaya kushirikisha maarifa katika jamii ila jamii inayopuuza jasho la mtu ni jamii inayokosa kutambua hali wanazopitia watu wengine. Mfano uandishi wa kitabu ni mgumu sana na walio waandishi wanajua. Utatumia muda kuandika, kusoma sana na pengine kutumia pesa kukamilisha kitabu hicho. Ni maumivu makubwa ambayo mtu anayapitia ila wale wanaotaka kazi hiyo hiyo kwa urahisi hawajali wala kuweka uzito.

Tukianza kujifunza kuwa katika viatu vya watu wanapopitia hali mbalimbali katika maisha hatutakuwa watu wepesi kuongea ongea au kulaumu watu hao. Tunapojua kuwa hata sisi tungekuwa katika hali kama zao huenda tungeumia zaidi kuliko wao au tungeishia njiani kabisa. Tusiwe wepesi kusema mambo au kuyaona mambo kiwepesi wepesi hasa yanapotokea kwa watu wengine. Inapotokea watu wengine wanapitia hizo hali tuvae viatu vyao na kuona namna si mambo rahisi bali tunahitaji tuwatie moyo katika hilo waweze kuvuka.

Unaposikia jambo lolote lile kuhusu watu basi kabla ya kufanya chochote kile au kuiga mkumbo wa maoni ya watu wengine basi jifunze kutulia na kuwaza vipi kama ingekuwa ni wewe umepata hiyo hali ungefanyaje ?. Ukiwa unajiuliza hivi mara kwa mara maishani utajifunza kuwa kimya na kujua hali wanazopitia hao watu zikoje.

KOCHA   MWL.  JAPHET   MASATU ,

 ( WhatsApp +255 716 924136  ) , +  255  755  400128