Sunday, March 15, 2020

UMEHITIMU SHAHADA NA HUJUI CHA KUFANYA !! FANYA YAFUATAYO.

Haya hapa ni mambo matano unayoweza kufanya kama umehitimu na huna kazi.
( 1 ). UZA  NGUVU   ZAKO.
Hapa unachagua kutafuta kazi ambayo inahitaji nguvu zako kuifanya, hapa elimu yako haina nafasi, bali ni nguvu pekee.
Zipo kazi nyingi za kufanya ambazo zinahitaji nguvu za watu, iwe ni kusaidia kwenye shughuli za ujenzi, kilimo, na kazi nyingine, tafuta nafasi ya kutoa nguvu zako na fanya hivyo.
Kama huna kazi yoyote unayoifanya, usijiambie huwezi kufanya kazi ya kutumia nguvu, unachohitaji sasa ni kitu cha kufanya, hivyo tumia nafasi hiyo kuanza kujenga misingi yako.
( 2 ). UZA  TAALUMA  YAKO  KWA  MLAJI  WA  MWISHO.
Elimu imekuandaa kuuza taaluma yako kwa mtu wa kati, ambaye anaiuza kwa mlaji wa mwisho. Yaani kama ni mwalimu basi unategemea uajiriwe na shule kisha utoe taaluma yako kwa wazazi wenye watoto.
Sasa kama hilo linashindikana, wewe nenda moja kwa moja kwa mlaji wa mwisho. Uza taaluma yako moja kwa moja kwa wale wenye uhitaji nayo.
Hivyo kama ni mwalimu, nenda moja kwa moja kwa wazazi wenye watoto wanaosoma, kisha wape huduma ya masomo ya ziada kwa watoto wao kupitia taaluma yako na wao wakulipe.
Kadhalika kama umesomea uhasibu, badala ya kusubiri kuajiriwa na taasisi fulani, nenda moja kwa moja kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati na wape huduma zako za kihasibu, ambazo wanazihitaji sana ila hawajui wanazipata wapi.
Kwa taaluma yoyote uliyosomea, kuna nafasi ya kwenda moja kwa moja kwa mlaji wa mwisho na ukamuuzia taaluma hiyo. Usisubiri mpaka upate ajira rasmi, andaa sasa huduma unazoweza kutoa na nenda kwa walaji kuwashawishi wakupe nafasi ya kuwauzia taaluma yako.
 ( 03 ). UZA   VIPAJI   VYAKO.
Kabla hata hujaingia kwenye mfumo wa elimu na kupata shahada, kuna vitu ulikuwa unapendelea kufanya au kufuatilia. Vitu hivyo uko tayari kuvifanya hata kama hakuna anayekulipa.
Sasa ni wakati mzuri wa kugeuza vitu hivyo kuwa sehemu ya wewe kuingiza kipato. Angalia ni nini unapenda kufanya, kisha jiulize ni watu gani wanaweza kuwa na uhitaji wa kitu hicho, kisha wapatie na wao wakulipe.
Kama unapenda michezo angalia ni jinsi gani unaweza kuwapa wengine thamani kupitia mapenzi yako ya michezo na wao wakakulipa, labda ni kwa kuchambua vizuri michezo au kushauri vizuri maeneo hayo na kadhalika.
Kama unapenda kusoma vitabu angalia ni kwa namna gani wengine wanaweza kukulipa kwa usomaji wako wa vitabu, labda ni kwa kuwachambulia vitabu au kutafuta vitabu vizuri na kuwashawishi wengine wanunue kwa kuwaeleza kile kilichopo ndani.
Haijalishi unapenda vitu gani au una vipaji gani, wapo wengine wengi ambao wanaweza kunufaika na kile unachofanya. Muhimu ni wewe kuwajua na uweze kuwafikia.
( 04 ). UZA  VITU  VYA   WENGINE.
Kuna makampuni mengi ambayo yana bidhaa na huduma nzuri, lakini hayajalifikia soko vizuri. Wewe unaweza kutumia nafasi hiyo kwa kuwa muuzaji kwenye makampuni hayo.
Kuna makampuni ambayo tayari yana mfumo wa kuchukua wauzaji na kuwalipa kwa kamisheni, kama ukipata kampuni ya aina hii unaweza kujiunga nayo, ukawa muuzaji na ukalipwa kwa kamisheni.
Kuna makampuni mengine hayana mfumo huo, lakini unaweza kuyashawishi na yakakupa nafasi ya kuuza bidhaa zao. Kwa mfano umetumia bidhaa fulani na ukaikubali sana, na unawaona wengine wanaihitaji lakini hawajui kama wanaweza kuipata. Unaweza kuishawishi kampuni husika ikupe bidhaa hiyo ukauze kwa wengine, au ukanunua na kwenda kuuza kwa mfumo huo.
Hapa pia unaweza kujiunga na kampuni zinazofanya biashara kwa mfumo wa mtandao (Network Marketing). Huu ni mfumo unaoruhusu mtu yeyote kuweza kuingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo au bila mtaji kabisa.

 ( 05 ). ANGALIA  UNACHOWEZA  KUWASAIDIA  WENGINE.
Hata kama yote uliyojifunza hapo juu yameshindikana, basi angalia ni msaada gani unaoweza kutoa kwa wengine wenye uhitaji na wao wakakulipa. Iko hivi rafiki, fedha ni zao la thamani, kama unataka kupata fedha, zalisha thamani zaidi kwa wengine.
Kama umesoma mpaka kupata shahada, basi akili yako imefunguka, tumia akili hiyo iliyofunguka kuona watu wana uhitaji gani ambao unaweza kuwasaidia.
Wacha nikupe mfano mmoja ambao utakufungua zaidi, halafu baada ya hapo jiongeze mwenyewe. Chukua mfano wewe ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya kijamii, kila siku lazima uingie kwenye mitandao hii kufuatilia yanayoendelea. Lakini hapo ulipo kuna wafanyabiashara wengi wadogo ambao hawajui jinsi ya kutumia mitandao hii kupata wateja wengi zaidi. Wewe unayo nafasi ya kuwasaidia kwenye hilo, unaweza kuwafungulia akaunti kwenye mitandao hii, kuendesha kampeni mbalimbali ambazo zitawapa wateja zaidi na wao wakakulipa kulingana na wateja wa ziada wanaopata. Kuna mengi kama haya unaweza kufanya, fungua akili yako, angalia mahitaji ya watu kisha ona ni jinsi gani unaweza kuwasaidia kuyatimiza.
Anza sasa kufanya mambo haya uliyojifunza hapa, mambo yote haya hayahitaji uwe na akili zaidi au uwe na mtaji ndiyo uanze kufanya, yanahitaji maamuzi kwamba utafanya na uanze kufanya.
Fikiria umekaa nyumbani miaka miwili bila kufanya chochote tangu umehitimu, hebu pata picha kama ungekuwa unafanya kimoja tu kati ya hivi, kwa miaka miwili ungekuwa wapi?
Endelea kusubiri ajira, endelea kutuma maombi, lakini wakati huo usiyasimamishe maisha yako, chagua kile ambacho utakifanya katika haya uliyojifunza hapa, kisha kifanye kila siku, kazana kutoa thamani zaidi kila siku. Na miaka miwili ijayo, hutahitaji hata kuwa na hiyo ajira unayoisubiri sasa, maana utakuwa umepiga hatua kubwa, kama utajitoa kweli sasa.