Kuna fursa mpya imekuja, umeshawishiwa kwamba ni nzuri na ukafanya maamuzi ya kuingia kwenye fursa hiyo. (fuga kware)
Umeamua
kuingia, wakati unaanza kufanya unakutana na ugumu fulani, kabla
hujaanza kutatua ugumu uliokutana nao, unasikia kuna fursa nyingine bora
zaidi ya hiyo ya kwanza. Hii ya sasa ni ya uhakika zaidi inalipa zaidi na haisumbui. (fuga sungura, ndiyo habari ya mjini).
Unaingia
kwenye fursa ya pili nayo unaianza, ukiwa na matumaini makubwa, lakini
pia unakutana na baadhi ya changamoto kwenye fursa hiyo, ambazo awali
hukuambiwa. Wakati
unaanza kufanyia kazi changamoto hizo, unasikia kuna fursa nyingine
kabambe, hiyo siyo ya kukosa, ni nzuri, na haikuhitaji wewe ufanye kazi
kabisa, ni kukaa kwenye mtandao tu kwa dakika chache na kuingiza fedha. Oh,
tena huhitaji kufanya, wewe unaweka tu hela na wataalamu wanakusaidia
kufanya unasubiri kupokea tu faida (fanya forex au cryptocurrency).
Kama mpaka sasa hujaelewa kinachoendelea hapo, una tatizo, na nipo hapa kutatua tatizo hilo.
Iko
hivi rafiki, kila fursa ni nzuri na ina changamoto zake, kila fursa ina
ugumu ambao lazima ukutane nao, uuvuke na ndiyo uweze kufanikiwa.
Sasa
unapokutana na ugumu kwenye fursa moja, usikimbilie kwenye fursa
nyingine, badala yake tatua ugumu huo na kuendelea na fursa hiyo mpaka
ufanikiwe.
Ninachokuambia leo ni hiki; ACHA kukimbizana na kila aina ya fursa mpya inayokuja. Hutafanikiwa
kwa kujaribu kila fikra, bali utafanikiwa kwa kuchagua fursa moja na
kuifanyia kazi kweli mpaka kufanikiwa, na hapo utakutana na magumu na
changamoto nyingi, katika kuyavuka magumu hayo ndiyo utafanikiwa.
Bilionea Richard Branson amewahi kusema fursa ni kama daladala, ukikosa moja jua kuna nyingine inakuja. Hivyo
ACHA kabisa kukimbizana na kila aina ya fursa, chagua kitu kimoja na
kifanye, weka kazi, weka muda na kuwa na subira na ung’ang’anizi mpaka
upate kile unachotaka.
Na
kwa kumalizia, ukiona unakaribishwa kwenye fursa ambayo unaahidiwa
kupata fedha bila ya kufanya kazi yoyote ile, yaani wewe unaweka tu
fedha halafu kwa namna fulani zinazaliana na unavuna faida kubwa na kwa
haraka, basi jua hili; WEWE NDIYO FURSA YENYEWE.
ACHA kukimbizana na kila aina ya fursa, chagua kitu kimoja au vichache utakavyofanya mpaka ufanikiwe.