Kwenye
 maisha, wapo watu wengi sana ambao watakucheka. Labda ni kwa kile 
ulichosema au unachofanya. Wengi wanapochekwa, hukata tamaa na kuona 
hawawezi na hawafai pia. Hivyo huacha kabisa kile ambacho wanafanya na kurudi kwenye maisha ya kawaida, kitu ambacho kinaua ndoto zao.
KWANINI  WATU  WANAKUCHEKA ?
Sababu ya kwanza ni kama unachekesha, kama umeongea au kufanya kitu ambacho kinachekesha, basi watu watacheka. Kama unafanya vituko, watu hawawezi kujizuia, watacheka.
Sababu ya pili ni kama hawakuelewi, kama watu hawaelewi kile ambacho umeongea au unafanya, watakucheka.
 Na hapa ndipo kundi kubwa la watu wanaocheka lipo. Kwa sababu kila 
ambaye alikuja na wazo la kufanya mambo makubwa, alichekwa. Mwanzilishi
 wa simu alichekwa, waliotengeneza ndege kwa mara ya kwanza walichekwa, 
wanasayansi wakubwa kama kina Newton na Einstein walichekwa kwa nadharia
 zao na hata Viongozi wakubwa wa kifalsafa na kiimani kama Yesu, Mohamad
 na wengine walichekwa sana wakati wanaanza na maono yao.
Hivyo
 basi, watu wanapokucheka, chagua ni kwa sababu ipi kati ya hizo mbili, 
kama ni kwa sababu unachekesha basi endelea, maana kuwapa watu kitu cha 
kucheka ni jambo jema pia. Na
 kama ni kwa sababu hawakuelewi, endelea kufanya, itafika hatua na 
watakuelewa, kama wote waliochekwa huko nyuma walivyokuja kueleweka 
baadaye. Kwa vyovyote vile, usiache kufanya unachofanya, na wala usiogope kusema unachotaka kusema kwa sababu watu wanakucheka. Watu kukucheka hakuna uhusiano wowote na wewe kuacha, ni wao wenyewe.
