Saturday, May 4, 2019

WEKA MALENGO YA MUDA MREFU ( MIAKA MITANO , KUMI ........... !! ) YA BIASHARA YAKO.

Ni lengo lipi kubwa unataka kufikia ndani ya miaka MITANO ,  KUMI ?  YA  BIASHARA   YAKO ?

Kabla sijaendelea hapa, hebu tafakari hilo swali na jipe majibu sahihi. Ni lengo lipi kubwa unalofanyia kazi ambalo unataka kulifikia miaka MITANO , KUMI  ijayo? Watu wengi wanaweza kushangaa unapangaje miaka kumi ijayo, wengi kupanga mwaka mmoja tu ni shida.

Huwezi kufanikiwa kwenye biashara kama huna malengo ya muda mrefu. Na hata kinachofanya wafanyabiashara wengi kukimbizana na fursa mpya zinazojitokeza ni kwa sababu hawana malengo yoyote ya muda mrefu, hivyo chochote kinachojitokeza wanaona ni sahihi kwao kukimbizana nacho.

Unapaswa kuwa na lengo kuu la miaka MITANO , KUMI  ijayo ya biashara yako, wapi unataka kufika na kwa kiwango gani. Lengo hili ndiyo litakusukuma kila siku, ndiyo litakuwa mwongozo wako na ndiyo litaathiri kila maamuzi unayofanya.

Kama huna lengo la miaka MITANO , KUMI  ijayo ya biashara yako, hujajitoa kufanikiwa kweli kwenye biashara hiyo. UNATANIA  NDUGU !  BADILIKA !  NA  AMKA !

WEKA KIPAUMBELE KIKUU CHA BIASHARA YAKO .

JIULIZE  Kipi kipaumbele kikuu cha biashara Yangu ?

Hakuna kitu kinachowapoteza wafanyabiashara wengi kama fursa mpya na nzuri zinazojitokeza kila wakati. Iwapo mfanyabiashara atakuwa mtu wa kukimbizana na kila fursa inayojitokeza, hawezi kufanikiwa kabisa kwenye biashara.

Hii ni kwa sababu fursa mpya huwa ni nyingi na haziishi, na ili upate mafanikio kwenye jambo lolote, unahitaji kuweka muda na kazi.

Jukumu lako kama mfanyabiashara ni kuweka kipaumbele kikuu cha biashara yako, yaani ni aina gani ya biashara utafanya na kisha kuachana na kelele nyingine zozote.

Ukishachagua biashara utakayofanya, funga masikio kuhusu biashara nyingine zisizoendana na biashara hiyo. Hata uambiwe kuna biashara mpya na yenye faida kubwa, usidanganyike kuondoka wenye vipaumbele vyako na kwenda kwenye biashara hiyo mpya, utajipoteza mwenyewe.

Ukichagua nini unataka na kuweka nguvu zako zote kwenye kitu hicho, lazima utakifikia. Lakini ukigawa nguvu zako kwenye kila kitu kipya kinachojitokeza, unajizuia mwenyewe kufanikiwa.

Kama biashara uliyoanzisha imekuwa na unaona fursa ya kuingia kwenye biashara nyingine, fanya hivyo kwa mipango na maono yako na siyo kwa kusukumwa na tamaa zako na za wengine.

JENGA MISINGI MIKUU YA BIASHARA YAKO.

JIULIZE   SWALI  HILI  WEWE  MFANYABIAHARA . Ipi ni misingi mikuu ambayo inaendesha biashara yako?
Kama unataka kujenga nyumba basi msingi ni sehemu ya kuweka umakini mkubwa. Kadhalika kwenye biashara, unapaswa kujenga msingi imara kama unataka biashara yako ifanikiwe.
Hatua ya kwanza kwenye maono ya biashara ni kuainisha misingi mikuu ambayo inaendesha biashara hiyo. Hizi ni kanuni na maadili ambayo kila anayekuwa kwenye biashara hiyo anapaswa kufuata, ukianza na wewe mmiliki wa biashara.
Misingi hii ni muhimu kwa sababu inaongoza jinsi maamuzi yanavyofanywa kwenye biashara. Pia inawavutia watu sahihi na kuwaondoa wale wasio sahihi.
Unapaswa kuwa na misingi imara ya maadili ya kuendesha biashara yako, ambapo maamuzi yote yataongozwa kwa misingi hiyo. Pia utaajiri, kutunza na hata kufukuza wafanyakazi kwa kutumia misingi hiyo.

Wednesday, May 1, 2019

FURSA 8 KWA WAAJIRIWA----Maisha Na Mafanikio Blog ( Life & You )

FURAHA HAIPATIKANI KWENYE MATOKEO , BALI IPO KWENYE MCHAKATO.

Kama unaitafuta furaha kwenye maisha, tayari umeshapotea, kwa sababu unatafuta kitu ambacho hakipatikani. Furaha haipo mwisho wa safari, bali ipo kwenye safari yenyewe. Furaha haipatikani mwishoni, bali katika ufanyaji wenyewe.
 
Ndiyo maana nakuambia furaha ndiyo njia yenyewe, hakuna njia ya kukupeleka kwenye furaha.
 
Mtu anajiambia nikipata kazi nitakuwa na furaha, anaipata na haioni furaha, anajiambia nikipanda cheo nitapata furaha, anapanda cheo hapati furaha, anajiambia tena nikiwa bosi nitakuwa na furaha, anakuwa bosi na haioni furaha. Mtu huyu haoni furaha kwa sababu anaangalia sehemu ambayo siyo sahihi. Furaha haipo kwenye matokeo bali ipo kwenye mchakato. Hivyo kama mtu huyo anataka furaha, basi inapaswa kutoka kwenye kazi zake za kila siku, na siyo matokeo ya mwisho ya kazi zake.

JINSI YA KUOKOA MUDA UNAOPOTEZA KILA SIKU NA OKOA MASAA MAWILI YA ZIADA KILA SIKU.

Kila mtu ana masaa 24 kwa siku ila kuna wanaofanikiwa sana na kuna ambao wanaishia kulalamika kwamba hawana muda. Kama una jambo ambalo ni muhimu kwako lazima utapata muda wa kulifanya. Tumia njia hizi hapa chini kuokoa muda unaopoteza kila siku na uanze kuwekeza kwenye maisha yako.

  Hebu fikiria unaambiwa ujisomee kila siku, ufanye mazoezi, ufanye  meditation, utenge muda wa kuweka mipango yako kwa siku, upate muda wa kupitia mipango yako, upate muda wa kupumzika na pia upate muda kwa ajili ya wale unaowapenda na wanaokupenda. Kwa mambo hayo tu tayari siku imeisha na bado hujaweka muda wa kufanya kazi na muda wa kulala.
 
  Kwa muda mfupi tulio nao ni vigumu sana kufanya mambo yote hayo kila siku. Unaweza kujiaminisha hivyo ila ni uongo mkubwa sana ambao umekuwa unajidanganya kila siku.
  Ili uache visingizio visivyo na maana leo ninakupa njia ya kupata masaa mawili ya ziada kila siku ambapo unaweza kufanya mambo hayo ambayo yatabadili maisha yako na kuwa bora zaidi.

  Kwanza hebu tuangalie muda wetu kwa siku. Kila binadamu ana masaa 24 kwenye siku moja. Wapo wengi ambao wameyagawa masaa yao kwa masaa nane ya kulala, nane ya kazi na nane ya kupumzika. Kwa vyovyote ulivyoyagawa wewe haijalishi, ila unaweza kuokoa masaa mawili ili kufanya mambo yako.

  Ili kupata masaa mawili ya ziada kila siku fanya mambo yafuatayo;
1. Amka nusu saa kabla ya muda uliozoea kuamka kila siku. Utumie muda huo kufanya jambo lenye manufaa kwenye maisha yako kama kujisomea au kuweka MALENGO   NA  MIPANGO. Na ili uweze kuamka nusu saa kabla ni vyema ulale mapema na ulale usingizi mzuri.

2. Punguza nusu ya muda unaotumia kusikiliza redio, kuangalia tv na kuangalia filamu. Asilimia 80 ya vipindi unavyofuatilia kwenye tv au redio havina msaada wowote kwenye malengo yako ya maisha. Asilimia kubwa ya taarifa zinazokushtua kila siku sio za kweli au zimeongezwa chumvi mno. Hivyo punguza muda huu unaotumia kwenye vyombo vya habari na uutumie kubadili maisha yako.

3. Punguza muda unaotumia kwenye mitandao ya kijamii hasa facebook na twitter. Mitandao hii ina ulevi fulani, unaweza kusema unaingia kuchungulia ujue ni nini kinaendelea ila ukajikuta saa nzima unashusha tu kuangalia zaidi. Na asilimia 90 ya unayofuatilia kwenye mitandao hii hayana msaada kwenye maisha yako. Tenga muda maalumu kwa siku wa kutembelea mitandao hii ili kujua nini kinaendelea.

4. Zima simu yako au iweke kwenye hali ya kimya kabisa(wala isitetemeshe). Hapa najua utanipinga sana na unaweza kudhani nimechanganyikiwa. Tumehamishia fikra zetu kwenye mawasiliano hasa ya simu. Mtu unakaa na simu ikiita kidogo tu unakimbilia kujibu bila ya kujali ni kitu gani cha muhimu unafanya. Inaingia meseji ambayo haina hata maana ila inakuhamisha kutoka kwenye jambo la muhimu unalofanya. Najua una madili mengi yanayokuhitaji kupatikana kwenye simu ila kuiweka simu yako mahali ambapo huwezi kuiona kwa masaa mawili kwa siku haiwezi kukupotezea dili lolote. Muda ambao unafanya kazi inayokuhitaji ufikiri sana na uwe na utulivu hakikisha simu yako haiwezi kukuondoa kwenye kazi hiyo. Hivyo izime au iwe kimya kabisa na iwe mbali.