Thursday, December 20, 2018

ISHI KILA SIKU KWA KIASI.

Kila unachofanya kwenye maisha yako, kinapaswa kuwa kwa kiasi, hupaswi kufanya kwa kiwango kidogo sana wala kufanya kwa kupitiliza.

Kuanzia kwenye maisha binafsi na hata kazi au biashara, fanya kwa kiasi. Usile kupitiliza, usinywe kupitiliza, usiwe na hisia kali kupitiliza na wala usipumzike kupitiliza.

Kuishi kwa kiasi ni tabia muhimu sana ambayo itakuwezesha kufika kwenye mafanikio makubwa. Kwa sababu unapofanya kupita kiasi, unauchosha mwili na unashindwa kufanya yale ambayo ni muhimu.

Zoezi la kufanya; kwa yale unayofanya kila siku kwenye maisha yako, fanya kwa kiasi, jidhibiti wewe mwenyewe usifanye jambo lolote kupitiliza. Usile kupitiliza, kunywa kupitiliza au kupatwa na hisia zilizopitiliza. Kufanya hivyo kutakupeleka kwenye matatizo makubwa.

JALI NA BORESHA MAHUSIANO YAKO.

Huwezi kufanikiwa wewe mwenyewe, kauli ya jeshi la mtu mmoja ni kauli ya kujidanganya, hakuna jeshi la mtu mmoja. Mafanikio yako yanahitaji timu kubwa sana ya watu, kuanzia familia yako, watu wako wa karibu, unaohusiana nao kwenye kazi na hata biashara na jamii inayokuzunguka kwa ujumla.
Moja ya tabia muhimu ya kujijengea kila siku ni kutengeneza na kuboresha mahusiano yako na watu wengine. Kila unachokitaka kinatoka kwa watu wengine hivyo mahusiano haya yanapokuwa bora, unaweza kupata zaidi kila unachotaka.
Zoezi la kufanya; yajue mahusiano muhimu kwenye kila eneo la maisha yako, kuanzia familia, marafiki, kazi, biashara na jamii kwa ujumla. Kisha tenga muda wa kuboresha mahusiano haya kupitia mawasiliano na hata kufanya vitu kwa ajili ya wengine.

JALI NA BORESHA AFYA YAKO KILA SIKU.

Yote unayotaka kwenye maisha yako yatabaki kuwa ndoto kama hutakuwa na afya bora. Kwa sababu kama afya siyo bora, hutaweza kuweka mapambano yanayohitajika. Pia kama utaweka juhudi sana kupata mafanikio na ukasahau afya yako, ukayapata mafanikio lakini afya ikawa mbovu hutaweza kufurahia mafanikio hayo.

Tengeneza tabia ya kujali afya yako kila siku. Na maeneo mawili ya kujali na kuboresha afya yako ni kwenye ulaji na mazoezi.

Kwenye ulaji unapaswa kula chakula bora kiafya na kula kwa kiwango ambacho siyo kingi. Epuka vyakula vinavyoandaliwa haraka maana huwa siyo vizuri kiafya.

Pia kuwa na mpango wa mazoezi kila siku. Kila siku fanya mazoezi kwa angalau dakika 30. Mazoezi ya kukimbia ni mazuri kuliko mazoezi ya aina nyingine yoyote.

Zoezi la kufanya; pangilia mlo wako wa kila siku ili kuwa na afya bora. pia tenga nusu saa kwenye kila siku yako kwa ajili ya mazoezi.

JIENDELEZE ZAIDI KILA SIKU.

Ukomo pekee ambao unao kwenye maisha yako ni ule unaojiwekea ndani yako. Mafanikio yako hayawezi kukua zaidi ya unavyokua wewe. Hivyo tabia muhimu sana unayopaswa kujijengea ni ya kujiendeleza zaidi kila siku.

Jiendeleze kila siku kwa kujifunza na kujisomea angalau kwa dakika 30 kila siku. Yaani siku isipite kama hujajifunza kitu kipya. Tenga muda wa dakika 30 wa kujifunza ili uwe bora zaidi.

Soma vitabu, sikiliza vitabu, angalia mafunzo kwa njia ya video na kadhalika, lakini hakikisha kila siku unajifunza. Hakikisha siku inapoanza na kuisha, unakuwa bora zaidi kuliko ulivyoanza siku hiyo.

Zoezi la kufanya; tenga dakika 30 kwenye kila siku yako kwa ajili ya kujifunza na kuwa bora zaidi. Tenga vitabu utakavyosoma, kusikiliza na hata mafunzo utakayoangalia. Usikubali siku ipite hujajifunza kitu kipya.

KUWA NA MALENGO YA KILA SIKU, KILA WIKI, KILA MWEZI, KILA MWAKA NA YA MUDA MREFU.

Bila ya kuwa na malengo unayoyafanyia kazi, juhudi zozote unazoweka unapoteza. Unaweza ukachoka sana, lakini ukiangalia hakuna kikubwa ulichokamilisha.
Unapaswa kuwa na malengo unayoyafanyia kazi kila siku, malengo yako yanapaswa kugawanywa kwenye siku, wiki, mwezi, mwaka na muda mrefu.
Malengo ya siku unayaweka mwanzo wa siku, kwa kuweka orodha ya vile utakavyofanyia kazi siku hiyo.
Kila mwanzo wa wiki weka malengo ambayo unataka kuyakamilisha wiki hiyo. Kadhalika kwenye mwezi na hata mwaka.
Unapaswa kuwa na malengo ya muda mrefu, miaka 5, 10, 20 na mpaka 50 ijayo. Kila wakati unapaswa kuwa unasukumwa na malengo unayoyafanyia kazi.
Zoezi la kufanya; kaa chini na weka au pitia malengo uliyonayo, kisha yaweke kwenye mafungu ya malengo ya muda mrefu, malengo ya mwaka, ya mwezi, ya wiki na kisha ya siku. Anza kila siku yako ukiwa na malengo na mipango unayofanyia kazi na hutapoteza muda kabisa kwenye siku yako.

KUWA MTUMWA WA TABIA NZURI KILA SIKU.

Hatua ya kwanza kabisa kwenye kutengeneza mafanikio ni kujijengea tabia nzuri za kila siku na kuwa mtumwa wa tabia hizo. Na wala huhitaji kuanzia mbali sana kujenga tabia nzuri, bali anza na tabia ulizonazo sasa kisha zigeuze kuwa tabia nzuri.

Kwa mfano kama sasa hizi unatumia muda wako mwingi kuangalia tv au kwenye mitandao ya kijamii, jiwekee ukomo kwenye mambo hayo. Mfano jiambie utatenga saa moja pekee kwenye siku yako kwa ajili ya habari, tv na mitandao ya kijamii. Kwa tabia kama hii utaokoa muda wako mwingi ambao kwa sasa unaupoteza.

Kadhalika badili tabia ulizonazo sasa kwenye ulaji, unywaji, muda wa kuamka, muda wa kulala na mengine yote unayofanya kila siku ya maisha yako.
Zoezi la kuchukua; orodhesha tabia zote unazofanya kwenye kila siku yako, kisha angalia zipi ni nzuri kwako na zipi siyo nzuri kwako. Zile nzuri endelea na nazo na zile mbaya zigeuze kuwa nzuri.

KUWA NA FIKRA ZA KITAJIRI KILA SIKU.

Kuna fikra za kitajiri na fikra za kimasikini. Fikra za kitajiri ni fikra chanya, za hamasa na matumaini makubwa. Fikra za kimasikini ni fikra hasi, za kukata tamaa na kushindwa.
Ili uweze kufanikiwa unapaswa kuwa na fikra za kitajiri kila siku, unapaswa kuwa na kauli chanya ambazo unajiambia kila siku, kauli ambazo zinakupa hamasa na kukusukuma kusonga mbele zaidi. Jijengee taswira ya kile unachotaka kwenye maisha yako na mara kwa mara jione umeshapata kitu hicho. Kwa kufanya hivi unaipa akili yako kazi ya kuhakikisha unapata unachotaka.
Zoezi la kufanya leo; dhibiti fikra zako ziwe chanya na za kitajiri kila siku. Fikiria yale ambayo yanakufikisha kwenye kile unachotaka. Jione tayari umeshafika pale unapotaka na weka picha hiyo kwenye akili yako mara zote. Hili litakufanya uvutie mazingira yatakayokuwezesha kupata unachotaka.