Saturday, June 4, 2016

WATANZANIA WANACHUKUA HATUA KUDHIBITI KISUKARI ?

Takwimu kutoka za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha idadi ya watu wanaoishi na ugonjwa wa kisukari imeongezeka mara nne zaidi na kufikia watu milioni 422 mwaka wa 2014 kutoka watu milioni 108 waliokuwa na ugonjwa huo katika miaka ya 80.
Je, tunachukua tahadhari ya kutosha kujiepusha na athari za ugonjwa wa kisukari?

CHANZO  CHA  HABARI: BBC  SWAHILI,  23,MEI  2016

Saturday, May 14, 2016

UMOJA WA MATAIFA WAMSIFU MACHAR KURUDI NYUMBANI

Riek MacharNEW YORK, MAREKANI

UMOJA wa Mataifa (UN) umesifu hatua ya kiongozi wa waasi nchini Sudan Kusini, Riek Machar kurudi nchini humo kuunda serikali ya mpito, ikiwa ni sehemu ya mpango uliolenga kukomesha vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu kwa miaka miwili.
“Kurejea nyumbani kwa Makamu wa Rais kunapaswa kuwa mwanzo mpya kwa nchi hiyo na kuelekea mpango wa kubadilisha utawala,” Mkuu wa Jopo la Usalama la UN, Herve Ladsous aliliambia Baraza la Usalama la Umoja huo jana.
Baraza hilo lenye nchi 15 wanachama lilikutana kujadili vita nchini humo, huku Machar akiapishwa kurejea katika nafasi yake ya umakamu wa rais katika serikali mpya inayoongozwa na Rais Salva Kiir.
Mafanikio hayo yametokana na juhudi za kimataifa ‘kuwalazimisha’ waasi na serikali kutekeleza kikamilifu makubaliano ya kudumisha amani, ambayo yalitiwa saini Agosti, 2015.
Kwa mujibu wa makubaliano hayo, Machar ataongoza pamoja na Kiir katika serikali ya mpito ambayo itaandaa Uchaguzi Mkuu.
“Ni muhimu pande zinazohusika kutumia nafasi hii kuonyesha walivyojitolea kutekeleza makubaliano ya amani kwa manufaa ya nchi na wananchi wao,” alisema Ladsous.
Balozi Msaidizi wa Sudan Kusini katika UN, Joseph Mourn Malok alisema Serikali mpya inatarajiwa kuundwa baada ya majadiliano ya wadau nchini humo na itachukua siku moja au mbili ili kuyakamilisha.
Machar alirudi nchini humo Jumanne jioni na kuapishwa kuwa makamu wa rais wa taifa hilo jipya zaidi duniani na kutoa wito wa amani baada ya vita vya zaidi ya miaka miwili.
“Tunahitaji kuwaleta watu wetu pamoja ili waungane,” alisema Machar ambaye alilakiwa na mawaziri pamoja na mabalozi aliposhuka katika ndege ya UN.
Awali, kiongozi huyo alitarajiwa kuwasili Aprili 18, lakini akachelewa na kuzua hofu kuhusu hatima ya makubaliano ya amani.
Baada ya kutua katika uwanja wa ndege alienda moja kwa moja hadi Ikulu ambako aliapishwa na hasimu wake, Rais Salva Kiir.
“Nimejitolea kutekeleza makubaliano haya ili hatua ya maridhiano ya kitaifa ianze haraka iwezekanavyo, watu wawe na imani kwa nchi ambayo waliipigania kwa muda mrefu,” alisema.

CHANZO   CHA   HABARI :  GAZETI   LA   MTANZANIA ,IJUMAA, APRIL ,2016

TRUMP AANIKA SERA ZAKE ZA KIGENI


Donald TrumpWASHINGTON, MAREKANI

MGOMBEA urais wa Chama cha Republican nchini Marekani, Donald Trump, ametoa hotuba muhimu kuhusu sera zake za kigeni huku kukiwa na wasiwasi kwamba hana uzoefu wala uelewa wa kutosha kuliongoza taifa hilo lenye nguvu zaidi duniani.
Katika hotuba hiyo, Trump aliahidi kuweka maslahi ya Wamarekani mbele akisema lengo la Marekani litakuwa amani na ufanisi na si vita na maangamizi.
Trump ambaye anapigiwa upatu kushinda tiketi ya chama cha Republican kutokana na kushinda katika majimbo mengi katika chaguzi za mchujo, alitumia muda mwingi katika hotuba yake kuhusu sera zake za kigeni kumponda Rais Barack Obama.
Alisema sera za kigeni za Obama ‘hazikuwa na mbele wala nyuma’ na zimewafanya washirika wa Marekani kupoteza imani na mahasimu kutoiheshimu.
Trump ameahidi kupambana dhidi ya itikadi kali za Kiislamu katika ukanda wa Mashariki ya Kati kwa kuimarisha udhibiti wa kikanda na pia ameahidi kuwa na uhusiano mzuri na Urusi.


CHANZO  CHA  HABARI :  GAZETI  LA  MTANZANIA,IJUMAA, 29  MAY, 2016.

RAIS WA ZAMANI BURUNDI AFARIKI DUNIA


bagaza
BRUSSELS, UBELGIJI

MMOJA wa marais wa zamani wa Burundi, Kanali Jean-Baptiste Bagaza, amefariki dunia mjini hapa jana akiwa na umri wa miaka 69.
Kanali Bagaza amekuwa akitibiwa kwa muda katika Hospitali ya Sainte Elisabeth ya hapa baada ya kuugua kwa muda mrefu.
“Imethibitishwa, Rais wa zamani Jean Baptiste Bagaza amefariki dunia akitibiwa Ubelgiji,” aliandika Mshauri wa Rais wa Burundi, Willy Nyamitwe kwenye Twitter.
Kauli kama hiyo pia iliandikwa katika mtandao huo na Rais Pierre Nkurunziza mwenyewe.
“Salamu za rambirambi kwa familia yake na Warundi wote,” alisema Rais Nkurunziza.
Kanali Bagaza aliyezaliwa Agosti 29, 1946 aliingia madarakani Novemba 1976 kwa njia ya mapinduzi ya kijeshi akianzia uenyekiti wa Baraza Kuu la Mapinduzi Burundi na baadaye rais.
Hata hivyo, naye aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na binamu yake, Meja Pierre Buyoya Septemba 1987.
Alipinduliwa akiwa nje ya nchi yake na hivyo alienda kuishi uhamishoni Uganda na baadaye Libya hadi mwaka 1993 aliporudi nyumbani.
Tangu mwaka 1994 amekiongoza Chama cha Ufufuko wa Taifa (PARENA) na kutokana na hadhi yake kama mkuu wa zamani wa nchi, amefariki dunia akiwa seneta wa maisha.
Anakumbukwa kwa kujenga sehemu kubwa ya miundombinu iliyopo sasa nchini humo wakati wa utawala wake ambao ulikuwa moja ya vipindi ambavyo kulikuwa na udhabiti wa kisiasa katika historia ya taifa hilo baada ya uhuru.

CHANZO  CHA  HABARI :  GAZETI  LA  MTANZNIA , ALHAMISI, MAY,  05 , 2016.

RAIS BUHARI AHAMAKI KUITWA FISADI

Muhammadu_BuhariABUJA, NIGERIA

RAIS wa Nigeria, Muhammadu Buhari, amesema amepigwa butwaa na matamshi ya kushtusha na ya aibu ya Waziri Mkuu wa Uingereza, David Cameron aliyekaririwa akisema Nigeria na Afghanistan ni mataifa fisadi zaidi duniani.
Buhari ameyasema hayo muda mfupi tu baada ya kupata habari hiyo kuhusu kauli zilizotolewa na Cameron.
Akizungumza kupitia msemaji wake, Garba Shehu, ametaja matamshi ya Cameron kuwa ya aibu na kushtua.
“Kiongozi wa Nigeria anasema labda Cameron alikuwa akizungumzia utawala ulioondoka madarakani Mei mwaka uliopita wa aliyekuwa Rais Goodluck Jonathan.
“Buhari alichaguliwa kwa jukwaa la kupambana na ufisadi. Yeye ndiye kifagio cha ufisadi nchini Nigeria.
“Usisahau kuwa Rais Buhari alialikwa katika kongamano la London linalofanyika Alhamisi (leo) kutokana na jitihada zake kubwa za kupigana na ufisadi, itakuwaje awe fisadi,” alisema Shehu.
Habari hizo ziliibuka baada ya Cameron kunaswa na kamera katika dhifa ya kusherehekea miaka 90 tangu kuzaliwa kwa Malkia Elizabeth.
Alisikika akimwambia Malkia, “Viongozi wa mataifa fisadi zaidi duniani wakiwemo wa Afghanistan na Nigeria, yanayoorodheshwa kuongoza kwa ufisadi zaidi kote duniani, watakuwa nchini Uingereza siku ya Alhamisi (leo) kuhudhuria kongamano la kutathmini mbinu za kukabiliana na zimwi la ufisadi.”
Kiongozi wa Kanisa la Anglikana, Askofu Mkuu wa Canterbury, Justin Welby aliyekuwa na viongozi hao wawili anaonekana akimkumbusha Cameron kuwa Buhari aliyeingia madarakani mwaka jana si fisadi.
Hata hivyo Cameron alionekana akiendeleza mada hiyo.
Nigeria pamoja na Tanzania ni nchi pekee kutoka Afrika kati ya nchi 60 duniani zilizoalikwa kuhudhuria mkutano huo wa London.

CHANZO   CHA   HABARI :  GAZETI   LA  MTANZANIA, ALHAMISI, MAY, 12, 2016.

TSVANGIRAI : FEDHA MPYA SI SULUHU KIUCHUMI

Morgan-Tsvangirai1HARARE, ZIMBABWE

KIONGOZI wa chama cha upinzani nchini Zimbabwe, Movement for Democratic Change (MDC) kinachoongozwa na Morgan Tsvangirai, amesema kuanzishwa kwa fedha ya dhamana si suluhisho la tatizo la uchumi.
Katika taarifa iliyotolewa na msemaji wake, Luke Tamborinyoka, alisema tatizo la uchumi ni matokeo ya hali ya sintofahamu iliyoanzia wakati wa uchaguzi uliovurugwa mwaka 2013.
“Bahati mbaya, kitendo cha chama tawala cha Zanu PF kuchapisha noti mpya hakiwezi kuwa dawa kwa tatizo la kisiasa linalohitaji suluhu ya kisiasa.
“Hizo noti za dhamana ni ushahidi wa ukatili wa Serikali inayong’ang’ania kuongoza nchi,” alisema Tamborinyoka.
Wiki iliyopita, Gavana wa Benki Kuu ya Zimbabwe (RBZ), John Mangudya, alitangaza kuwa Zimbabwe itaanzisha noti mpya za fedha ya dhamana ili kuziba pengo la fedha linaloikabili.
Fedha hizo zitadhaminiwa kwa dola milioni 200 na Benki ya Afrexibank iliyopo Misri.
Lakini pia Tsvangirai alisema Serikali imetumia mlango wa nyuma kuirudisha dola ya Zimbabwe na kwamba itairudisha nchi katika zama za mfumuko mkubwa wa bei ulioshuhudiwa miaka minane iliyopita.
Alisema chama chake kitakutana haraka kuzungumzia suala hilo na kinapanga kuanzisha maandamano makubwa kupinga mpango huo.
Hatua hiyo ambayo RZB imekiri kuwa fedha hizo hazitaweza kununua chochote nje ya nchi, imewatia hofu wananchi ambao wameanza kuondoa fedha zao benki.

CHANZO   CHA  HABARI :  GAZETI   LA  MTANZANIA, ALHAMISI, 12, MAY, 2016.


MABASI YA MWENDO KASI TISHIO BIASHARA YA DALADALA



Mabasi ya mwendo kasiAsifiwe George na Ruth Mnkeni, Dar es Salaam

KUANZA rasmi kwa mabasi ya mwendo wa haraka Dar es Salaam huenda kukawa  tishio la biashara kwa wenye wamiliki wa daladala, imeelezwa.
Hali hiyo ilijitokeza jana baada ya abiria wanaotumia barabara ya Morogoro kutokea Kimara hadi Kivukoni kujitokeza kwa wingi kutumia mabasi hayo yalipoingia barabarani kwa mara ya kwanza huku yakitoa huduma ya bure ambayo itaendelea leo.
Baadhi ya madereva wa daladala wanaofanya safari kati ya Kimara na Posta na Mbezi hadi Kivukoni, walisema magari hayo huenda yakawakosesha hesabu za kupeleka kwa mabosi wao kwa kuwa abiria wengi huyakimbilia.
Mmoja wa madereva wa daladala, Juma Abdalla alisema kitendo cha mabasi hayo kutoa huduma bure kuanzia saa 4.00 asubuhi jana kitawasababishia hasara kubwa kwa sababu hawatarajii kufikisha kiwango cha fedha walichotakiwa kupeleka kwa mabosi wao.
“Leo (jana) tutapata hasara kubwa kwa sababu hatutafikisha kiwango cha fedha tunachotakiwa kukipeleka kwa mabosi wetu ukizingatia kwamba huduma hiyo inatolewa bure leo (jana) na kesho (leo),” alisema Abdalla.
Pamoja na malalamiko hayo,  wananchi  walieleza kuridhishwa na viwango vya nauli viliyopangwa na Mamlaka ya Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA), huku wakisema wataokoa muda   kwa kuwa watafika mapema katika shughuli zao za uchumi.
“Pia ingekuwa vema magari haya yaanze kufanya kazi saa 11:00 asubuhi hasi saa 6:00 usiku ili kuondokana na usumbufu wa usafiri,” alisema.
Neema Salimu mkazi wa Kinondoni, alisema magari hayo yamekuwa mkombozi mkubwa kwake kwa sababu anafanya kazi Mbezi Mwisho na alikuwa akilazimika kutumia magari mawili hadi matatu kufika kazini.
Hata hivyo mbali na pongezi hizo, wananchi hao wamelalamikia tiketi za kuingilia kwenye vituo kwamba zinachukua dakika 10 kwa mtu mmoja kuruhusu kuingia kituoni jambo ambalo linapoteza muda mrefu.
Dereva Dotto Edward aliyekuwa akiendesha  basi namba T 144 BGV alisema gari hilo limeboreshwa miundombinu kwa sababu lina viti maalumu kwa ajili ya walemavu wa aina zote pamoja na wajawazito.
Alisema mtu yeyote anaweza kukaa katika viti hivyo, lakini anapopakia mlemavu au mjamzito anapaswa kumpisha.
VITUKO
Baadhi ya wanafunzi wa darasa la pili waliangua kilio baada ya basi walilokuwa wamepanda kupita kwenye kituo chao bila kusimama. Hiyo lilitokana na wanafunzi hao kutoelewa namna ya kutumia mashine zilizo ndani ya basi hilo ambazo humuarifu dereva kusimamisha gari.
MENEJA UDAT
Meneja Uhusiano wa UDART, Deus Bugaywa alisema changamoto kubwa waliyokumbana nayo kipindi hiki cha kuanza kwa mradi ni watu, pikipiki, bajaji na maguta  kuendelea kupita katika barabara za mabasi hayo.

CHANZO   CHA  HABARI :   GAZETI   LA   MTANZANIA, JUMATANO ,11, MAY, 2016.