MAHAKAMA ya Hakimu
Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, jana imetoa hati ya kukamatwa Meya wa
Manispaa ya Kinondoni, Boniface Jacob akidaiwa kutofika mahakamani.
Meya Jacob anakabiliwa
na shtaka la kumshambulia mwandishi wa Habari wa Gazeti la Uhuru,
Christopher Lissa na kumsababishia maumivu makali.
Kesi hiyo ililetwa
mbele ya Hakimu Mkazi, Hellen Riwa kwa ajili ya kusikilizwa ambapo
upande wa mashtaka ulikuwa na shahidi mmoja.
Wakili wa Serikali
Onolina Mushi, alidai mshtakiwa pamoja na wakili wake hawajafika
mahakamani hivyo aliiomba mahakama itoe hati ya kukamatwa mshtakiwa na
kupanga tarehe nyingine ya kuendelea kusikiliza shauri hilo.
Hakimu Riwa alikubali
maombi hayo likiwemo la kutoa hati ya kukamatwa Meya huyo. Kesi hiyo
iliahirishwa hadi Mei 23, mwaka huu, kwa ajili ya usikilizwaji.
Katika kesi hiyo, Jacob
anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 11,2015 katika maeneo ya Kinondoni,
kipindi hicho akiwa Diwani wa Kata ya Ubungo. Ilidaiwa mshtakiwa huyo
alimpiga Lissa mateke na ngumi sehemu mbalimbali za mwili wake na
kumsababishia maumivu makali.
Shtaka la pili ilidaiwa
mshtakiwa siku hiyo hiyo kwa makusudi na kinyume cha sheria, aliharibu
kamera aina ya Nicon yenye thamani ya sh. milioni 8 mali ya Kampuni ya
Uhuru Publication Limited.
CHANZO CHA HABARI: GAZETI LA MAJIRA, Jumanne, mei , 2016.