Wednesday, May 4, 2016

AJALI YA BUTIAMA, TUMEJIFUNZA NINI ?



 









































WATANZANIA wamepokea kwa huzuni kubwa habari kuhusu ajali iliyoua wenzao 36 kule Butiama, Mara, na wengine wapatao 76 wakijeruhiwa, wengine vibaya sana.
Ni huzuni ya Taifa. Nachukua fursa hii kuwapa pole wafiwa na kuwatakia waliojeruhiwa kila la heri wapone haraka.
Hata hivyo, ajali ya Butiama ni kengele nyingine ya hatari tunayopigiwa. Zipigwe kengele ngapi za hatari ili tuamke na kuanza kuchukua hatua madhubuti?
Hatupaswi kuishia kwenye kuomboleza tu na kumwachia Mungu. Tuna wajibu wa kuchukua hatua.
Tunajua, kuwa nyingi ya ajali za barabarani zinatokana na uzembe wa madereva ikiwamo ulevi; kwamba madereva wanaendesha wakiwa wamelewa. Kuna wanaokunywa viroba, wenye kuvuta bangi na hata kumung'unya kubeli. Ni hawa tuliowaachia dhamana ya kuendesha malori na mabasi yenye abiria 65 na zaidi.
Na tuwe na maswali ya msingi ya kujiuliza; Hivi madereva wetu wa malori na mabasi wanapatikana vipi? Kwamba mafunzo yao wanayapata wapi? Kwanini hatuna idara ya Serikali yenye kuthibitisha leseni zao ikiwamo mafunzo waliyoyapata?
Hakika kuna maswali mengi yenye kuhitaji majibu kutoka kwetu wenyewe. Kwamba tunahitaji kongamano la kitaifa kujadili ajali za barabarani na njia ya kuzipunguza. Maana, kubaki kuomboleza na kutochukua hatua madhubuti kupambana na hali hii kunatuacha kila mmoja wetu kuwa kwenye hatari ya kuathirika na ajali za barabarani kwa njia moja au nyingine. Na tuchukue hatua, SASA.
Nimepata kuandika haya huko nyuma, lakini nayarudia hapa kutokana na umuhimu wake kwa kuzingatia kilichotokea Butiama.
Ajali,  na hususan, ajali za barabarani imekuwa ni janga kwa nchi yetu. Kwa mujibu wa ripoti iliyotoka miaka michache iliyopita, Mtafiti wa usalama barabarani (public transport and safety) katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam T. Rwebangira , asilimia 76 ya ajali nyingi zinazohusisha mabasi ya abiria zinatokana na mambo ya kibinadamu, asilimia 17 zinatokana na magari yenyewe na asilimia 7 ni sababu nyingine zisizoweza kuzuilika.
Hizo asilimia 17 zinabainisha kuwa vyombo vingi vya usafiri ikiwamo mabasi mengi tunayotumia hapa Tanzania ni mabovu na usalama wake si thabiti kwa lengo la kusafirisha abiria.
Tuangalie basi hizi asilimia 76 ya sababu za kibinadamu zinazosababisha ajali nyingi hapa Tanzania.
Mtafiti  Rwebangira alibaini kwamba kila mwaka Tanzania inapoteza zaidi ya shilingi bilioni 20 kutokana na ajali mbalimbali za barabarani.
Vyanzo na tafiti mbalimbali vinaainisha kwamba asilimia zaidi ya 78 ya waathirika wa ajali za barabarani ni abiria na watembea kwa miguu.
Kiundani takwimu za kuanzia miaka ya 2000 zinaonyesha asilimia zaidi ya 40 ya wanaokufa kwenye ajali za barabarani ni abiria na zaidi ya asilimia 38 ni watembea kwa miguu.
Takwimu hizo hizo kutoka vyanzo mbalimbali zinaonyesha viini vya ajali za barabarani ambavyo ni uendeshaji wa hatari/uzembe zaidi ya asilimia 54, ubovu wa magari zaidi ya asilimia 16, uzembe wa watembea kwa miguu zaidi ya asilimia 6.8, mwendo kasi zaidi ya asilimia 3, uzembe wa wapanda pikipiki zaidi ya asilimia 3, uzembe wa wapanda baisikeli, zaidi ya asilimia 6, ulevi, zaidi ya asilimia 1.2 na mengineyo kama vile utelezi na ukungu husababisha zaidi ya asilimia 6 za ajali barabarani.
Hivyo basi, zaidi ya asilimia 94 ya ajali za barabrani zinaweza kuzuilika na jamii yenyewe.
Tukiangalia sababu za ajali nyingi za barabarani utakuta nyingi zinahusiana sana na uzembe na kutokuwa makini.
Sababu kubwa ya kwanza ni ulevi wa aina zote wa madereva na abiria.
Wakati fulani nikiwa nasafiri, moja ya sifa alizokuwa anapewa dereva wa basi nililopanda na lililokuwa likienda kwa kasi ni kuendesha akiwa na mzinga wa konyagi nyuma ya kiti chake. Akifika mwisho wa safari chupa hiyo ya konyagi huwa haina kilichobaki. Eti hii pia ni sifa! Jamii nzima inapaswa kupiga vita tabia za kilevi za madereva wetu.
Sababu nyingine ni mwendo kasi unaoendana na kutojali sheria na alama za barabarani. Tunajua, kwamba madereva wetu wengine wanaendesha wamelewa. Tunawaacha wakimbize basi wanavyotaka.
Tujiulize, je, dereva huyu aliyekunywa pombe kabla ya kuanza kuendesha gari anaweza kuwa na maarifa yake ya kawaida na uwezo wake wa kawaida kumudu kasi ya mwendo wa gari? Je, atakuwa makini na kutumia akili yake yote kwenye chombo anachokiendesha?
Siku hizi utakuta dereva anakwenda spidi ya kilomita 150 kwa saa halafu anazungumza kwenye simu. Kuzungumza kwenye simu za mikononi hakufai kabisa kwa dereva wa gari la abiria aendeshapo gari. Hii ni hatari kwa abiria na watu wengine watembeao kwa miguu. Tunalitia hasara kubwa taifa na familia zetu kwa mambo tunayonaweza kuyazuia bila gharama yoyote.
Mabasi mengine utakuta yamepakia abiria na mizigo kupita kiasi. Hatari iliyopo ni basi kushindwa kupita kwenye baadhi ya madaraja na kusababisha ajali mbaya.
Tuangalie sheria Namba 30 ya Mwaka 1973 na marekebisho yake ya mwaka 1996 inayohusu ni jinsi gani magari yanatakiwa yawe yakiwa barabarani.
Tatizo letu si dereva wala abiria kama wanasoma sheria za barabarani.
Suala la ubovu wa magari nao ni sababu mojawapo ya ajali nyingi za barabarani. Kuna rafiki yangu aliyenusurika kufa katika milima ya Kitonga kwa sababu basi alilopanda lenye abiria zaidi ya 65 lilikuwa halina breki. Tujiulize, je, inawezakanaje gari bovu liruhusiwe kuwa barabarani? Kwa kutumia gari bovu hatulidanganyi jeshi la polisi bali tunajidanganya sisi wenyewe.
Kumekuwa na sababu nyingine nyingi kama vile watu wanaondesha magari kwa sababu wana magari lakini si madereva, kuacha nafasi ndogo kati ya gari na gari, uzoefu mdogo wa barabara na zaidi ya yote ni dereva na hasa dereva wa mabasi anapaswa kupumzika vya kutosha.
Tafiti zinaonyesha, kwamba dereva anapaswa kupumzika kila baada ya saa mbili za kuendesha kwa mfululizo. Na tafiti nyingine zinaonyesha dereva anapaswa kuendesha gari kati ya saa tatu hadi nne.
Lakini kwa vyovyote vile, dereva hapaswi kuendesha gari zaidi ya saa nne bila kupumzika. Dereva hapaswi kulazimishwa safari, dereva anapaswa kula chakula kizuri kinachofaa, anapaswa kulala sehemu nzuri na yenye ubora, na apewe maslahi bora.
Haiwezekani hujui dereva amelala wapi ukaruhusu aendeshe gari la abiria. Unajuaje kama alikwenda kulala saa 9 usiku au hakulala kabisa.
Tukumbuke, kwamba ajali hizi zinachukua nguvu kazi kubwa ya nchi yetu. Na mbaya zaidi baadhi ya watu wanachukuliwa na ajali za barabarani ni viongozi bora kabisa.
Kwa pamoja, twapaswa kuchukua hatua katika hili na kupunguza gharama na mzigo kwa Serikali na familia zetu. Mzigo usiokuwa wa lazima kutokana na ajali za barabarani zinazoweza kuzuilika. Nahitimisha.

NA  MAGGID  MJENGWA,  10  SEPT  2014 , GAZETI  LA  RAIA   MWEMA ,