Sunday, May 1, 2016

MAGUFULI APUNGUZA KODI YA MAPATO NA 2%






Huku wafanyikazi kote duniani wakiadhimisha sikukuu ya wafanyakazi, nchini Tanzania, wafanyikazi wanakila sababu ya kutabasamu.
Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli amewaongezea wafanyikazi wote nchini humo asilimia mia mbili 2% mishahara.
Katika hotuba ya kuadhimisha siku ya wafanyikazi, bw Magufuli alitangaza kupunguzwa kwa kodi ya mapato PAYE kutoka asilimia 11% hadi asilimia 9%.

Hii inamaanisha kuwa kila mfanyikazi atapata ongezeko la mapato yake kwa asilimia 2%.
Magufuli alitangaza kauli hiyo kufuatia ombi la wafanyikazi kupitia kwa katibu mkuu bwana Nicholus Mgaya la kutaka wanusuriwe makali ya mfumuko wa bei ya bidhaa muhimu.
Aidha rais Magufuli alisema anatimiza ahadi aliotoa kwa wapiga kura wakati wa kampeini kuwa endapo watamchagua angefanya kila jitihada kuwapunguzia mzigo wa kodi wafanyikazi wa Tanzania.

Kuhusu ongezeko la mshahara wa chini zaidi atakaolipwa mtanzania bwana  Magufuli amewasihi wampe muda kidogo akomeshe rushwa na kuimarisha uchumi wa taifa kisha atatoa tangazo.


''Pamoja na uamuzi huo, Rais Magufuli pia amewaahidi wafanyakazi kuwa baada ya kupunguza kodi katika mishahara ya wafanyakazi, serikali yake itafanyia kazi mapendekezo ya kuongeza mishahara''


''aidha, amewataka wafanyakazi kuunga mkono juhudi za kuwafichua wanaozalisha wafanyakazi hewa, huku akibainisha kuwa mpaka kufikia jana tarehe 30 Aprili, 2016 jumla ya wafanyakazi hewa waliobainika walikuwa 10,293 ambao kwa mwezi mmoja tu wamelipwa shilingi bilioni 11.6.''
Taarifa ya Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, ikulu Dodoma Gerson Msigwa ilisema.

CHANZO  CHA  HABARI : BBC  SWAHIL, Jumapili, 01  mei, 2016.

Saturday, April 30, 2016

ZOMBE ARUDISHWA KORTINI


Abdallah-Zombe1
MANENO SELANYIKA NA SECILIA ALEX,  DAR ES SALAAM
RUFAA ya kesi ya mauaji iliyomkabili aliyekuwa Mkuu wa Upelelezi Mkoa wa Dar es Salaam (RCO), Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP), Abdallah Zombe na wenzake watatu imeanza kusikilizwa jana katika Mahakama ya Rufani huku pande zote mbili zikiwasilisha hoja zake.
Kusikilizwa kwa rufaa hiyo kumetokana na Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kupinga uamuzi uliotolewa Agosti 17, 2009 katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam uliowaacha huru watu wanne akiwemo Zombe na wenzake waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya mauaji.
Kuachiwa huko kulitokana na maelezo kuwa upande wa Jamhuri ulishindwa kupeleka ushahidi mzuri ambao ungeweza kuishawishi mahakama hiyo iwaone washtakiwa hao wana hatia.
Wakibishana kwa hoja katika mahakama hiyo iliyopo Dar es Salaam mbele ya Jaji Benard Luanda wakati upande wa mawakili wa Serikali uliongozwa na Timothy Vitavi, aliyedai kuwa wanapinga kuachiwa huru kwa watuhumiwa hao kwa kuwa ushahidi uliotolewa katika kesi ya msingi ulikuwa hauna shaka.
“Kimsingi washtakiwa wote walikuwa na kosa la mauaji kwa kuwa upande wetu hoja zimewasilishwa zilikuwa hazina tatizo,” alidai Vitavi.
Alidai watazidi kupinga kuachiwa kwao kwa kuwa ushahidi wa awali ulikuwa hauna shaka dhidi ya kosa lililokuwa likiwakabili.
Kwa upande wa utetezi ulioongozwa na Wakili Richard Rweyongeza, ulipinga na kudai kuwa wateja wao hawana makosa na wala hawakushiriki katika tukio hilo la mauaji hivyo waliitaka mahakama hiyo itende haki.
Akiendelea kutoa hoja zake, Rweyongeza ambaye ni Wakili wa Zombe, alidai kuwa katika tukio hilo mteja wake hakufanya kitendo hicho.
“Wanaotuhumiwa walitajwa tu na kesi nyingi huwa watu wanasingiziwa sasa kwa hapa ilipofikia tunaomba mahakama iangalie suala hili kwa kuwa kesi iliisha na sijaelewa kwanini jalada limerudishwa tena,” alidai Rweyongeza.
Baada ya kusikiliza pande zote mbili, mahakama hiyo ilisema ipewe muda ili msajili aweze kupitia hoja hizo kisha atangaze tarehe kwa ajili ya kusoma hukumu.
Hata hivyo, Jaji Luanda, aliagiza kuwa hoja zote ni za msingi hivyo ziwasilishwe kwa Msajili wa Mahakama Kanda ya Dar es Salaam kwa ajili ya kutolea majibu yatakayoelekeza kuendelea kusikilizwa ama la.
Zombe na wenzake walidaiwa kuwa Januari 14, 2006 waliwaua wafanyabiashara watatu wa madini wa Ulanga mkoani Morogoro ambao ni Ephraim Chigumbi, Sabinus Chigumbi na Mathias Lukombe pamoja na dereva teksi Juma Ndugu, mkazi wa Dar es Salaam kwa madai kuwa walikuwa majambazi.

CHANZO   CHA  HABARI :  GAZETI  LA  MTANZANIA, Jumamosi, April  30 , 2016.

Friday, April 29, 2016

JPM AMTUMBUA KIGOGO KWA KUSUSA MSHAHARA



juliet-Kairuki (1)

Na Jonas Mushi, Dar es Salaam

RAIS Dk. John Magufuli, ameendelea na kazi yake ya kutumbua majipu, baada ya kutengua uteuzi wa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC), Julieth Kairuki.
Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari na Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Profesa Adolf Mkenda, Dar es Salaam jana, ilisema Rais Magufuli ametengua uteuzi huo kwa sababu Kairuki amekuwa hapokei mshahara wake tangu alipoajiriwa mwaka 2013, jambo ambalo linazua maswali mengi.
“Pamoja na mambo mengine, hatua hii imechukuliwa baada ya Rais kupata taarifa Kairuki amekuwa hachukuwi mshahara wake tangu alipoajiriwa Aprili, 2013 hadi sasa jambo ambalo linazua maswali mengi,” ilisema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo haikueleza kwa kina sababu za Kairuki kutopokea mshahara wake au kama kulikuwa na mgogoro wa kimkataba au la.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, Kairuki atapangiwa kazi nyingine kama atakuwa tayari kufanya kazi na Serikali.
Kutokana na hali hiyo, Clifford Tandari ameteuliwa kukaimu nafasi iliyoachwa na Kairuki, huku mchakato wa kumpata Mkurugenzi Mtendaji mpya ukiendelea.
Kutokana na suala hilo kuibua maswali mengi, MTANZANIA ilizungumza na Wakili wa kujitegemea, Emmanuel Muga ambaye alisema kutopokea mshahara si kosa na ndiyo maana hajapelekwa mahakamani.
“Kutopokea mshahara si kosa, lakini kwa kanuni za utumishi wa umma mtu hatakiwi kujiweka kwenye nafasi ambayo inaleta picha mbaya, mfano kutopokea mshahara kunaleta maswali mengi, sasa anafanyaje kazi bila kulipwa?” alihoji Muga.
Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Haji Semboja, alisema haiwezekani mtu aache kupokea mshahara pasipo sababu.
“Haiwezekani mtu afukuzwe kwa kutopokea mshahara, sisi pale chuoni zinapita hata awamu tatu hatujapokea stahiki zetu.
“Naona kama Rais ameamua kuunda Serikali mpya, ni bora angetamka anavunja bodi zote ili aunde upya kuepuka watu kufanya kazi katika hali ya taharuki kila siku, huyu katumbuliwa, kesho yule,” alisema.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Profesa Abdallah Safari, alisema haoni sababu ya kufukuza kazi mtu aliyeamua kujitolea kwa kufanya kazi bila kupokea mshahara wake.
“Kama mtu anajiweza na akaamua kufanya kazi bila kupokea mshahara, sioni sababu ya kumfukuza, ningekuwa Rais ningempa tuzo ya ufanyakazi bora,” alisema Safari.
Juhudi za kumpata Kairuki kuzungumzia suala hilo la kutumbuliwa na sababu za kutochukua mshahara wake hazikuweza kufanikiwa hadi tunakwenda mitamboni.

CHANZO   CHA  HABARI:  GAZETI  LA  MTANZANIA, Ijumaa ,  Aprili , 29, 2016.