Friday, September 3, 2021

MITIHANI YA MAISHA HAINA MWISHO , UKISHINDA MTIHANI HUU UNAKUJA ULE.

Bila maandalizi maishani ni kukubali kushindwa au kufeli. Maandalizi hutusaidia kupunguza mawezekano ya kushindwa, kushangazwa au hata kuumia. Wanasema wakati wa vita sio wakati sahihi wa kufanya maandalizi isipokuwa kabla ya vita ndo ulikuwa wakati sahihi wa kujiandaa. Si hilo tu hata maisha ya kila siku bila maandalizi ya mapema ni mtu kujiandaa kushindwa au kuumia zaidi.

Imekuwa ni kawaida yetu sisi binadamu kutoweka uzito katika maandalizi ya mambo mengi maishani na hili linajitokeza kutokea kwa mambo yakitukuta hatukuwa na maandalizi yoyote yale. Inawezekana ni suala la kiuchumi, mahusiano au hata masuala ya kiafya huwa hatujiandai mpaka pale mambo yamejitokeza na kutuzindua kuwa tulipaswa kujiandaa mapema kabisa.

Maisha yamejaa mitihani na majaribu katika kila kona ya kuishi kwetu ikiwa ni kutufungua na kutukumbusha ilivyo haja kubwa ya kuwa na maandalizi mapema ya mambo hayo. Mambo mengi yanayojitokeza na tukayaona ni kama yametokea ghafla kama ajali ni kuwa hatukuwa na maandalizi nayo. Kila mtego ambao mtu anaweza kukutwa amenaswa ni kuwa hakugundua mapema kuwa ilibidi kujua ishara za awali na kujiandaa ili asijekushindwa katika mtihani huo. Wengi tumejikuta tunaanguka katika mambo mengi maishani sababu ya kuondoa nafasi ya maandalizi ambayo ilipaswa kuwepo kila siku.

Maisha hayaachi kutufundisha uhalisia wake kuwa kuna nyakati ngumu na nyepesi, furaha na huzuni, giza na nuru, kushuka na kupanda, kufaulu na kufeli na kuishi na kufa. Safari zote hizi hujitokeza na zinakuja wakati wowote ule ambao mtu anaweza asitegemee ingekuwa hivyo. Bila maandalizi ya kujua hilo ndo kunakozalisha kuyaona maisha yana sura moja tu ya kuwa ni magumu na yasoruhusu watu kuwa na furaha. Yote hujitokeza sababu ya mtu kukosa kujiandaa na kujua ukweli huu wa maisha kuwa wakati wowote ni safari ya maandalizi kwa kuwa mitihani haikosi kuwepo maishani.

Tunapaswa kujiandaa kukutana na kila aina ya watu ambao wanaweza kutufundisha vitu au kutuachia maumivu, wanaweza kutusaidia kukua au kutudumaza kabisa, watu wanaoweza kutuunga mkono au kutukatisha kabisa tamaa, watu ambao watafurahia hatua zetu au kutozifurahia. Aina ya watu hawa tunaweza kukutana nao katika safari ya maisha yetu ya kila siku. Tunapokosa kuwa tayari kujiandaa kwa hilo tunakubali kuumia na kushangazwa na mambo yatakapojitokeza.

Jiandae kwa kila hatua yako hasa pale ambapo upo karibu na watu wanaokuzunguka. Watu wanaotuzunguka wana uwezo mkubwa wa kutufanya tujikute tunaumizwa nao kwa vitu ambavyo wanaweza kuvifanya na tukabaki kushangaa kwa sababu huwa hatujiandai kuwa hata wanaotuzunguka ni watu wenye madhaifu na wanaweza kutuumiza pia. Mitihani ya maisha inaweza kuja kutoka eneo lolote na mtu anapokosa kujua hili tu ni kujiandaa kuumia na kushangazwa na mambo hayo.

Jiandae kwa kuyaweka mambo katika makundi mawili. Kundi la kwanza ni lile lile la kuangalia mambo yaliyo katika uwezo wako ushughulike nayo na kundi la pili ni yale mambo yaso katika uwezo wako uyaache kama yalivyo au kuwa tayari kuishi nayo. Ni falsafa ngumu kuifuatilia ila inampa nguvu mtu katika kujiandaa na kukabiliana na mitihani maishani na majaribu mengi ambayo hujitokeza kutupima na kufungua uhitaji wa kujiandaa zaidi kila siku. 

JIUNGE  DARASA--ONLINE  "  UJIFUNZE   MENGI USIYOYAJUA  TUWASILIANE  SASA  NIKUUNGE KWA   DARASA. "

NA KOCHA   MWL. JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA

WhatsApp + 255 716924136  /    + 255  755 400128

 

Thursday, September 2, 2021

KUWA NA VIPAUMBELE KATIKA MAISHA NA VIFANYIE KAZI



Tunaingia katika taabu maishani sababu ya kukosa msingi wa kujipa msimamo dhidi ya mambo fulani fulani katika maisha. Mtu anaporuhusu kila kitu kiwe sehemu ya maisha yake ni kuruhusu kuyaweka maisha hatarini. Mtu anayekosa msimamo ni rahisi kuyumbishwa na hali zozote zile zitakazojitokeza katika safari ya maisha. Na watu wengi wapo katika hatari hii ya kutoyapa maisha msimamo au msingi fulani unaowaongoza kutoyumbishwa na mambo maishani.

Msimamo hauendi pekee katika maisha bali hata uendeshaji wa kazi unahitaji mtu ajiwekee msimamo fulani ili kutoyumba kwa kazi zake. Mfano kama kazi ya utabibu mtu akikosa msimamo fulani alojiwekea wa kazi ni rahisi kuyakubali mambo mengine ambayo ni nje na maadili ya kazi yake.

Msimamo huu wa maisha ni kuchagua mambo ambayo hutakuwa tayari kuyavunja iwe kwa namna yoyote ile mtu atashawishiwa. Msimamo huu ni katika kuweka ugumu wa kutovunja ahadi ambayo mtu amejiwekea mwenyewe dhidi ya misingi fulani maishani. Hili humsaidia mtu kuwa na maisha yasoyumbishwa.

Ni hatua ngumu ambayo si watu wote wanaweza kuiendea katika maisha. Kuwa maisha yao yataongozwa na misimamo fulani fulani ambayo itawafanya waonekane ni watu wenye misimamo mikali dhidi ya wengine, au watu wasojali hisia za watu wengine. Ila hakuna matokeo mazuri maishani yanaweza kujitokeza isipokuwa kwa mtu kuweka mambo yake katika msimamo asokubali kuvunja kwa namna iwayo yoyote ile.

Weka msimamo katika kazi unayofanya, weka msimamo katika namna unavyohusiana na watu na weka msimamo katika mambo yote unayojua bila kuwa na msimamo thabiti basi mambo mengi yanaweza kuharibika. Hili litakusaidia kuwa na maisha yenye uimara na utulivu wakati wote. Kuna faida kubwa katika kujenga msimamo maishani ili lolote linalokuja kwako linakukuta ukiwa imara na hutayumbishwa na kitu chochote kile. 

 

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES  SALAAM , TANZANIA.

WhatsApp + 255 716 924 136 / + 255 755 400128 / + 255 68 361  539

 

MAGUMU , MATATIZO NI SEHEMU UKUAJI KATIKA SAFARI YA MAISHA , USIJILAUMU NA KULALAMIKA

Kujilaumu ni kitendo cha kujiona mwenye hatia dhidi ya jambo fulani unaloona kwa namna moja umelisababisha litokee na linakuumiza sana ukilitafakari. Hali hii ni mbaya tena iso na usaidizi wowote ule mbali na kuongeza ugumu na taabu ya jambo apitialo mtu. Mtu anaweza kuendelea kuumia juu ya jambo alofanya iwe ni siku za karibuni au miaka mingi imepita. Haisaidii kujilaumu au kulaumu mtu juu ya matukio mbalimbali yanayotokea maishani.

Jamii zetu nyingi tumejengewa hali za kulaumu watu pale mambo yanapoenda tofauti na vile ambavyo tumepanga. Hivyo watu wengi kulaumu wengine inakuwa inaonekana ni kisingizio cha kujiondoa dhidi ya jukumu hilo na kuona wengine walipaswa kuadabishwa kwa hilo. Wakati wote kulaumu au kujilaumu hakujawahi kusaidia kutatua majukumu ya maisha mtu anapoishi. Ni kujisahaulisha tu kuwa tatizo halipo ingali tatizo lipo.

Eneo mojawapo ambalo watu wengi huanza kujilaumu ni pale ambapo vipindi vya hali ngumu maishani vinapobisha hodi, watu hujilaumu huenda wao si watu wenye bahati maishani, wao ni watu wanaonewa, wao hawastahili kupitia hayo na wengine ni kuona ni mikosi tu wao kutokoma kupitia hayo magumu. Magumu ni tafsiri yetu tunayoiweka katika yale yanapotokea maishani. Inaweza kuwa ni matukio yenye kuumiza yamekuja kwa mkupuo kama misiba, hali zisizoleta dalili za afueni iwe ni mahusiano au uchumi, hali za kiugonjwa na kadhalika.

Magumu hutukuza misuli ya akili, hutukuza kuwaza kiutu uzima. Hili ndilo linalowasaidia watu wengi katika umri mdogo kuwa na uwezo mkubwa wa kukabiliana na maisha ambapo kumetokana na wao kupitia magumu na magumu hayo hayakuwadumaza bali yaliwasaidia kukua zaidi. Si rahisi mtu aliyepitia magumu na yakamsaidia kukomaa kushangazwa na hali ngumu za maisha zikitokea maana tayari anajua na uzoefu wa kupitia magumu ya awali. Watu imara hawatengenezeki kwa njia rahisi isipokuwa kwa darasa la kushinda changamoto na kukabiliana na kila gumu njiani.

Mtoto ambaye anaepushwa asipitie magumu au kujua uhalisia wa maisha mapema ni kumwandaa kutokuwa imara siku za baadaye. Atakapokuja kuishi na kukutana na magumu kwa mara ya kwanza lazima itampa wakati mgumu sana kukabiliana na hilo. Huenda wazazi wengi wanaogopa kuwaambia watoto wao juu ya ugumu katika kuyakabili maisha kwa kuona watakuwa wakiwaonea ila si kweli bali wanawapa wakati mgumu baadaye watakapopita katika magumu hayo. Magumu humfanya mtu akutane na ukweli wa maisha kuwa maisha ili ukue kiuzoefu lazima upite magumu mbalimbali yanayomjenga mtu kuwa imara na kuyaendesha maisha.

Uhalisia wa maisha ni kuwa mtu atapitia magumu katika siku za kuishi kwetu. Magumu yapo na yataendelea kuja kwa namna tofauti tofauti. Si kuyalaumu pale yanapokuwa zamu yake kujitokeza. Magumu hutuimarisha na kutukuza kuyaona mambo

NA  KOCHA  MWL.  JAPHET   MASATU , DAR  ES  SALAAAM , TANZANIA

WhatsApp + 255 716 924136 / + 255 755 400128  /   +  255 688  361 539


 

KUPOTEZA " TUMAINI " NI KITU KIBAYA SANA KATIKA MAISHA

Maisha yanaweza kukupitisha katika nyakati ngumu ambazo mbele yako huoni kama utatoka au kuna nafuu yoyote. Nyakati hizi ndizo zinazofanya wengine wasiamini kama lipo tumaini au njia ya kuvuka. Ni lugha ngumu mtu kukuelewa pale anapopitia magumu na unamwambia kuwa hayo magumu utashinda tu huku akiangalia hakuna dalili zozote za suluhisho. Kibinadamu si hali rahisi kushawishiwa kuwa mambo yatakaa sawa na yatapita. Hili ndilo ambalo watu wengine huamua kukatisha maisha yao kwa kuona hawaoni msaada unaoweza kuwatoa walipo.

Hali ya kukosa tumaini inaweza kumkuta mtu yeyote yule katika zama tuishizo. Mambo yanapobadilika ghafla na matarajio mbalimbali kupotea ni hali inayosababisha mtu ashuke hamasa ya kufanya vitu, changamoto zinapokuwa hazikomi, hali ngumu za kiuchumi, migogoro katika kazi au mahusiano, nyakati ngumu za masoko na biashara vinapokuja kwa pamoja kwa mtu mmoja si jambo jepesi la kuvumilika. Ni wengi utakuta wanapata hali ya kukosa hamasa, wanashuka ari ya kufanya kazi na mzigo unapowazidia basi tumaini la nafuu ya hali wapitiazo hufifia au hata kuzima kabisa. Inahitaji ustahimilivu, faraja na nguvu ya kutia moyo na watu wengine kipindi cha hali ngumu.

Mtu anapoanza kupoteza matumaini ni dalili za hatari ambapo asiposaidiwa ni rahisi kufanya maamuzi mabaya ya kimaisha. Hali ya kukosa tumaini huanza pale ambapo mtu huanza kukata tamaa kwa yale anayoyapitia. Huenda ni katika kila jaribio mtu anaona kushindwa na kuanguka. Kukata tamaa kunamsababisha mtu afadhaike na kupata hali ya kupata hatia, kuona hamasa haipo tena na kujawa na hali ya kukata tamaa kabisa ya kimaisha. Hali hizi huwatokea watu wengi wanaopitia hali za sonona katika maisha ambapo kutokana na hali mbalimbali walizoshindwa kuzikabili basi wakajikuta wanazidiwa na kupoteza tumaini.

Magumu katika maisha hayakosekani na si kuwa watu hawapitii magumu. Ikiwa kila mmoja atahadithia simulizi ya yale aloyapitia utakuja kuona unayoyapitia huenda ni madogo. Kinachotia moyo ni kuwa wapo ambao maisha yao ukiyatazama unaona la kwako unalopitia ni dogo na wakati mwingine maisha yao yanaweza kukutia moyo kuwa hupaswi kumbe kukata tamaa. Kila wasaa unapoona tumaini linafifia jipe wasaa wa kuona watu wengine wenye magumu zaidi wasivyokata tamaa wala mioyo yao kuinama.

Unaweza kupoteza kila kitu maishani na ukarejea tena katika kuyaishi maisha endapo hutapoteza “tumaini”. Watu wengi ambao wamepitia magumu, taabu na shida na wakainuka tena hawakupoteza tumaini. Waliweka tumaini kuwa licha magumu yote ambayo yamejitokeza bado wanaona ipo njia, hali zitabadilika na mbele kuna njia ya kutoka. Maisha huwa mapya pale ambapo kila unapopitia magumu hupotezi tumaini kwa kile unachokifanya, tumaini la kuishi na tumaini la kuona kila kitu kitakuwa sawa kadri muda unavyoenda.

Kuna nyakati ambazo nilipitia ngumu sana, niliona siwezi kuinuka tena, niliona ndo mwisho wa kile nilichokuwa nakitegemea ila ninashukuru kuwa nilibakiwa na hali ya kuwa na tumaini kuwa hali nayoipitia itapita. Hili limekuwa likinisaidia hata sasa kuwa kwa kila hali ambayo itatokea iwe ngumu, yenye misusuko mingi nachotakiwa kukitunza ni kuwa na tumaini kuwa mambo yataenda tu. Tumaini ni ukombozi mkubwa katika maisha tuishiyo duniani.

NA  KOCHA   MWL.  JAPHET  MASATU , DAR  ES    SALAAM

WhatsApp + 255 716924136 /   + 255 755 400128