BADILI FIKRA.FIKIRI TOFAUTI .BADILI MAISHA.JITAMBUE .JIFUNZE ELIMU YA SAIKOLOJIA,TEOLOJIA , FEDHA ,UTAMBUZI(SELF HELP EDUCATION),FALSAFA YA MAISHA,MAISHA NA MAFANIKIO,BIASHARA / UJASIRIAMALI.FURAHIA WASAA WAKO NA MAISHA NA MAFANIKIO BLOGU.THIS IS THE COMMUNITY CAPACITY BUILDING BLOG.ENJOY THE BLOG.STRETCH YOUR MIND. YOU CAN CHANGE YOUR LIFE FOR EVER. YOU CAN ACHIEVE EXCELLENCE.YOU CAN MAKE A DIFFERENCE.
Tuesday, March 31, 2020
Monday, March 30, 2020
Sunday, March 29, 2020
Friday, March 27, 2020
Wednesday, March 25, 2020
MWONGOZO WA KUFANYIA KAZI AU KUJISOMEA KWA WANAFUNZI NYUMBANI !!!
FAIDA ZA KUFANYIA KAZI / KUJISOMEA NYUMBANI.
Kufanyia kazi zako nyumbani, iwe umeajiriwa au umejiajiri au wewe ni mwanafunzi wa shule za msingi , sekondari au chuo kuna faida nyingi sana, baadhi ya faida hizo ni kama ifuatavyo;
- Unaokoa muda mwingi ambao huwa unaupoteza kwa kwenda eneo la kazi, shule au chuo Kuanzia muda unaotumia kwenda, kurudi na mwingine unaopotea, kwa kufanyia kazi nyumbani hupotezi muda wako.
- Unapunguza fursa za kupoteza muda zinazopatikana kwenye eneo la kazi, mfano mikutano mbalimbali ambayo hufanyika maeneo ya kazi, ambayo kwa sehemu kubwa haina tija.
- Unafanya kazi kwa mpango wako bila ya kusumbuliwa na wafanyakazi wengine.Kama mwanafunzi au mwanachuo unaepuka kelele za wanafunzi wenzako . Japo kunakuwa na mawasiliano ya simu au njia nyingine za mtandao, ile hali ya kukatishwa na wengine wakati unafanya kazi au unajisomea inapungua.
- Kwa sehemu kubwa unakuwa na uhuru wa kupanga muda wako mwenyewe, hasa kama kazi yako haihitaji kushirikiana na wengine wakati mnaifanya. Unaweza kupanga kufanya kwa muda unaofaa kwako.
- Unapata muda mwingi wa kupumzika, majukumu yako unayofanya ukiwa kazini, shule , chuo ukiyafanyia nyumbani itakuchukua nusu ya muda unaotumia kuyafanya ukiwa kazini , shule au chuo .Hivyo unapata muda mwingi wa kupumzika au kufanya mambo mengine.
Changamoto za kufanyia kazi nyumbani.
Hakuna kisichokuwa na changamoto, na katika kufanyia kazi nyumbani, zipo changamoto nyingi. Hapa ni baadhi ya changamoto hizo;
- Kushindwa kutekeleza majukumu yako kwa wakati kwa sababu hakuna anayekusimamia moja kwa moja au anayekuangalia. Unahitaji nidhamu kali sana kuweza kujisimamia mwenyewe.
- Usumbufu wa wanafamilia wakati unafanya kazi, wengi hawajui kwamba japo upo nyumbani pia upo kazini, hivyo kuingilia kazi zako pale wanapokuwa na mahitaji mbalimbali.
- Kukosekana kwa mipaka kati ya kazi na maisha. Kwa kuwa unafanyia vyote nyumbani, ni rahisi kushindwa kuweka mipaka, ukajikuta unaruhusu mambo ya kifamilia kuingia kwenye wakati wa kazi au mambo ya kikazi kuingia kwenye wakati wa familia.
- Wageni usiokuwa na miadi nao wanapokuja nyumbani na kujua upo, wanaingilia sana muda wako wa kazi. Wengi hawawezi kuelewa kwamba japokuwa upo nyumbani, upo kazini, hivyo kuhitaji muda wako mwingi.
- Ni rahisi kwa uvivu kukunyemelea, ukipatwa na usingizi kidogo ni rahisi kwenda kulala au kufanya mambo mengine ya kupoteza muda kama kuangalia tv, kuzurura mitandaoni na kadhalika.
MKAKATI BORA KWAKO WA KUFANYIA KAZI NYUMBANI.
Ili
kupata manufaa ya kufanyia kazi nyumbani, pamoja na kuzuia changamoto
zake zisiwe kikwazo kwako, tengeneza mkakati mzuri kwako kufanyia kazi
nyumbani
Zingatia mambo yafuatayo katika kutengeneza mkakati wako wa kufanyia kazi nyumbani utakaokupa matokeo mazuri.
( 01 ). TENGA ENEO LA KUFANYIA KAZI.
Kitu
cha kwanza muhimu kabisa kwako kufanya ni kutenga eneo la kufanyia kazi
ukiwa nyumbani. Huwezi kuwa unafanyia kazi kila mahali na ukawa na
nidhamu nzuri. Badala yake unapaswa kutenga eneo ambalo utakuwa
unafanyia kazi zako, na ukiwa eneo hilo unachofanya ni kazi tu na siyo
kitu kingine.
Hii
inakuandaa kisaikolojia kuheshimu eneo hilo na unapokuwa kwenye eneo
hilo unajua cha kufanya ni kazi. Kama unaishi kwenye nyumba kubwa
unaweza kutenga chumba utakachotumia kama ofisi. Lakini kama huwezi
kufanya hivyo unaweza kutenga eneo kwenye chumba chochote, hata kile
unacholala na kulitumia kama eneo la kazi.
Kama
unatenga eneo ndani ya chumba chenye matumizi mengine, hakikisha
unaweka kiti na meza kwa ajili ya kufanyia kazi. Hivyo unapokaa kwenye
kiti na meza hiyo, unajua kabisa hili ni eneo la kazi. Usifanye kitu
kingine unapokuwa kwenye kiti na meza ulivyoandaa kwa ajili ya kazi.
Epuka
kufanyia kazi kitandani au kwenye kochi, kwenye maeneo hayo hutaipa
kazi uzito kwa sababu kisaikolojia unayachukulia kama maeneo ya
kupumzika
( 02 ). TENGENEZA RATIBA YAKO YA KILA SIKU NA IFUATE.
Japokuwa
una uhuru wa muda gani ufanye kazi unapokuwa nyumbani, uhuru huo una
mipaka. Huwezi kufanya kazi zako pale unapojisikia, ukienda kwa mpango
huo hutafanya chochote. Ndiyo una uhuru, lakini lazima utengeneze ratiba
yako mwenyewe na uifuate kila siku.
Panga
kabisa ni muda gani unaamka, ukiamka unafanya nini, muda gani
unapumzika, unakula na unakuwa na familia. Yote hayo lazima uyapange na
kisha kuyafuata.
Ukianza siku zako bila mpango, utajikuta umefanya mengi, umechoka lakini hakuna kikubwa ulichokamilisha.
Kwenye ratiba yako ya siku tenga kabisa masaa ambayo huhitaji usumbufu, hayo ni masaa ya kazi zinazohitaji umakini mkubwa.
( 03 ). VAA KAMA UNAENDA KAZINI / SHULENI / CHUONI
Unapofanyia
kazi nyumbani, una uhuru wa kuvaa utakavyo au hata kutokuvaa kabisa.
Lakini hilo unapaswa kuwa nalo makini, kwa sababu lina madhara ya
kisaikolojia kwenye utekelezaji wa majukumu yako ya kazi. Kama umevaa
nguo za kawaida utajiona kama hauna majukumu makubwa.
Hivyo
unapaswa kujiandaa vizuri kama vile unaenda kazini shuleni, chuoni kwa kuvaa kabisa
nguo zako za kazi na kisha kukaa eneo lako la kazi wakati unafanya kazi.
Unapovaa nguo kama vile unaenda kazini, akili yako inakupa uzito wa
kikazi na unatekeleza majukumu yako vizuri.
( 04 ). WATU WOTE WAJUE RATIBA YAKO.
Ukishaweka
ratiba yako ya siku, kila mtu kwenye familia anapaswa kuijua. Na
waeleze wazi kwamba japokuwa upo nyumbani, lakini pia upo kazini au unajisomea. Kwa
muda ule wa kazi, mambo yote hapo nyumbani yanapaswa kuendelea kama vile
wewe haupo kabisa.
Ule
muda ambao umetenga usisumbuliwe, usisumbuliwe kweli, labda kwa jambo
la dharura, ambalo hata kama ungekuwa kazini basi ungepigiwa simu. Na
weka kabisa vigezo vya dharura ni vipi. Usipofanya hivi, watu watatumia
uwepo wako kuuliza vitu mbalimbali na hilo kuathiri kazi zako.
Kuhusu
wageni, kama kuna mgeni amekuja na hukuwa na miadi naye, usikutane naye
wakati ambao unafanya kazi. Anapaswa kuelezwa ratiba yako na muda mzuri
kwako kukutana naye. Na kama ni mgeni muhimu, unaweza kumsalimia na
kumpa ratiba yako ilivyo na mkapanga muda gani mzuri wa kuwa na
maongezi, kama yapo na ni muhimu.
( 05 ). TENGENEZA MIPAKA YA KAZI / KUSOMA NA MAISHA.
Kwa
kuwa upo nyumbani na unafanyia kazi nyumbani, mpaka kati ya kazi na
maisha unafutika kabisa. Wakati wa kazi utaingiliwa na mambo ya
kifamilia na wakati wa familia utaingiliwa na mambo ya kikazi.
Ni
lazima utengeneze mpaka kati ya kazi na maisha, ufanye kazi wakati wa
kazi na maisha wakati wa maisha. Jisukume kutekeleza majukumu yako ya
kazi kwa wakati uliopanga kufanya kazi na ule wakati uliopanga kupumzika
au kuwa na familia basi usiruhusu kazi au masomo kuingilia wakati huo.
( 06 ). TUMIA VIFAA VYA KUONDOA USUMBUFU.
Kama
mazingira ya nyumbani kwako siyo rafiki kwako kupata utulivu wa kazi au kusoma,
labda kuna kelele mbalimbali za majirani na watu wengine, basi tumia
vifaa vya kuondoa usumbufu.
Hapa
unapaswa kuwa na spika za masikioni (headphone au earphone) ambazo
utazivaa wakati wa kufanya kazi. Kuna ambazo zina sifa ya kufunga kelele
za nje zisikuingie na hivyo kukupa utulivu mkubwa wa kufanya kazi zako.
Pia
kitendo cha kuvaa spika hizo, kinamfanya mtu asikusemeshe mara kwa
mara, kwa sababu anajua humsikii. Pia mtu anapokusemesha, jifanye kama
humsikii, hata kama unamsikia, hasa pale jambo linapokuwa siyo muhimu.
Inayoendana
na hii ni kuandaa orodha ya nyimbo (playlist) zinazokupa utulivu na
kuitumia wakati unafanya kazi zako. Hapa unasikiliza nyimbo hizo kwa
kujirudia rudia na hilo linafanya akili yako izame kwenye kazi
unayofanya na kuepuka usumbufu.
( 07 ). JALI AFYA YAKO.
Unapofanyia
kazi nyumbani, kama kazi zako ni za kutumia akili na unazipenda sana,
unaweza kujikuta umekaa kwenye kazi siku nzima na hujatoka kabisa nje ya
nyumba yako. Pia ulaji ni rahisi sana unapokuwa nyumbani kuliko ukiwa
kazini, ni rahisi kula mara kwa mara ukiwa nyumbani kuliko ukiwa kazini.
Hivyo
unapaswa kuwa na mkakati wa kujali na kuboresha afya yako. Kitu cha
kwanza muhimu ni kufanya mazoezi, tenga muda wa kufanya mazoezi ambayo
yatakutoa jasho. Cha pili ni kudhibiti ulaji, usile kwa sababu kuna kitu
cha kula, bali kula kwa utaratibu maalumu na kuwa makini na kile
unachokula. Cha tatu ni muda wa kupumzika, unaweza ukakosa mapumziko
mazuri japo uko nyumbani na hilo likaathiri afya yako.
(08 ). PANGILIA MUDA UNAOENDANA NA WEWE NA UNAOEPUKA USUMBUFU.
Kitu
kimoja ambacho kimekuwa kinanisaidia sana mimi binafsi kuweza
kukamilisha sehemu kubwa ya uandishi ni kutenga muda wa uandishi ambao
unaendana na mimi na pia unaepuka usumbufu.
Huwa
ninaamka saa kumi kamili asubuhi kila siku na baada ya kufanya tahajudi
na tafakari kisha kuipangilia siku, kuanzia saa kumi na nusu mpaka saa
12 kamili huo ni muda wa kuandika tu, sifanyi kingine kwenye muda huo.
Kwa muda huo, nimekuwa na uwezo wa kuandika kwa kiwango kikubwa sana,
kwa sababu akili inakuwa na utulivu na hakuna usumbufu, maana watu
wengine wanakuwa wamelala kwenye muda huo.
Hivyo
na wewe pangilia majukumu yanayohitaji utulivu na umakini kulingana na
wewe binafsi na mazingira. Yaani yapange kwenye muda ambao akili yako
iko vizuri lakini pia hakuna usumbufu wa nje.
Watu
tumegawanyika kwenye makundi mawili; kuna ambao wanaweza kuamka asubuhi
na mapema na akili zao zikawa vizuri (early birds) na kuna ambao
wanachelewa kulala na muda wa usiku ndiyo akili zao zinakuwa vizuri
(night owls). Jijue wewe uko kundi gani, kisha tenga muda ambao wengine
wamelala na ufanye kuwa wa kazi.
Mfano
kama uko vizuri kwenye kuamka asubuhi basi amka asubuhi na mapema sana,
labda saa tisa au saa kumi na kisha tumia masaa mawili ya kwanza kwenye
kazi inayohitaji umakini wako na utulivu. Muda huo wengi wanakuwa
wamelala na hivyo usumbufu unakuwa mdogo.
Na kama unachoelewa kulala basi tenga masaa mawili ya usiku mnene ambapo wengine wamelala na akili yako imetulia kufanya kazi.
Ukiweza
kutenga masaa mawili ambapo akili yako imetulia na ina umakini na
hakuna usumbufu wa nje, kisha kuyaweka masaa hayo mawili kwenye kazi,
utatekeleza majukumu makubwa kuliko anayefanya kazi siku nzima kwenye
ofisi isiyo na utulivu.
Rafiki
yangu mpendwa, mdau wangu huu ndiyo mwongozo sahihi kwako wa kufanyia kazi
nyumbani .( kama wewe ni MWAJIRIWA , UMEJIAJIRI , MWANAFUNZI , MWANACHUO ni mwongozo mzuri sana kuufuata.
Monday, March 23, 2020
Sunday, March 22, 2020
Thursday, March 19, 2020
Wednesday, March 18, 2020
Monday, March 16, 2020
Sunday, March 15, 2020
UMEHITIMU SHAHADA NA HUJUI CHA KUFANYA !! FANYA YAFUATAYO.
Haya hapa ni mambo matano unayoweza kufanya kama umehitimu na huna kazi.
( 1 ). UZA NGUVU ZAKO.
Hapa unachagua kutafuta kazi ambayo inahitaji nguvu zako kuifanya, hapa elimu yako haina nafasi, bali ni nguvu pekee.
Zipo
kazi nyingi za kufanya ambazo zinahitaji nguvu za watu, iwe ni kusaidia
kwenye shughuli za ujenzi, kilimo, na kazi nyingine, tafuta nafasi ya
kutoa nguvu zako na fanya hivyo.
Kama
huna kazi yoyote unayoifanya, usijiambie huwezi kufanya kazi ya kutumia
nguvu, unachohitaji sasa ni kitu cha kufanya, hivyo tumia nafasi hiyo
kuanza kujenga misingi yako.
( 2 ). UZA TAALUMA YAKO KWA MLAJI WA MWISHO.
Elimu
imekuandaa kuuza taaluma yako kwa mtu wa kati, ambaye anaiuza kwa mlaji
wa mwisho. Yaani kama ni mwalimu basi unategemea uajiriwe na shule
kisha utoe taaluma yako kwa wazazi wenye watoto.
Sasa
kama hilo linashindikana, wewe nenda moja kwa moja kwa mlaji wa mwisho.
Uza taaluma yako moja kwa moja kwa wale wenye uhitaji nayo.
Hivyo
kama ni mwalimu, nenda moja kwa moja kwa wazazi wenye watoto wanaosoma,
kisha wape huduma ya masomo ya ziada kwa watoto wao kupitia taaluma
yako na wao wakulipe.
Kadhalika
kama umesomea uhasibu, badala ya kusubiri kuajiriwa na taasisi fulani,
nenda moja kwa moja kwa wafanyabiashara wadogo na wa kati na wape huduma
zako za kihasibu, ambazo wanazihitaji sana ila hawajui wanazipata wapi.
Kwa
taaluma yoyote uliyosomea, kuna nafasi ya kwenda moja kwa moja kwa
mlaji wa mwisho na ukamuuzia taaluma hiyo. Usisubiri mpaka upate ajira
rasmi, andaa sasa huduma unazoweza kutoa na nenda kwa walaji
kuwashawishi wakupe nafasi ya kuwauzia taaluma yako.
( 03 ). UZA VIPAJI VYAKO.
Kabla
hata hujaingia kwenye mfumo wa elimu na kupata shahada, kuna vitu
ulikuwa unapendelea kufanya au kufuatilia. Vitu hivyo uko tayari
kuvifanya hata kama hakuna anayekulipa.
Sasa
ni wakati mzuri wa kugeuza vitu hivyo kuwa sehemu ya wewe kuingiza
kipato. Angalia ni nini unapenda kufanya, kisha jiulize ni watu gani
wanaweza kuwa na uhitaji wa kitu hicho, kisha wapatie na wao wakulipe.
Kama
unapenda michezo angalia ni jinsi gani unaweza kuwapa wengine thamani
kupitia mapenzi yako ya michezo na wao wakakulipa, labda ni kwa
kuchambua vizuri michezo au kushauri vizuri maeneo hayo na kadhalika.
Kama
unapenda kusoma vitabu angalia ni kwa namna gani wengine wanaweza
kukulipa kwa usomaji wako wa vitabu, labda ni kwa kuwachambulia vitabu
au kutafuta vitabu vizuri na kuwashawishi wengine wanunue kwa kuwaeleza
kile kilichopo ndani.
Haijalishi
unapenda vitu gani au una vipaji gani, wapo wengine wengi ambao
wanaweza kunufaika na kile unachofanya. Muhimu ni wewe kuwajua na uweze
kuwafikia.
( 04 ). UZA VITU VYA WENGINE.
Kuna
makampuni mengi ambayo yana bidhaa na huduma nzuri, lakini
hayajalifikia soko vizuri. Wewe unaweza kutumia nafasi hiyo kwa kuwa
muuzaji kwenye makampuni hayo.
Kuna
makampuni ambayo tayari yana mfumo wa kuchukua wauzaji na kuwalipa kwa
kamisheni, kama ukipata kampuni ya aina hii unaweza kujiunga nayo, ukawa
muuzaji na ukalipwa kwa kamisheni.
Kuna
makampuni mengine hayana mfumo huo, lakini unaweza kuyashawishi na
yakakupa nafasi ya kuuza bidhaa zao. Kwa mfano umetumia bidhaa fulani na
ukaikubali sana, na unawaona wengine wanaihitaji lakini hawajui kama
wanaweza kuipata. Unaweza kuishawishi kampuni husika ikupe bidhaa hiyo
ukauze kwa wengine, au ukanunua na kwenda kuuza kwa mfumo huo.
Hapa
pia unaweza kujiunga na kampuni zinazofanya biashara kwa mfumo wa
mtandao (Network Marketing). Huu ni mfumo unaoruhusu mtu yeyote kuweza
kuingia kwenye biashara kwa mtaji kidogo au bila mtaji kabisa.
( 05 ). ANGALIA UNACHOWEZA KUWASAIDIA WENGINE.
Hata
kama yote uliyojifunza hapo juu yameshindikana, basi angalia ni msaada
gani unaoweza kutoa kwa wengine wenye uhitaji na wao wakakulipa. Iko
hivi rafiki, fedha ni zao la thamani, kama unataka kupata fedha, zalisha
thamani zaidi kwa wengine.
Kama
umesoma mpaka kupata shahada, basi akili yako imefunguka, tumia akili
hiyo iliyofunguka kuona watu wana uhitaji gani ambao unaweza kuwasaidia.
Wacha
nikupe mfano mmoja ambao utakufungua zaidi, halafu baada ya hapo
jiongeze mwenyewe. Chukua mfano wewe ni mtumiaji mzuri wa mitandao ya
kijamii, kila siku lazima uingie kwenye mitandao hii kufuatilia
yanayoendelea. Lakini hapo ulipo kuna wafanyabiashara wengi wadogo ambao
hawajui jinsi ya kutumia mitandao hii kupata wateja wengi zaidi. Wewe
unayo nafasi ya kuwasaidia kwenye hilo, unaweza kuwafungulia akaunti
kwenye mitandao hii, kuendesha kampeni mbalimbali ambazo zitawapa wateja
zaidi na wao wakakulipa kulingana na wateja wa ziada wanaopata. Kuna
mengi kama haya unaweza kufanya, fungua akili yako, angalia mahitaji ya
watu kisha ona ni jinsi gani unaweza kuwasaidia kuyatimiza.
Anza
sasa kufanya mambo haya uliyojifunza hapa, mambo yote haya hayahitaji
uwe na akili zaidi au uwe na mtaji ndiyo uanze kufanya, yanahitaji
maamuzi kwamba utafanya na uanze kufanya.
Fikiria
umekaa nyumbani miaka miwili bila kufanya chochote tangu umehitimu,
hebu pata picha kama ungekuwa unafanya kimoja tu kati ya hivi, kwa miaka
miwili ungekuwa wapi?
Endelea
kusubiri ajira, endelea kutuma maombi, lakini wakati huo usiyasimamishe
maisha yako, chagua kile ambacho utakifanya katika haya uliyojifunza
hapa, kisha kifanye kila siku, kazana kutoa thamani zaidi kila siku. Na
miaka miwili ijayo, hutahitaji hata kuwa na hiyo ajira unayoisubiri
sasa, maana utakuwa umepiga hatua kubwa, kama utajitoa kweli sasa.
Friday, March 13, 2020
Wednesday, March 11, 2020
Tuesday, March 10, 2020
Saturday, March 7, 2020
Subscribe to:
Posts (Atom)