Sisi binadamu huwa tunasumbuka na mambo mengi sana, lakini tukianza
kuyaangalia mambo hayo, mengi tunajisumbua nayo bure, kwa sababu yapo
nje ya uwezo wetu, hakuna chochote tunachoweza kufanya tukayabadili au
kuyaathiri.
Mambo yote yanayotokea kwenye maisha yetu tunaweza kuyagawa kwenye
makundi mawili, yaliyo ndani ya uwezo wetu, haya ni yale ambayo tunaweza
kuyaathiri, tunaweza kuyafanya kuwa bora zaidi. Na kuna yale ambayo
yapo nje ya uwezo wetu, ambapo hatuna cha kufanya.
Baadhi ya vitu vipo ndani ya uwezo wetu na vingine vipo nje ya uwezo
wetu. Vilivyo ndani ya uwezo wetu ni maoni yetu, fikra zetu, maamuzi
yetu na matendo yetu, kwa kifupi yale yote ambayo sisi tunayafanya. Vitu
vilivyo nje ya uwezo wetu ni miili yetu, mali zetu, sifa zetu na nafasi
nyingine tunazopewa, kwa kifupi chochote ambacho hatufanyi sisi moja
kwa moja, kipo nje ya uwezo wetu. Vitu vilivyo ndani ya uwezo wetu ni
bure, huru na visivyo na ukomo, vilivyo nje ya uwezo wetu ni dhaifu,
visivyo huru, vyenye ukomo na visivyo vyetu.
Kwa vyovyote vile, hupaswi kusumbuliwa na chochote, kwa sababu kama
kitu kipo ndani ya uwezo wako basi unahitaji kuchukua hatua, na kama
kipo ndani ya uwezo wako huna hatua ya kuchukua hivyo kubaliana nacho
kama kilivyo au kipuuze.
No comments:
Post a Comment